Tuesday, November 27, 2012

Serikali yasema Mwafaka kati yetu na Malawi bado unawezekana


Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wakipeana mikono na Rais wa Malawi Joyce Banda 

Rais Jakaya Kikwete amerudisha matumaini yaliyokuwa yamepotea baada ya kusema kwamba siyo kweli kwamba mazungumzo kati ya Malawi na Tanzania yameshindikana. Rais alisema mgogoro huo wa mpaka katika Ziwa Nyasa hautapelekwa katika jopo la viongozi wastaafu wanaoshughulikia migogoro ya nchi mbalimbali barani Afrika kwa usuluhishi.
Taarifa za awali zilizokuwa zimechapishwa na kutangazwa katika vyombo vya habari nchini zilisema mgogoro huo ungepelekwa kwa viongozi hao wastaafu baada ya nchi hizo kudaiwa kushindwa kuafikiana katika mazungumzo yaliyomalizika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita na kuwakutanisha mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hizo mbili ambao walifuatana na maafisa wa juu wa serikali hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe alikaririwa na vyombo hivyo vya habari akidaiwa kusema kwamba pande zote mbili zilikuwa na matumaini kwamba viongozi hao wastaafu wangesaidia kumaliza tatizo hilo. Hata hivyo, Membe alikuwa amewaeleza waandishi wa habari kuwa, Ziwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu za Tanzania, Malawi na Msumbiji na kwamba siyo sahihi kwa upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa hilo.
Tumetiwa moyo na kauli ya Rais Kikwete kwamba mgogoro huo bado unazungumzika na kwamba nchi hizo mbili bado zinao uwezo wa kumaliza tatizo hilo pasipo kuhitaji wasuluhishi kutoka nje. Hata hivyo, tungependa kutoa angalizo kwa Serikali yetu kwamba mgogoro huo wa mpaka kati yetu na Malawi sasa umeingia katika hatua nyeti na muhimu, hivyo kauli zote zinazohusu mgogoro huo lazima zitolewe kwa tahadhari kubwa ili kuepuka kuupa upande wa pili kisingizio cha kujitoa katika usuluhishi huo.
Kama tulivyoshuhudia mwenendo wa mgogoro huo huko nyuma, baadhi ya kauli za viongozi wetu hakika zilionekana kuchochea kuvunjika kwa mazungumzo hayo kwa sababu upande wa pili ulihisi Tanzania haikuwa na dhamira ya kupata mwafaka wa mgogoro huo.
Tunachotaka kusema hapa ni kuwa, pamoja na ukweli kwamba Serikali ina kila sababu za kupinga hatua ya Malawi kudai kwamba eneo lote la Ziwa Nyasa liko katika himaya yake, Serikali yetu hiyo iache kutumia vyombo vya habari kuelekeza lawama upande wa pili. Kama alivyosema Rais Kikwete, Serikali lazima ithamini vikao vya usuluhishi.
Pamoja na kauli hiyo ya Rais, tungependa kushauri kwamba Serikali itafanya vyema kwa kutambua kuwa, huu sasa ni wakati wa kutumia mbinu za kidiplomasia kuzishawishi nchi marafiki na jumuiya ya kimataifa kwa jumla kwamba mpaka kati ya nchi hizo mbili uko katikati ya ziwa hilo. Tunasema hivyo kwa kuwa, Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa katika mgogoro huo, kutokana na ukweli kwamba tangu uhuru imekuwa na sera ambazo siyo tu zimeifanya iwe kisima cha amani na kimbilio la wanyonge duniani kote, bali pia imekuwa moja ya nchi chache zinazoendelea ambayo imekoga nyoyo za jumuiya ya kimataifa kama mfano wa kuigwa.
Tunapendekeza pia kuwa, Serikali ibuni mkakati wa kidiplomasia kwa kuwatumia mabalozi wake na wasomi waliobobea kupeleka hoja zake kwa nchi na jumuiya mbalimbali zenye ushawishi, lengo likiwa ni kutaka msimamo wetu uiridhishe dunia kwamba hakika mpaka wetu na Malawi uko katikati ya ziwa hilo.
Sisi tunadhani kwamba Serikali haijachelewa kufanya hivyo. Jambo muhimu ni kwa viongozi wetu kutambua kuwa, katika wakati tuliomo mchakato wa usuluhishi na upatanishi wa migogoro una taratibu zake na kwamba siasa za diplomasia ya kimataifa haziendeshwi kwa fujo, kelele wala ubabe, bali kwa ushawishi na mashauriano miongoni mwa pande zote husika.
Ni matumaini yetu kwamba kupatikana kwa mafuta na gesi katika ziwa hilo hakutazifanya nchi zetu hizi majirani kutangaza uadui. Kauli ya Rais sasa inatupa matumaini mapya kwamba mgogoro huu utamalizika kwa njia ya maridhiano.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...