Sunday, November 11, 2012

Kikwete amlilia Askofu Balina

Asema kifo chake ni pigo katika sekta za afya na elimu nchini
Rais Jakaya Kikwete akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Rais Jakaya Kikwete, amesema kifo cha aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Aloysius Balina, kimeacha pengo si kwa kanisa pekee bali kwenye sekta za elimu na afya nchini.
Akizungumza katika ibada ya mazishi iliyofanyika Ijumaa wiki hii alisema hayati Askofu Balina alikuwa rafiki yake kwa siku nyingi na kuongeza kuwa kabla ya kifo chake walikuwa wakiwasiliana kwa simu akiwa hospitalini Bugando.
Askofu Balina alifariki Jumanne wiki hii katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza, baada ya kusumbuliwa na saratani ya ini na kisukari.
Rais alikuwa akitoa salamu za serikali katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo mjini Shinyanga.
Pamoja naye alikuwepo Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa na Mama Maria Nyerere, Mawaziri wa Mambo ya Nje Bernad Membe na wa Ujenzi Dk. John Magufuli, wabunge , viongozi wa dini na waumini.
Rais Kikwete alimsifu Balina kuwa tangu alipopata upadirisho mwaka 1971 alikuwa kiongozi madhubuti wa kiroho, asiyebagua na alikuwa mwadilifu katika shughuli zake .
Akieleza zaidi alisema Askofu huyo aliisadia serikali katika masuala mengi yanayohusu afya na elimu huku akishirikiana kutafuta wafadhili wa ndani na nje kwa kukisaidia Chuo Kikuu cha Afya Bugando.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Tarsius Ngalalekumtwa, alisema kifo cha Askofu Balina , kimewahuzunisha kwani alijitoa kwa ajili ya TEC na kwa Watanzania .
Alisema Balina alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Kanisa Katoliki na Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Fedha ya Shirika la Maendeleo la Kanisa Katoliki (CARITAS).
Alimueleza kama kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kupamba na Ukimwi na mtumishi wa Jimbo la Shinyanga na taifa kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisco Padilia, aliwapa pole Wakatoliki wa Jimbo la Shinyanga na Geita na kusema Baba Mtakatifu Papa Bendictor wa 16 amemteuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mwanza Thadeus Rwaichi kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo la Shinyanga kwa sasa mpaka atakapomteua askofu mwingine.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...