Wednesday, November 14, 2012

VIONGOZI WANAOKWEPA KUJAZA FOMU ZINAZONESHA UTAJIRI WAO KUBANWA HAPA

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma jana ilitangaza kuziweka fomu za kujazwa na viongozi wa umma kwenye tovuti  ili kuondoa visingizio vya kukosa fomu.

Imesema kuanza sasa viongozi wote watapata fomu kupitia tovuti  ya  HYPERLINK "http://www.ethicssecreriat.go.tz" www.ethicssecreriat.go.tz na kuzijaza kwa muda mwafaka uliopangwa kisheria.

Alisema lengo ni  kuwabana viongozi wanaokwepa kutangaza mali zao kwa visingizio vya kutopelekewa fomu baada ya kuanzisha utaratibu mpya wa kuziweka katika tovuti.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wengi waliokuwa wakifikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za kutojaza fomu za kueleza mali wanazomiliki kujitetea kwamba walikuwa hawajapata fomu hizo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda alisema visingizio hivyo havitakuwapo baada ya kuzindua tovuti yao.

Mwaka 2011 viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge waliofikishwa mbele ya Baraza la Maadili walijitetea kwamba mfumo mzima wa usambazaji wa fomu hizo ulikuwa na kasoro kwa sababu wengi hawakuzipata.

Lakini jana, Jaji Kaganda alisema fomu hizo zimeshawekwa kwenye tovuti ya sekretarieti hiyo na kwamba viongozi wote wanatakiwa kuzichukua na kuzijaza.

“ Vile visingizio vilivyokuwa vinatolewa zamani vya viongozi kutozipata fomu hizo sasa havitatolewa tena, chukueni fomu hizo, jazeni na kuzirudisha kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Jaji Kaganda.

Alisema viongozi hao wanatakiwa kuzijaza fomu hizo na kuzirejesha katika Sekretarieti hiyo kabla ya Desemba 31 mwaka huu vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria .
Jaji Kaganda alisema njia hiyo ya kuweka fomu katika tovuti hiyo itawarahisishia viongozi kuweka wazi mali na madeni waliyonayo.

Alisema sheria inawataka viongozi kutangaza mali na madeni yao mara tu wanapopata nafasi za uongozi.

“Baada ya kupata uongozi kila mwaka wanatakiwa kujaza fomu za mali na madeni ili sekretarieti iweze kufahamu wanachokimiliki na wanachodaiwa,” alisema.

Akizungumzia tovuti hiyo, Kaganda alisema itakuwa na taarifa muhimu zitakazowapa fursa wananchi kufahamu sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Alisema tovuti hiyo itarahisisha mawasiliano ya haraka na usiri baina ya watumishi wa sekretarieti  na viongozi.

Alisema pia katika tovuti hiyo kuna fomu za malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi wao ambazo zitatakiwa kujazwa na kupelekwa katika sekretarieti.
“ Kwa hiyo wananchi wanaweza kutuletea malalamiko yao dhidi ya viongozi wao, tunaomba wananchi waitumie tovuti hii,” alisema Jaji Kaganda.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...