Saturday, January 19, 2013

MAELFU YA WAKAZI WA MTWARA WAJIANDIKISHA KUPINGA GESI KUPELEKA DARE SALAAM, NINI MTAZAMO WAKO MSOMAJI WETU?

 
SAKATA la kupinga ujenzi wa bomba la gesi inayovunwa katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, limechukua sura mpya baada ya maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara kujiandikisha katika fomu maalumu kupinga mradi huo.
Tayari majina hayo yamekabidhiwa kwa Katibu wa Wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya kwa ajili ya kuyawasilisha bungeni kama kielelezo halali cha wananchi hao kupinga mradi huo, ambapo utaratibu wa wananchi hao kujiorodhesha uliandaliwa na chama hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa zaidi ya wakazi 30,000 wa Mtwara wamejiorodhesha kupinga mradi huo wa gesi.
Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka wilaya zote tano ya mkoa huo, ambao hawakujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Watu wa kada mbalimbali waliliambia Mwananchi Jumapili kwamba haijawahi kutokea umati mkubwa wa watu kuhudhuria mkutano wa hadhara mkoani humo kama ilivyokuwa kwa mkutano wa jana.
Walisema kuwa idadi hiyo ya watu ni zaidi ya waliojitokeza katika maandamano ya kupinga mradi huo, yaliyofanyika Desemba 27 mwaka jana.
Majina hayo yalikabidhiwa na makatibu wa CUF wa wilaya za mkoani huo  huku mwakilishi wao Saidi Kulaga, akisema kuwa zaidi ya watu 30,000 wamejiandikisha kupinga mradi huo.
Alisema wananchi hao wanataka Serikali kujenga mitambo ya kufua umeme  mkoani humo, ili kuinua uchumi wa mikoa ya kusini.
“Kwa niaba ya wananchi hawa na mbele yao,  nakukabidhi majina na  sahihi zao, wakipinga mradi wa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam. Wazee wetu waliwaondoa wanyonyaji weupe, sasa ni zamu ya vijana kuwaondoa wanyonyaji weusi,”  alisema Kulaga huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akipokea fomu hizo, Sakaya alisema kuwa wabunge wa CUF, wamesikia kilio cha wananchi wa Mtwara na kwamba watahakikisha wanawasilisha katika Bunge lijalo.
Katika mkutano huo mabango kadhaa yalibebwa na baadhi yakisomeka: “Shemejiii gesi haitoki…: Kikwete tuachie gesi yetu.”
Kabla ya mkutano kuanza umeme ulikatika eneo hilo hali  iliyosababisha kundi la vijana kuivamia Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mkoani humo wakiishinikiza urudishwe, kitendo kilichowalazimu polisi kuingilia kati na kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi hao.
Wananchi waliondoka eneo la ofisi hizo na kurudi uwanja wa mkutano, ambapo baadaye na mkutano huo uliendelea kwa  amani na utulivu, huku polisi wakiwa katika tahadhari kubwa.
Kabla ya kutoa hotuba yake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro aliwalisha kiapo viongozi na wananchi waliohudhuria mkutano huo, kikiwataka kutorudi nyuma na kudai gesi hadi mwisho.
“Katibu wa wabunge na wabunge wote wa CUF, nawaagiza hakikisheni hoja hii ya wananchi mnaifikisha bungeni na kuitetea,  vinginevyo chama hakitawaelewa,”alisema Mtatiro.
Tukio hilo linatokea wakati jana Waislamu walifanya dua maalumu ya kumwomba Mwenyezi Mungu kutia wepesi hoja yao ya kutaka gesi ibaki Mtwara na kuwalaani wale wote wanaotaka rasilimali hiyo iondoke.
Hata hivyo, katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa CUF, Katani Katani alitoa taarifa kwamba moja ya gari lililokuwa limebeba wananchi kutoka Tandahimba kwenda kwenye mkutano huo limepinduka na watu kadhaa wamejeruhiwa.
Katika siku za karibuni, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na taasisi mbalimbali wamekuwa wakizungumzia suala la gesi, huku wakishinikiza wananchi kuwa wasikubali gesi hiyo isafirishwe kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na baadaye mikoa mingine.
Hatua hiyo ilisababisha kufanyika maandamano Desemba 27, mwaka jana yaliandaliwa na kupokewa na viongozi wa vyama tisa vya upinzani na asasi kadhaa zisizo za kiserikali yalikuwa na mabango kadhaa yenye ujumbe wa kupinga hatua hiyo ya Serikali kusafirisha gesi hiyo.
Akizungumza wakati alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini, anayemaliza muda wake Dianne Corner aliyekwenda Ikulu Januari 15 kumuaga, Rais Jakaya Kikwete alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia rasilimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha wananchi.
Baada ya maandamano hayo ya Desemba 27,2012, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema: “Nina wasiwasi na elimu ya hawa wanaoshabikia hii gesi bila kufahamu. Ninawataka kwanza warudi tena shuleni, wanachokifanya kuchochea wananchi na wananchi wanachofanya ni upuuzi tu.”

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...