Sunday, November 11, 2012

Wachezaji Yanga waibua mambo mapya Simba



SIMBA inacheza na Toto African leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Mwanza lakini mastaa wawili wa Yanga, Mbuyu Twite na Kelvin Yondani wameibua mambo makubwa Msimbazi kwani Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' anaweza kubwaga manyanga baada ya mchezo huo.

Ingawa Kaburu hakutaka kutoa ufafanuzi wowote kwa Mwanaspoti jana Ijumaa na uongozi ukisema haujapata taarifa zozote, lakini habari za ndani zinasema huenda akatangaza rasmi kujiuzulu Simba baada ya mechi ya Toto African bila kujali matokeo ya mchezo huo kwa kuwa amekuwa akiandamwa sana na maadui zake.

Mwanaspoti linajua kwamba Kaburu aliyekuwa akihifadhi mabasi ya Simba aliyakabidhi yote matatu kwa uongozi juzi Alhamisi jioni kwenye Uwanja wa Kinesi wakati Simba ilipokuwa ikifanya mazoezi na nyaraka nyingine za ofisi.

Ameendelea kukabidhi vitu huku ikidaiwa kuwa amekuwa akipokea vitisho vya hapa na pale kutoka kwa mashabiki wa Simba.

VITISHO
Mmoja wa viongozi wa Simba aliiambia Mwanaspoti kuwa baadhi ya wanachama wa Simba walifika eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam anakofanya kazi Kaburu na kumweleza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni anayofanya kazi (jina tunalo) kwamba amshauri Kaburu aachane haraka na Simba.
Alisema mkurugenzi huyo alikaa na Kaburu na kumshauri arudishe mali za Simba ikiwamo mabasi aliyokuwa ameyahifadhi kama kiongozi na aachane na uongozi huo kwa kuwa hali si nzuri.
Jioni yake siku ya Alhamisi (juzi), Kaburu alipiga simu na kuyapeleka mabasi yote matatu Coaster, Hiace na basi kubwa kwa viongozi wenzake na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji maarufu kama Mzee Kinesi aliyapokea Uwanja wa Kinesi na kuyahifadhi. Jambo ambalo liliibua gumzo mazoezini huku mashabiki wakiimba nyimbo za kumkejeli Kaburu.

WAASI
Habari za ndani zinadai kuwa baadhi ya wajumbe wa Friends of Simba wanatumia tawi moja maarufu la Wilaya ya Kinondoni kuzungusha fomu kwenye matawi mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoani kupata majina ya wanachama 700 ili kupiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi ili uitishwe mkutano mkuu wa dharura.

"Tunazunguka kwenye matawi ya Dar es Salaam, kukusanya saini za wanachama 700 ili kuitisha mkutano kwa nia ya kuupindua uongozi. Wanaonekana kupata sapoti lakini kwenye baadhi ya matawi wanatimuliwa kwa kuwa watu wengine hawaoni sababu ya kufanya hivyo," alidokeza kiongozi mmoja wa juu wa tawi linalofanya kampeni.

Hoja kubwa wanazotumia kushawishi wenzao ni nne. Mosi, ahadi zisizotekelezeka zinazotoka kwenye uongozi.
Pili, suala la Kelvin Yondani kwenda Yanga kirahisi na kuiachia Simba matatizo kwenye beki.

Tatu, kukubali kushindwa na kutorudishwa fedha za kumsajili Mbuyu Twite. Nne, Simba kushindwa kutekeleza ujenzi wa uwanja mpya ambao wanachama walichangishwa fedha katika Mkutano Mkuu Mei mwaka huu.

KASHESHE LA AZAM
Suala la Azam kuituhumu Simba kuhonga wachezaji wake watatu mabeki Said Morad na Erasto Nyoni pamoja na kipa Deo Munishi limeibua kasheshe Msimbazi kwani baadhi ya viongozi wameanza kuwa na wasiwasi.

Azam inaituhumu Simba kwamba ilihonga wachezaji ndiyo maana wakaishinda mabao 3-1 katika Uwanja wa Taifa hivi karibuni. Azam wamesisitiza kuwa wana ushahidi wa kutosha kuhusiana na sakata hilo jambo ambalo limewatia hofu baadhi ya vigogo wa Simba kwani Azam imeapa kutumia gharama yoyote kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili ukweli ubainike.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...