Sunday, November 18, 2012

DEREVA WA PAROKO ALIYEPIGWA NA MAJAMBAZI AHUSISHWA NA SAKATA HILO


Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, Wiliam Lukuvi (Katikati) akimjulia hali Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Isimani mkoani Iringa, Angelo Burgio wakati alipomtembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa jana. Picha na Mpiga Picha wetu. 


IDADI ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ujambazi katika matukio mawili tofauti kwenye Parokia za Kanisa Katoliki za Kihsesa na Isimani mkoani Iringa imeongezeka na kufikia nane huku mmoja wa watu waliokamatwa akiwa ni Dereva wa Paroko wa Parokia ya Isimani, Padri Angelo Burgio.
Tukio hilo ambalo lilisababisha mapadri wawili wa Parokia ya Isimani ambao ni Paroko wa Kanisa hilo Padri Burgio na msaidizi wake Padri Herman Myala na mlinzi wa Parokia ya Kihesa, Batholomeo Nzigilwa kujeruhiwa na kulazwa katika hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa lilitokea usiku wa Novemba 15 na 16 mwaka huu.
Akitaja orodha hiyo mpya huku akisisitiza kuwa msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Dereva wa Paroko huyo ambaye hivi karibuni ndiye aliyemsindikiza kwenda kuchukua fedha Benki.
“Idadi ya watuhumiwa hadi sasa imefikia 8 na kati ya watuhumiwa wanne waliokamtwa jana katika msako unaoendelea hivi sasa mmoja wao ni Dereva Baba Paroko na ndiye aliyempeleka hivi karibuni kwenda Iringa Mjini kuchukua fedha,” alisema Kamuhanda.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali imesema vitendo vya uvamizi wa Parokia za Kanisa Katoliki za mkoani Iringa hauna uhusino na migogoro yoyote ya kidini inayoendelea nchini bali wahusika walifanya tendo hilo kwa tamaa ya kujitatia utajiri wa haraka.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mapadri waliojeruhiwa kwa kwa risasi na mapanga wa Parokia ya Isimani mkoani Iringa Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Mbunge William Lukuvi  alisema Serikali imejipanga kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu hasa vinavyofanyika katika maeneo wanakoishi mapadri wakigeni.
“Serikali itahakikisha inaimarisha ulinzi hususani katika maeneo wanakoshi wamisionari kutokana na watu kujenga dhana kuwa kila anapoishi mzungu huenda kuna fedha ama mali wanazoweza kujipatia kwa nguvu kama walivyowafanyia mapadre wa Isimani,” alisema Lukuvi.
Pia wazili Lukuvi alilitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kutoa mafunzo maalumu kwa watu wanaofanya kazi za ulinzi kwenye nyumba zote za misheni wanazoishi mapadri wawe na mbinu za kuwabaini kwa haraka majambazi na kuwadhibiti kabla ya kusababisha  madhara.
"Hawa walinzi ambao wanalinda maeneo mbalimbali katika misheni, taasisi na maeneo mengine wanatakiwa wapewe mafunzo ya ulinzi ili amani iwe ya kuaminika katika maeneo hayo… jeshi la polisi kwa sasa wajipange ili watoe mafunzo hayo kwa mfumo huo tunaweza kuzuia matukio ya wizi na  watu kuvamiwa," alisema  Lukuvi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hosptali hiyo, Dk Faustine Gwanchele alisema afya ya mapadri hao akiwemo Paroko Burgio aliyefanyiwa upasuaji na kutolewa risasi tano mwilini inaendelea vizuri.
“Kwa sasa hali ya Padri Burgio inaendelea vizuri baada ya kumfanyia upasuaji na kutoa risasi tano mwilini mwake, pia hali ya Padri Hermani aliyecharangwa kwa mapanga inaendela vizuri isipokuwa mlinzi aliyepigwa kichwani katika Parokia ya Kihesa, Botholomeo Nzigilwa hali yake ni mbaya na tumempatia rufaa ya kwenda Muhimbili,” alisema Dk Gwanchele.
Akizungumzia tukio hilo akiwa hospitalini alipolazwa Padri Myala (36) ambaye ni msaidizi wa Paroko wa Parokio hiyo alisema majambazi walikuwa na mwenyeji kwani walionyesha wanajua kila kona ya majengo ya Parokia hiyo.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...