Sunday, November 13, 2016

MUNGU HAKUUMBA MASIKINI, KWA NINI WEWE MASIKINI?



Mungu alipomuumba binadamu, hakusema kwamba anamuumba akiwa tofauti na mwingine. Leo, unaponiona mimi, nina moyo mmoja, nina figo, ini, kichwa, macho kama wewe.

Sikuzaliwa nikiwa na magari, sikuzaliwa nikiwa na fedha, nilizaliwa kwenye familia masikini sana, inawezekana ilikuwa masikini hata zaidi ya familia yako.

Baba yangu akanifundisha kuhusu biashara na kila siku akaniambia kwamba kama nitakuwa mfanyabiashara mkubwa, basi natakiwa niwe na nidhamu ya fedha.

Ni mara ngapi umekuwa ukipokea fedha na kuzitumia katika vitu visivyo na maana? Ni mara ngapi umepokea fedha na kusema kwamba kiasi hicho ni kidogo na hakiwezi kukufanya kuwa milionea?

Ndugu zangu! Hakuna bilionea aliyeanza kuwa bilionea kwa kupewa mamilioni ya shilingi. Wapo mabilionea waliopewa laki moja na mwisho kuwa mabilionea.

Wengine walikuwa mafundi wa viatu, mwisho wa siku ni mabilionea wakubwa. Tangu lini fundi viatu akawa na kiasi cha shilingi milioni moja kuanzia maisha? Ni lazima atakuwa na shilingi elfu hamsini, hizohizo akajichanganya, akazipanga na mwisho wa siku akawa bilionea.

Wewe unapata milioni moja, bado unasema ndogo, unapata elfu hamsini, bado unasema ndogo. Ndugu yangu, Mungu anapotaka kukufanya bilionea, hakupi milioni mia moja moja, anakupa kiasi cha chini ili utakapokuwa bilionea uwe na ushuhuda wa kutosha.

Mungu anataka utakaposimama useme kwamba ulikuwa na elfu thelathini, ikabadilisha maisha yako na mwisho wa siku kuwa bilionea. Mungu hakupi milioni mia moja ghafla kwa kuamini kwamba ukipata hiyo, utawaambia watu kuwa ulipata milioni mia moja na baadaye ukawa bilionea.

Ni kiasi kikubwa sana, utawavunja moyo watu wengine kukipata, lakini ukisema kupitia shilingi elfu kumi nikawa bilionea, ni kiasi kidogo sana ambacho mtu anaweza kupambana na kukipata kisha kubadilisha maisha yake.

Ndugu yangu, kumbuka kwamba nilikuja Dar nikiwa sina kitu. Sikuwa na fedha ya kutosha mfukoni, sikuwa na sehemu ya kulala, hakukuwa na mtu aliyenifahamu, nililala kwenye kituo cha mabasi ya mkoa kipindi hicho pale Kisutu, lakini pamoja na hayo yote, bado maneno ya baba yangu kunitaka niwe mfanyabiashara mkubwa yalinirudia kichwani mwangu.

Maneno hayo yakaniongoza, nikawa naamini kwamba kuna siku nitakuwa mfanyabiashara mkubwa. Sijisifii bali ninataka ubadilishe maisha yako kupitia maisha yangu, wewe uliyekata tamaa, ujue kwamba kama ukipanga mikakati yako basi utafanikiwa.

Najua unaweza kuchukua hatua, kuna watu watakwambia, utawezaje? Mbona baba yako alishindwa? Mbona mama yako naye alishindwa? Kuna ndugu yako anajiweza kifedha? Mtu akikwambia hivyo au hata ukiisikia sauti inakwambia hivyo, wajibu kwa kuwaambia, baba yangu hakuweza, mama hakuweza, ila rafiki yangu Shigongo aliweza! Kama yeye aliweza, kwa nini mimi nishindwe?

Kama mtu wa elimu ya darasa la saba aliweza, kwa nini mimi na elimu yangu nishindwe? Kwa nini yule mtoto wa masikini kuliko wazazi wangu aliweza halafu mimi nishindwe?

Huwezi kushindwa rafiki yangu. Nakuambia tena kwamba HUWEZI KUSHINDWA. Unachotakiwa kufanya ni kuamini kisha anza kufanya huku ukimtanguliza Mungu mbele.

Mungu hana ndoto za wewe uwe masikini. Mungu hapendi umasikini, anachotaka na wewe uendeshe magari, uwe na nyumba zako, hoteli kubwa, ila kinachokufanya kuwa masikini ni kutokujiamini kwako. Unahisi kushindwa hata kabla hujaanza safari.

Utakapoanza, wapo watakaokukatisha moyo, usiwasikilize, wewe songa mbele. Kwenye safari ya mafanikio, tuna maadui wengi mno kuliko marafiki. Labda rafiki unayempenda, unayemuona yupo bega kwa bega nawe leo ndiye huyohuyo atakayetaka kuona hupigi hatua baadaye.

Ndugu yangu! Umeumbwa kwa mfano wa Mungu! Unalijua hilo? Kabla ya wewe kuumbwa, Mungu alikutana na malaika na kusema tuumbe mtu kwa mfano wetu. Wewe ni mfano wa Mungu na ndiyo maana unaona, unasikia, unaumia na kufurahi.

Huwezi kushindwa hata mara moja. Inuka ulipo, simama na piga hatua na ninaamini utafika unapotakiwa kufika.

MUNGU AKUONGOZE. TUKUTANE JUMAMOSI KWA MAKALA NYINGINE YA KUKUTOA HAPO ULIPO. USIKOSE KUSHARE ILI MARAFIKI ZAKO NAO WAJIFUNZE. KAMA NILIVYOJITOA KUKUFUNDISHA BURE, JITOE KWA KUWASHIRIKISHA WENGINE UJUMBE HUU KWA KUSHARE. ASANTENI.

E.J SHIGONGO

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...