Wednesday, November 14, 2012

MWANAFUNZI AJIUA KWA KITANZI( MUCCOBS) MOSHI

MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara cha Moshi (Muccobs), mkoani Kilimanjaro, amejiua kwa kujinyonga.

Mwanafunzi huyo, Samson Bena (24), alijinyonga usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alilithibitishia gazeti hili  jana kuhusu tukio hilo na kwamba mwili wa marehemu ulikutwa ikining’inia juu ya  mti katika Kijiji cha Uru Timbirini, Moshi Vijijini.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, polisi wameanzisha uchunguzi wa kubaini kiini cha kijana huyo kujinyonga.

Wakati wa uhai wake, kijana huyo alikuwa  anasomea shahada ya sanaa katika Menejimenti ya Taasisi ndogo za fedha.
Habari zilisema wananchi wa eneo la mwisho wa lami katika Kijiji cha Uru Timbirini, ndio waliougundua mwili wa mwanafunzi huyo ukining’inia juu ya mti.
Baadaye walitoa taarifa polisi na kufuatiwa na hatua ya askari kwenda katika eneo la tukio na kuushusha mwili na kisha kuupeleka chuoni ambako  wanafunzi walimtambua mwanafunzi mwenzao.

Habari zilisema baadaye, mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Mawenzi, ambako umehifadhiwa ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.
Hili ni tukio la pili kwa mwanafunzi wa Muccobs, kukutwa akiwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha.

Oktoba  mwaka juzi, mwanafunzi  Lucy Genge (20) aliuawa kikatili baada ya kubakwa na kundi la watu wasiojulikana.

Maiti yake ilitupwa kwenye kichaka kidogo kilichokuwa umbali wa meta 100 kutoka katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa Kilimanjaro na kugunduliwa na wapita njia saa 6:00 mchana.

Marehemu ndio kwanza alikuwa amemaliza kozi ya cheti katika fani ya Utawala na Uhasibu.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...