Friday, November 30, 2012

UMOJA WA MATAIFA WAONGEZA VIKWAZO KWA M23

BARAZA Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa , limepitisha kwa kauli moja azimio linaloongeza muda wa vikwazo vya silaha na vikwazo vingine dhidi ya vikundi vya waasi ambavyo viko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

Azimio hilo nambari 2078 ( 2012) linaelezea pia haja ya kuongeza vikwazo vya ziada kwa uongozi na wapiganaji wa kundi la waasi la M23, kundi ambalo hivi karibuni lilichukua Jimbo la Goma.

Baraza Kuu la Usalama ambalo lilikutana siku ya Jumatano limeongeza muda huo wa vikwazo hadi Februari Mosi mwaka 2014.

Vikwazo dhidi ya silaha viliwekwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003 mara baada ya kumalizika kwa vita vya mara kwa mara nchini DRC, vita ambavyo vimedumu kwa miaka mitano na kukadiriwa kuua zaidi ya watu milioni tano.

Azimio hilo pia linalaani vikali kundi la waasi la M23, kundi ambalo linahusisha wanajeshi walioasi kutoka Jeshi la Kitaifa la DRC Aprili mwaka huu. Kundi ambalo kwa sasa linashikilia Goma, ambao ni Mji Mkuu wa Kivu ya Magharibi.

Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeagiza na kurudia tena kusitishwa mara moja kwa misaada ya aina yoyote kutoka nje inayoelekezwa kwa kundi la M23.

Wakati huohuo, Baraza Kuu la Usalama pia limemwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kukiongezea muda Kikundi cha Wataalamu kuhusu DRC, hadi Februari Mosi mwaka 2014 ili kiweze kufuatilia utekelezaji wa vikwazo hivyo.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa, umemtuma mshauri wake mkuu kuhusu masuala ya Kijeshi, Jenerali Babacar Gaye kwenda katika nchi za Maziwa Makuu ambako atakutana na kufanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala kadhaa yaliyojiri hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR).

Masuala hayo ni pamoja na utekelezaji wa kilomita 20 za Ukanda Huru ( Neutral Zone )eneo ambalo M23 litatakiwa kuondoka, na dhana ya kuwa na Jeshi la Kimataifa lisilofungamana na upande wowote.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...