Monday, November 26, 2012

TANGA: Mwalimu aua Mwanafunzi kwa kisu

 
Wanafunzi wakiwa darasani huku wamekaa chini. 

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kwamwachalima, iliyopo katika Kijiji cha Kwamwachalima Kata ya Komkonga wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, ametoweka baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa mwanafunzi wa darasa la tatu na kumjeruhi vibaya mwingine wa kidato cha pili.
Mwalimu huyo, Suhalungi Nangoma (23) anatafutwa na Polisi kwa tuhuma hizo
za kuua na kujeruhi kwa kisu wanafunzi hao ambao ni ndugu, na watoto wa mwalimu mwenzake, Ijumaa Mjaliwa.
Nangoma anatuhumiwa kumuua kwa kumchoma kisu kifuani binti huyo anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo, Farihia Mjaliwa (9), kisha kumjeruhi kwa kumcharanga kisu tumboni  kaka wa binti huyo, Mohamed Farhia anayesoma kidato cha pili katika Sekondari Kisaza.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi wanaendelea kumsaka mtuhumiwa ili afikishwe mahakamani.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea saa 9:00 usiku Novemba 23, mwaka huu wakati mtuhumiwa alipowavamia watoto hao chumbani kwao na kuanza kuwashambulia kwa kisu. Baba mzazi wa watoto hao, Mjaliwa anafundisha shule moja ya Kwamwachalima anasema hawakuwahi kugombana.
Mtuhumiwa huyo ametenda kosa hilo huku akikabiliwa kesi ya kumpachika mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Kisaza.
Akisimulia mkasa uliowakuta watoto wake mbele ya mkuu wa wilaya, Mjaliwa alisema Mohamed ambaye alinusurika kifo, alichomwa kisu tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje na kwamba sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga.
Kwa mujibu wa Mjaliwa, mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho alimgeukia mdogo mtu na kisha kumchoma kisu kifuani upande wa kushoto na kukiacha kikining’inia.
“Watoto hao walianza kupiga kelele kutoka na mashambulizi hayo, lakini mtuhumiwa alitimua mbio na kukimbilia kusikojulikana,” alisema Mjaliwa ambaye hakuwepo siku ya tukio.
“Cha kushangaza alikuwa nje kwa dhamana kwa kumpa mimba mwanafunzi,” alisema.
Habari zinadai kuwa siku ya tukio, baadhi ya walimu wa Shule ya Kwamwachalima walifanya kikao kifupi kujadili jinsi ya kumwekea dhamana Nangoma, iwapo angefikishwa mahakamani kwa kesi ya kumpachika mwanafunzi mimba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Ali Hatibu, alisema walimhoji majeruhi huyo kabla hajapoteza fahamu na kumtaja mwalimu huyo kwamba ndiye aliyemchoma kisu.
“Tuliingia chumbani kwa watoto na kukuta kumetapakaa damu nyingi, lakini binti huyu ambaye sasa ni marehemu tulikuta tayari ameshafariki dunia na alikuwa ameshikilia kisu, maana alichomwa kwenye moyo,” alisema Hatibu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kwamwachalima, Eva Msenga alisema kwamba siku ya tukio mchana alizungumza na mtuhumiwa baada ya kuona mwenendo wake hauridhishi na kwamba alimjibu kwamba alikuwa amechanganyikiwa kutokana na kesi inayomkabili.
Msenga alisema baadaye jioni alikuwa na watoto hao wakijisomea hadi saa tatu usiku, na kwamba muda huo aliwataka wakalale kwani muda ulikuwa umekwenda.
“Tuliagana na waliondoka kwenda kulala, baadaye usiku ndipo tuliposikia tukio hili na tuliambiwa kwamba mtuhumiwa alibisha hodi na watoto kwa kumfahamu walimfungulia kisha akawafanyia unyama huo wa kutisha,” alisimulia Msenga.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...