Sunday, November 13, 2016

MUNGU HAKUUMBA MASIKINI, KWA NINI WEWE MASIKINI?



Mungu alipomuumba binadamu, hakusema kwamba anamuumba akiwa tofauti na mwingine. Leo, unaponiona mimi, nina moyo mmoja, nina figo, ini, kichwa, macho kama wewe.

Sikuzaliwa nikiwa na magari, sikuzaliwa nikiwa na fedha, nilizaliwa kwenye familia masikini sana, inawezekana ilikuwa masikini hata zaidi ya familia yako.

Baba yangu akanifundisha kuhusu biashara na kila siku akaniambia kwamba kama nitakuwa mfanyabiashara mkubwa, basi natakiwa niwe na nidhamu ya fedha.

Ni mara ngapi umekuwa ukipokea fedha na kuzitumia katika vitu visivyo na maana? Ni mara ngapi umepokea fedha na kusema kwamba kiasi hicho ni kidogo na hakiwezi kukufanya kuwa milionea?

Ndugu zangu! Hakuna bilionea aliyeanza kuwa bilionea kwa kupewa mamilioni ya shilingi. Wapo mabilionea waliopewa laki moja na mwisho kuwa mabilionea.

Wengine walikuwa mafundi wa viatu, mwisho wa siku ni mabilionea wakubwa. Tangu lini fundi viatu akawa na kiasi cha shilingi milioni moja kuanzia maisha? Ni lazima atakuwa na shilingi elfu hamsini, hizohizo akajichanganya, akazipanga na mwisho wa siku akawa bilionea.

Wewe unapata milioni moja, bado unasema ndogo, unapata elfu hamsini, bado unasema ndogo. Ndugu yangu, Mungu anapotaka kukufanya bilionea, hakupi milioni mia moja moja, anakupa kiasi cha chini ili utakapokuwa bilionea uwe na ushuhuda wa kutosha.

Mungu anataka utakaposimama useme kwamba ulikuwa na elfu thelathini, ikabadilisha maisha yako na mwisho wa siku kuwa bilionea. Mungu hakupi milioni mia moja ghafla kwa kuamini kwamba ukipata hiyo, utawaambia watu kuwa ulipata milioni mia moja na baadaye ukawa bilionea.

Ni kiasi kikubwa sana, utawavunja moyo watu wengine kukipata, lakini ukisema kupitia shilingi elfu kumi nikawa bilionea, ni kiasi kidogo sana ambacho mtu anaweza kupambana na kukipata kisha kubadilisha maisha yake.

Ndugu yangu, kumbuka kwamba nilikuja Dar nikiwa sina kitu. Sikuwa na fedha ya kutosha mfukoni, sikuwa na sehemu ya kulala, hakukuwa na mtu aliyenifahamu, nililala kwenye kituo cha mabasi ya mkoa kipindi hicho pale Kisutu, lakini pamoja na hayo yote, bado maneno ya baba yangu kunitaka niwe mfanyabiashara mkubwa yalinirudia kichwani mwangu.

Maneno hayo yakaniongoza, nikawa naamini kwamba kuna siku nitakuwa mfanyabiashara mkubwa. Sijisifii bali ninataka ubadilishe maisha yako kupitia maisha yangu, wewe uliyekata tamaa, ujue kwamba kama ukipanga mikakati yako basi utafanikiwa.

Najua unaweza kuchukua hatua, kuna watu watakwambia, utawezaje? Mbona baba yako alishindwa? Mbona mama yako naye alishindwa? Kuna ndugu yako anajiweza kifedha? Mtu akikwambia hivyo au hata ukiisikia sauti inakwambia hivyo, wajibu kwa kuwaambia, baba yangu hakuweza, mama hakuweza, ila rafiki yangu Shigongo aliweza! Kama yeye aliweza, kwa nini mimi nishindwe?

Kama mtu wa elimu ya darasa la saba aliweza, kwa nini mimi na elimu yangu nishindwe? Kwa nini yule mtoto wa masikini kuliko wazazi wangu aliweza halafu mimi nishindwe?

Huwezi kushindwa rafiki yangu. Nakuambia tena kwamba HUWEZI KUSHINDWA. Unachotakiwa kufanya ni kuamini kisha anza kufanya huku ukimtanguliza Mungu mbele.

Mungu hana ndoto za wewe uwe masikini. Mungu hapendi umasikini, anachotaka na wewe uendeshe magari, uwe na nyumba zako, hoteli kubwa, ila kinachokufanya kuwa masikini ni kutokujiamini kwako. Unahisi kushindwa hata kabla hujaanza safari.

Utakapoanza, wapo watakaokukatisha moyo, usiwasikilize, wewe songa mbele. Kwenye safari ya mafanikio, tuna maadui wengi mno kuliko marafiki. Labda rafiki unayempenda, unayemuona yupo bega kwa bega nawe leo ndiye huyohuyo atakayetaka kuona hupigi hatua baadaye.

Ndugu yangu! Umeumbwa kwa mfano wa Mungu! Unalijua hilo? Kabla ya wewe kuumbwa, Mungu alikutana na malaika na kusema tuumbe mtu kwa mfano wetu. Wewe ni mfano wa Mungu na ndiyo maana unaona, unasikia, unaumia na kufurahi.

Huwezi kushindwa hata mara moja. Inuka ulipo, simama na piga hatua na ninaamini utafika unapotakiwa kufika.

MUNGU AKUONGOZE. TUKUTANE JUMAMOSI KWA MAKALA NYINGINE YA KUKUTOA HAPO ULIPO. USIKOSE KUSHARE ILI MARAFIKI ZAKO NAO WAJIFUNZE. KAMA NILIVYOJITOA KUKUFUNDISHA BURE, JITOE KWA KUWASHIRIKISHA WENGINE UJUMBE HUU KWA KUSHARE. ASANTENI.

E.J SHIGONGO

Saturday, November 12, 2016

otuba ya ndugu Kiongozi wa ACT Wazalendo katika Kikao Maalumu cha Bunge cha Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta

Tangulia Spika wa Bunge la Wananchi

Hotuba ya ndugu Kiongozi wa ACT Wazalendo katika Kikao Maalumu cha Bunge cha Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta

Ndugu Spika,
Ndugu Wabunge,
Mama Magreth Sitta,
Watoto wote wa Mzee Samwel John Sitta, Ndugu, Jamaa na Marafiki,
Ndugu zangu Watanzania,

Leo kikao maalumu cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wake wa Tano kinamuaga mtoto wa Mzee John Sitta na Hajjat Zuwena Said Fundikira. Nami nimepewa nafasi niseme maneno machache kuhusu mzee wetu huyu tunayemuaga.

John Samwel Sitta anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu, shujaa wa wote wanaoamini katika Uwajibikaji wa kitaasisi, Mwanasiasa aliyepanda na kushuka na kisha kupanda na kubakia kileleni, taswira ya mkoa wake wa Tabora, sio tu mdhamini wa klabu ya Simba, bali pia Mwanasimba aliyeipeleka klabu Brazil na kuwezesha kuifunga Yanga mabao mengi zaidi ambayo hayajapata kulipwa na wapinzani wetu hata kwa kuungakuunga, Mwanamageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania.

Hata katika kifo chake, Samwel John Sitta ameweka rekodi nyengine - kwa Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 - 2015 isipokuwa tu kwa kipindi cha 1995 - 2005. Rekodi hii itaendelea kwa wengine wote watakaofuata baada yake.

Ni mtu wa namna gani wewe Samwel Sitta? Spika wa Kasi na Viwango, unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya Jeneza lako lililopambwa na Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo kwenye nyumba yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu (The Peoples Speaker).

Tuliokupenda tunajua. Ulikuwa Baba mlezi. Ulikuwa Mume mwema. Ulikuwa Babu. Ulikuwa Kiongozi. Nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo. Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa katika kukukumbuka ewe Spika wa Watu.

Ulikuwa na vyeo vingi; Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Waziri tena, Mkurugenzi Mtendaji, Spika, Waziri tena na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Lakini, wala, tunakuita Spika Sitta tu. Kwanini? Kwa sababu 'Legacy' yako ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sio kwamba umeanzisha Bunge wewe, la hasha. Lakini ulipopokea Uspika wa Bunge letu, kama ilivyo jadi yako, uliliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha Mhimili huu na kuuweka katika nafasi yake ya Kikatiba.

Nakumbuka siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aongee na baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006. Mimi nikiwa nina miaka 29 tu. Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa kumshawishi Rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia;

"Babu, mimi sasa alasiri, ninyi ndio saa nne asubuhi. Nawawekea misingi tu na kuliweka Bunge katika nafasi yake ya kikatiba".

Kilichofuata ni mabadiliko makubwa ya Kanuni za Bunge, kuandikwa upya kwa Sheria ya Bunge (National Assembly Administration Act, 2008) na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo, Constituencies Development Catalyst Fund (CDCF).

Samwel Sitta, bado tunasikia mwangwi wa sauti yako nene kutoka kwenye kiti cha Spika ukiwataka Mawaziri wajibu maswali kwa ufasaha. Hukuisahau Tabora yako. Damu ya kichifu wa Unyanyembe ya Fundikira kutoka mama yako Zuwena ilikusambaa kwenye mishipa yako. Ukiona kuna swali linalohusu mkoa wako wa Tabora hukusita kuwaambia Mawaziri wajibu vizuri (haswa kuhusu barabara), au ukiamsha jeshi lako (akina Lucas Lumambo Selelii nk) wakisema "mheshimiwa Spika, wewe leo ukipata dharura Urambo unafikaje!". Yote hiyo kutilia nguvu umuhimu wa maendeleo ya mkoa wako.

Wewe ni kielelezo cha Demokrasia ya Vyama vingi bungeni. Ulitoa nafasi kwa wabunge wote wa kambi zote ndani ya Bunge. Hatusemi hukubagua, la hasha, uCCM wako ulikuwa pale pale. Lakini walio wengi walishinda na walio wachache walisikika. Ndio Demokrasia hiyo.

Sitta ulikuwa Muungwana. Nakumbuka siku ile unamwomba radhi Mzee John Momose Cheyo katika kamati ya Uongozi (baada ya kuwa ulimtoa kwa makosa bungeni), eti msongo wa mawazo ulikujaa kwani watu wanapitapita Jimboni. Lakini uliwashinda. Unyenyekevu wako wa kuomba radhi unapokosea ni somo kubwa sana kwa Viongozi wengine tuliobakia.

Wabunge wenzangu, tunataka kumuenzi Spika wa Watu - Samwel John Sitta? Basi hakuna kumuenzi bora zaidi kama kuimarisha uhuru na heshima ya Bunge letu.

Tuendeleze Jahazi.

Samwel Sitta anakwenda kwenye nyumba yake ya milele akiongozwa na imani yake kubwa kwa Mungu na uzalendo wake usio na mawaa kwa nchi yake Tanzania. Angalau bado ataendelea kuwa nasi kwa kutuachia mafundisho makubwa kutokana na Maisha yake, mambo mema aliyoyafanya kwa nchi yetu, ndoto aliyoiishi ya Tanzania imara na yenye heshima, na malezi kwa viongozi wengi vijana aliowafunda na kuwalea kiuongozi.

Ni dhahiri umeishi maisha yako Babu. Kama isemavyo biblia, 2 Timotheo 4:7 "Nimepigana Vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda".

Tangulia Spika wa Watu (The Peoples’ Speaker) Samwel John Sitta.

Mola akulaze pema.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 11, 2016
Dodoma

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...