Wednesday, November 14, 2012

HUKU TIMU YA TAIFA YA TANZANIA LEO ITAKUA INAJIPIMA NGUVU YA HARAMBEE STARS KUJIANDA NA MICHUANO YA CHALENJI, TANZANIA ITATUPA KARATA YAKE YA KWANZA KWA KUANZA NA SUDAN CHALENJI

 
 Kocha wa Kilimanjaro Stars,  Kim Poulsen 
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' imetupwa kundi B pamoja na timu za Sudan, Burundi na Somalia katika mashindano ya Chalenji yatakayofanyika Kampala, Uganda kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 8.

Jana Baraza la Vyama vya Soka la Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) lilitangaza makundi matatu ya timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo kupitia droo iliyofanyika jijini Kampala.

Wenyeji Uganda wamepangwa Kundi A wakiwa na mahasimu wao kisiasa Kenya pamoja na timu za Ethiopia na Sudan ya Kusini.

Uganda na Kenya mara kadhaa zilijikuta katika mzozo uliotokana na kila moja kudai ndiye mmiliki halali wa kisiwa cha Migingo.

Nao ndugu wa Kilimanjaro, timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' imesukumwa Kundi C ikiwa pamoja na timu za Rwanda, Eritrea na Malawi.

Akizungumzia nafasi ya kikosi chake, kocha wa Kilimanjaro Stars,  Kim Poulsen alisema,"Sudan inaoongoza katika viwango vya ubora duniani katika kundi letu, Burundi inafuatia na sisi tunashika ya tatu wakati Somalia inashika nafasi ya nne, kwa hiyo utaona hapa hakuna timu ya kubeza hata moja."

Alisema,"ninachokifanya ni kuiandaa timu yangu kwa ajili ya kwenda kupambamba na kupata matokeo mazuri."

Poulsen alisema,"tunacheza na Kenya, nitaangalia kama kuna mapungufu niyafanyie kazi, nadhani baada mechi hiyo tutakuwa na siku nyingine kama kumi hivi za kujiandaa zaidi kabla ya kwenda Kampala."

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mechi mbili zitapigwa siku ya ufunguzi wa mashindano hayo zikihusisha timu kutoka kundi A.

Katika pambano la kwanza Ethiopia itavaana na majirani zao Sudan ya Kusini katika pambano litakalofanyika saa 9 alasiri na kufuatiwa na lile la wenyeji Uganda watakaocheza na Kenya baadaye jioni.

Pia, ratiba hiyo inaonyesha kuwa mechi mbili zitapigwa kila siku katika siku za wiki na nne kwa siku za mwishoni mwa wiki.

Wakati huohuo, Kamati ya ulinzi na usalama ya Chama cha Soka mkoani Mwanza (MZFA) jana imekutana ili kupanga mikakati ya kuhakikisha mechi ya kirafiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' dhidi ya Kenya inamalizika kwa amani na utulivu.

Timu hizo mbili zitashuka uwanjani kesho katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambako Taifa Stars imeweka kambi yake ya kujiandaa na mashindano ya Chalenji yatakayofanyika Kampala, Uganda.

Akizungumza na Mwananchi jana Katibu mkuu wa MZFA, Nasib Mabruki alisema kuwa lengo kubwa la chama hicho kukutana na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama jana ni kupanga mikakati ya kuhakikisha mechi hiyo inamalizika kwa amani na utulivu ili Shirikisho la Soka Tanzania 'TFF' lishawishike siku nyingine kuukumbuka mkoa huo.

"Maandalizi ya mechi hiyo kwa hakika yanaendelea vizuri, uongozi wetu wa MZFA kwa kushirikiana na TFF tumejipanga vilivyo, ambapo Kamati yetu ya mkoa ya Ulinzi na Usalama leo (jana) imekutana na kupanga mikakati itakayosaidia mchezo huo kumalizika kwa amani,"alisema Mabruki.

Alisema,"tumejipanga kuhakikisha tunaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya uwanjani na sehemu zitakazotumika kwa ajili ya kuuza tiketi ikiwa ni pamoja na hoteli ambazo timu zote mbili zimefikia."

Alisema mbali na kamati hiyo kujadili suala zima la ulinzi na usalama pia viingilio vya mechi hiyo vilitangazwa, ambapo jukwaa kuu ni sh 15,000, mzunguko sh 5,000 na tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa leo mjini Mwanza.
Makundi
Kundi  A: Uganda, Kenya, Ethiopia, Sudan.
Kundi  B: Sudan, Tanzania, Burundi, Somalia
Kundi  C: Rwanda, Zanzibar, Eritrea, Malawi.

Ratiba

Kundi A

Novemba 24:  Ethiopia v Sudan: Uganda v Kenya
Novemba 27: South Sudan v Kenya: Uganda v Ethiopia
Novemba 30: Kenya v Ethiopia: South Sudan v Uganda

Kundi B
Novemba 25: Burundi v Somalia: Tanzania v Sudan
Novemba 28: Somalia v Sudan: Tanzania v Burundi
Decemba 1: Sudan v Burundi: Somalia v Tanzania

Kundi C
Novemba 26: Zanzibar v Eritrea: Rwanda v Malawi
Novemba 29: Malawi v Eritrea: Rwanda v Zanzibar
Desemba 1: Malawi v Zanzibar: Eritrea v Rwanda

Robo fainali: Desemba 3 na 4
Nusu fainali: Desemba 6
Fainali: Desemba 8.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...