Monday, November 19, 2012

Mrabaha wa dola 200,000 wawagawa madiwani


MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Geita wametofautia na madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Geita vijijini kuhusiana na mgawanyo wa mrabaha wa madini wa dola 200,000  za Marekani unaotolewa na Kampuni ya uwekezaji ya Mgodi wa dhahabu wa Geita[GGM] kila mwaka.
Hatua hiyo imekuja kutokana na madiwani hao kuonyesha msimamo wao kwa kuitaka halmashauri ya Geita Vijijini kuacha kuingilia rasilimali zilizomo ndani ya Mji wa Geita ikiwemo fedha inayotolewa na GGM.
Madiwani hao kupitia kikao cha baraza kilichofanyika Novemba 16,mwaka  huu katika ukumbi wa GEDECO walisema haiwezekani fedha inayotokana na mrabaha wa madini ikagawiwa kwa asilimia sawa wakati asilimia 100 ya Mgodi wa Geita  umo ndani ya halmashauri ya mji wa Geita.
Msimamo wa madiwani hao umekuja siku chache baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuanzishwa halmashauri hizo mbili ambapo katika kikao cha hivi karibuni madiwani hao walishindwa kuelewana kuhusu mgawanyo huo.
Hatua hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula kuingilia kati na kuwataka madiwani hao waliovutana kwa muda wa saa moja,kuunda kamati ndogo ya kufuatilia takwimu na mipaka halisi ya Mji wa Geita, kauli iliyoungwa mkono na madiwani hao na hivyo kulazimika kuwateuwa madiwani sita na wataalamu wa wilaya na mkoa kufuatilia suala hilo.
Mvutano huo wa madiwani uliibuka Novemba 7,mwaka huu muda mfupi baada ya Ofisa Utumishi, Charles Kimaro kusoma taarifa ya mgawanyo wa rasilimali ya mgodi,ambapo taarifa hiyo ilionyesha kwamba asilimia 70 ya mrabaha wa madini unabaki halmsahuri ya Wilaya ya Geita vijijini na asilimia 30 unabaki Halmashauri ya Mji wa Geita , licha ya mgodi huo kuwa ndani ya Mji wa Geita kwa asilimia 100.
Madiwani hao wa mji wamedai kutokuwa na imani na kamati hiyo iliyoundwa ambayo wameitilia mashaka kuwa huenda ikapindisha ukweli halisi wa mgawanyo wa mrabaha huo kwa kuwa halmashauri ya Geita Vijijini ina nguvu na ina watalaamu waliobobea.
Diwani wa kata ya Mtakuja ,Hirolius Buchuma alitoa angalizo kwa madiwani wenzake na kuomba suala hilo lijadiliwe kisheria ili kutenda haki kwa pande zote mbili za halmashauri hizo,huku diwani wa viti maalumu, Zaituni Fundikira akiweka msimamo wake  kwamba rasilimali zote za mji wa Geita zinabaki katika mji huo.
Kauli hiyo ya Fundikira iliungwa mkono na Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Geita, Martine Kwilasa ambaye alisema mrabaha huo wa madini unabaki katika mji wa Geita na kuongeza kuwa hata rasilimali zingine zilizomo ndani ya mji huo zifuatiliwe kuhahakikisha zinabaki mikononi mwa mji huo.
Msimamo huo ulitokana na mjadala wa madiwani baada ya mkurugenzi,  Margareth Nakainga kuwasilisha taarifa ya mgawanyo wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo madiwani hao walidai kuwa hawakutendewa haki katika mgawanyo huo mbali na kubaini kwamba kati ya magari 27 yaliyokuwapo  wametengewa magari 4 ambayo wamedaiwa hayakidhi utendaji wao.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...