Thursday, February 7, 2013

TAIFA STARS YAFANYA KILE WALICHO KITEGEMEA WATANZANIA, SAMATTA AUTHIBITISHIA UMA WA WATANZANIA KUWA YEYE NI MZALENDO

 

TAIFA Stars jana ilifanya kile kilichosubiriwa na mashabiki wa soka Tanzania baada ya kuitia ‘adabu’ Cameroon kwa kuichapa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, shukrani kwa bao la ‘jioni’ kutoka kwa mshambuliaji wa kimataifa Mbwana Samata.

Samata anayecheza soka la kulipwa TP Mazembe ya DRC, alifunga bao hilo muhimu kwenye Uwanja wa Taifa dakika ya 89 baada ya kuusukumiza wavuni kirahisi mpira wa krosi ya Frank Domayo uliompita kipa wa Cameroon, Offala Komguep.

Bao la Samata lilikuja baada ya Stars inayoshika nafasi ya 124 kwa ubora wa viwango vya soka kufanya mashambulizi yasiyo na idadi lango kwa Cameroon.
Dakika 20 za mwisho wa kipindi cha kwanza, Cameroon haikuwa mchezo na badala yake jezi za rangi ya bluu ndizo zilizokuwa zikimili mpira.

Ni ushindi wa kwanza kwa Stars dhidi ya Cameroon, kwani matokeo mazuri waliyowahi kupata ni sare moja ya bila kufungana kwenye uwanja huohuo, na kisha kukubali kipigo cha mabao 2-1 nchini Cameroon.
Stars wangeweza kupata bao la kuongoza kipindi cha kwanza kama siyo beki Erasto Nyoni kushindwa kufunga penalti iliyochezwa na kipa.
Mechi hiyo ilianza taratibu na dakika 10 za kwanza zilionekana kama za wachezaji wa pande zote kusomana kimchezo.

Wenyeji Stars walitumia mfumo wa kushambulia pamoja na kukaba kwa pamoja kama alivyosema Kocha Poulsen kabla ya mchezo huo.
Cameroon, mabingwa wa zamani wa Mataifa ya Afrika, hawakuonekana kuwa wakali kama ambavyo mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walitarajia.

Stars ikitumia mfumo wa 4-3-3, ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini hata hivyo Cameroon ndiyo walitawala mchezo, huku wakitumia mfumo wa 4-3-4.
Dakika ya 19, mpira ulisimama kwa muda baada ya kipa wa Stars Juma Kaseja kuumia kufuatia kugongana na Tchami Herve wa Cameroon.

Mabeki wa Stars,Aggrey Morris na Kelvin Yondan walifanya kazi ya ziada kuwazuia washambuliaji wa Cameroon sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza.

Cameroon waliokuwa wakicheza bila nahodha Samuel Eto’o walikaribia kufunga bao katika dakika ya 24, baada ya Aboubakar Vincent kupiga kiki iliyotoka nje kidogo la lango la Stars. Nyoni angeweza kubadilisha ubao wa matokeo, kama siyo kushindwa kutumbukiza wavuni kiki ya penalti dakika ya 26 iliyotolewa na mwamuzi kutokana na Ngoula kuucheza mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari. Beki huyo wa Stars alikwenda kupiga penalti hiyo akionekana kutojiamini kabla ya shuti lake kupanguliwa na kipa Effala. Kipindi cha pili Stars ilicheza kwa nguvu na hapana shaka ndiyo walitawala sehemu kubwa, wakifanya mashambulizi mara kwa mara.

Ngasa aliyeisumbua zaidi ngome ya Cameroon alimjaribu kwa shuti la mwendo mrefu kipa Offala ambaye alifanya kazi nzuri ya kulizuia.
Kiungo chipukizi Abubakary naye alikaribia kufunga kwa Stars kama siyo shuti lake kuchezwa na kipa wa cameroon ambaye sehemu kubwa ya kipindi cha pili hakupumzika kuokoa hatari.
Pamoja na kufanya mabadiliko mengi kipindi cha pili, Stars waliendelea kutawala mchezo na kuwafunika Cameroon sehemu ya kiungo.

Katika mchezo huo, Stars ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mwinyi na kuingia Thomas Ulimwengu ambaye aliongeza nguvu ya mashambulizi.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...