Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
aitwaye Madaraka, amesema viongozi wa sasa wameshindwa kufuata nyayo za
kiongozi huyo kutokana na sababu ambazo amesema “haziko wazi”.
Katika mahojiano yake na gazeti hili, Madaraka
anasema: “Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo ya uadilifu kuenziwa kwa
sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo ya kujinufaisha
mimi kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda”.
Yafuatayo ni mahojiano kamili na Madaraka.
Mwananchi: Ni miaka 14 sasa tangu kufariki kwa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, unaizungumziaje miaka hiyo
kimaisha katika familia, bila kuwapo kwa Mwalimu?
Madaraka: Binadamu tumeumbwa na uwezo wa
kukabiliana na kuondokewa ndugu na jamaa zetu wa karibu. Majonzi
yalikuwa makubwa baada ya kufariki Mwalimu, lakini tunatambua kuwa kuna
umuhimu wa kuomboleza na baadaye kuendelea kukabiliana na changamoto za
kila siku za maisha. Na yeye angetarajia hivyo.
Mwananchi: Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa
nchi, ni zipi fikra au mtazamo wako jinsi viongozi wetu wa sasa
wanavyomuezi kwa kuwa wafuasi wa nyayo zake?
Madaraka: Hebu tuseme tu bila unafiki kuwa katika
masuala mengi ya uongozi, hasa ya uadilifu, suala la kumuenzi Mwalimu
Nyerere ni lengo ambalo viongozi wengi wa sasa wanaweza kuwa wanalo,
lakini kutokana na sababu ambazo haziko wazi basi hilo lengo siku zote
halikamatiki, liko hatua kumi mbele yao. Na kila wakielekea kama
kulifikia na kulitimiza basi wanateleza na kuanguka na lengo hilo
linawaacha hatua nyingine 20 mbele.
Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo ya uadilifu
kuenziwa kwa sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo ya
kujinufaisha mimi kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda.
Mwananchi: Miongoni mwa mambo ambayo Mwalimu
Nyerere aliyaenzi na kuyasimamia enzi za uhai wake, ni Muungano. Kwa
maoni yako unadhani hili linaenziwa vipi? (rejea mvutano wa sasa wa
Serikali mbili, tatu nk, unatokana na mchakato wa Katiba Mpya).
Mwananchi: Nitumie msemo wa kisiasa kuwa sasa hivi
suala la kutengua Muungano linazungumzika. Wakati waasisi wenyewe wapo
hai wale waliofikiria kutengua Muungano walipata kigugumizi au
walishindwa kuwa wazi na fikra zao. Sasa hivi inaelekea kuna baadhi ya
makundi ya viongozi pande zote mbili za Muungano hawataki Muungano,
lakini wanashindwa kuwa wazi kutetea msimamo wao huo. Ni sauti chache
sana utazisikia zikisimama bila kutetereka kutetea kuwepo kwa Muungano.
Ni dhahiri kuwa sauti za kutaka Zanzibar iachane
na Muungano zimekuwa na nguvu zaidi kuliko zile ambazo zinatetea
Muungano. Naamini kuwa viongozi wanaozungumzia Muungano wa mkataba
hawajapata ujasiri wa kisiasa wa kusema kuwa hawataki kabisa Muungano.
Naweza kuwa siko sahihi, lakini naamini kuwa
yeyote anayejaribu kutetea umoja mkubwa zaidi kati ya Bara na Visiwani
na siyo mfano tu wa umoja anapingana na mtazamo uliojengwa juu ya fikra
kuwa maendeleo ya Zanzibar yanakwamishwa na kuwepo ndani ya Muungano.
Kwa sababu ni baadhi ya wanasiasa ndiyo wanajenga fikra hizi
tunaweza kusema kuwa ni siasa ndiyo inasukuma ukweli badala ya ukweli
kusukuma siasa. Kwa maoni yangu, ukweli wa kisiasa unajengwa juu ya
kushinda uchaguzi ujao.
Hilo ndilo jambo la msingi. Kusimamia ukweli
tofauti na hapo kunaweza kusababisha kushindwa uchaguzi. Ukweli
ninaoamini mimi ni kuwa siku zote umoja huleta nguvu, utengano udhaifu.
Hii ni kweli katika suala la uchumi na hata kisiasa.
Lakini iwapo hilo ndilo wananchi wanataka, huwezi
kulikwepa. Matokeo yake ni Serikali tatu. Umoja wa kweli ungekuwa
Serikali moja na sauti za ‘mimi’ na ‘wewe’ (Zanzibar na Bara) zingepotea
na kuchukuliwa na suala la ‘sisi’ (Watanzania). Lakini suala la
Serikali moja lilionekana haliwezekani, mwaka 1964 na la Serikali mbili
likaonekana mwafaka. Kwenda kwenye Serikali tatu ni kama kupiga hatua
moja nyuma katika kuulinda Muungano.
Mimi nalaumu uwezekano wa kupatikana kwa
rasilimali ya mafuta kama kichocheo kikubwa cha kuyumbisha Muungano.
Siku zote pesa na utajiri ndiyo hugombanisha ndugu. Ndugu wenye utajiri
wana fursa nyingi zaidi za kutoelewana kuliko ndugu wasio na utajiri.
Ukweli ni kuwa kama huna mali hutakuwa na ugomvi
kuhusu mali na ndugu yako. Mara tulipopata harufu ya mafuta chini ya
Bahari ya Hindi basi masuala ya kuukosoa Muungano yakapamba moto.
Mwananchi: Nje ya Serikali ambako Mwalimu Nyerere
alikuwa kiongozi, kuna familia ambako alikuwa baba. Ndani ya familia je,
mnamuenzi vipi Baba wa Taifa?
Madaraka: Ukiwa ndani familia huna uchaguzi juu ya
kama unataka kumuenzi Mwalimu au la. Watu watakupachika matarajio yao
na kiwango cha ulinganishi kimeshawekwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa hiyo mwanafamilia anapokuwa na mwenendo ambao
haufanani na hicho kiwango kinachotarajiwa, basi wengi wanashangaa.
Mfano, mimi nikivuta bangi nitaandikwa kwenye gazeti, lakini kitendo
hicho kikifanywa na Mtanzania ambaye baba yake hana wadhifa mkubwa wa
uongozi hiyo haiwezi kuwa habari.
Labda wengine watasikitishwa na suala hilo.
Watakaofurahi ni wale ambao wanakubali kuwa uadilifu katika uongozi na
utumishi wa umma ni suala lisilowezekana.
Baadhi ya wanafamilia tunasimamia kutangaza Kijiji
cha Butiama kama eneo la kihistoria na la kiutamaduni. Wageni wengi
bado wanafika kutembelea Butiama mahususi kwa sababu ndipo alipozaliwa
na kuzikwa Mwalimu Nyerere.
Mwananchi: Ni tabia ya viongozi wengi wa Afrika
kujilimbikizia mali wanapokuwa madarakani. Ukiwa kiongozi wa familia ya
Mwalimu Nyerere, unaweza kueleza tofauti yao na Baba wa Taifa? Je, yeye
aliwaachia mali kiasi gani (kwa maana ya fedha, nyumba na mashamba)?
Madaraka: Awali, mimi siyo kiongozi wa familia ya Mwalimu Nyerere. Hatuna nafasi hiyo ndani ya familia.
Mimi naamini kuwa mtu ambaye hana tamaa ya kujilimbikizia mali
huzaliwa hivyo. Huwezi kupenda kujilimbikizia mali na utajiri (kwa njia
halali au vinginevyo) halafu ukakaa madarakani kwa miaka 23 bila tabia
yako hiyo kujitokeza katika matendo yako au ya wale waliokuzunguka.
Ukweli utabainika tu.
Sasa inawezekana kuwa kiongozi akashika wadhifa
akiwa mwadilifu halafu akiwa madarakani akapata vishawishi vya
kujilimbikizia mali.
Hapa ndiyo natoa hoja kuwa kama wewe ulizaliwa
kuwa mtu usiyesumbuliwa na kukosa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti
yako basi hivyo vishawishi havitakusumbua. Lakini tofauti ya hivyo
utashawishika kujitajirisha mwenyewe na kusahau wajibu kwa umma.
Sisi hatukuachiwa mali yoyote ambayo ilitokana na
kipato chake. Kuna nyumba ile ya Msasani ambayo aliijenga kwa mkopo
ambao hakuweza kuulipa wakati anastaafu na aliamua kuikabidhi Serikali,
lakini Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilipitisha uamuzi wa kulipa au
kufuta deni na akakabidhiwa nyumba. Kuna nyumba ndogo ambayo alijenga
akiwa Rais, iko Butiama.
Vilevile, baada ya vita vya Kagera alijengewa
nyumba na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambayo baadaye Serikali
ilichukua jukumu la kuikamilisha. Awali, ni wanajeshi wenyewe walikuwa
wanakatwa mishahara yao kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo.
Nyumba nyingine ipo Butiama na alijengewa na CCM
baada ya viongozi wenzake kuamua kuwa nyumba yake aliyojenga Butiama ni
ndogo sana na haistahili kutumiwa na Rais wa nchi.
Alipewa eneo la shamba na Kijiji cha Buturu,
jirani na Kijiji cha Butiama, ingawa kumekuwa na mbinu za kutaka kupora
hilo shamba zinazoongozwa na baadhi ya viongozi wa zamani wa kijiji
hicho.
Mwananchi: Novemba 2004, familia ya Baba wa Taifa
ililalamikia Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa iliyopitishwa na Bunge,
kwa hofu kwamba ingepoteza uhalali wa kumilikia baadhi ya mali za
Mwalimu Nyerere. Ni kipi kinajitokeza kama changamoto tangu kupitishwa
kwa sheria hiyo?
Madaraka: Jibu hili litakuwa refu kidogo kwa kuwa
lina masuala mengi ndani yake. Mimi nilikuwa mmojawapo wa wajumbe wa
kamati ndogo ya Serikali iliyoshiriki kwenye kazi ya kuchangia vipengele
vya muswada wa ile sheria.
Nilikuwa ninaiwakilisha familia pamoja na dada
yangu Rosemary. Kuna baadhi ya vipengele ambavyo tulipendekeza kama
familia wakati wa kuandaa muswada na waziri mhusika alienda bungeni
kutoa tamko tukiamini kuwa mapendekezo yetu yangekuwa sehemu ya sheria,
lakini waziri alipofika huko hakuchukua mapendekezo yote kutoka upande
wa familia.
Changamoto siyo nyingi, lakini kuna jambo la
msingi ambalo nafikiri linahitaji kutolewa uamuzi haraka. Sheria inaweka
wazi kuwa kazi ya kuwaenzi waasisi wa Tanzania ni jukumu la pamoja na
kuwa yeyote anayemiliki kumbukumbu za Mwalimu Nyerere na za Sheikh Abedi
Amani Karume ataendelea kumiliki hizo kumbukumbu, lakini atatarajiwa
kushiriki kwenye kizitunza kwa mujibu wa sheria hii na sheria nyingine
zilizopo.