Bilionea wa kitanzania Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye ni mkurugenzi mtendaji na rais wa makapuni ya Mohammed Interprises (MeTL) amevunja ukimya baada ya kujitokeza na kuweka bayana nia yake ya kutaka kununu asilimia 51 za klabu hiyo kwa shilingi bilioni 20 za Tanzania.
MO amesema nia yake ya kutaka kuwekeza kitita hicho cha pesa ni kutaka kufanya mabadiliko ya mfumo mzima wa uendeshaji wa klabu hiyo ili kuleta ushindani ndani ya nchi na kimataifa lakini kubwa ni kuhakikisha klabu hiyo inapata mafaniko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati akiidhamini klabu hiyo.
“Nakumbuka mwaka 2004 nilisema mfumo huu wa uendeshaji hauko endelevu, na hatuwezi kuendelea kushindana na klabu kubwa za Afrika kama Ismailia, TP Mazembe na nyingine kama tukiendelea na mfumo huu ambao tunao. Niliwaomba sana viongozi tubadilishe mfumo lakini kwa bahati mbaya miaka 10 iliyopita ilionekana kama haiwezekani.”
Baada ya kusema hivyo, MO akaanza kuorodhesha kwanini anataka kuwekeza kwenye klabu ya Simba ili kuleta mafanikio na ushindani zaidi.
Bajeti ya timu
Bajeti ya Yanga ni ni takribani zaidi ya shilingi bilioni 2.5, bajeti ya Azam FC ni hiyohiyo lakini ukienda kuona bajeti ya Simba ni nusu ya bilioni 2.5. Bajeti yao ni karibia bilioni 1.2.
TBL inatoa milioni 400 hadi 500 lakini kuna mapato ya getini, kuna hela kutoka Vodacom na Azam TV ambao ndio wadhamini wa ligi hiyo hela haitoshelezi.
Malengo yangu ni kuitoa Simba kwenye bajeti ya bilioni 1.2 kwa mwaka na kuipeleka kwenye bilioni 5.5
Ukiingia kwenye dirisha la usajili kama tunamtaka mchezaji sisi tunasema tuna milioni 20 wenzetu wanasema wanaweka dau la milioni 40 hadi 50 lakini pia hatuna uwezo wa kumlipa mshahara mzuri mchezaji huyo.
Mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio
Lazima tusajili wachezaji wazuri, tuwalipe vizuri, tutafute kocha mzuri, kwahiyo ukitenga bilioni 4 kwa mwaka tayari unakuwa umewazidi wapinzani wako wa Azam na Yanga kwasababu wao wanatumia bilioni 2.5 hadi bilioni 3. Kwahiyo unakuwa umewazidi kwa asilimia 25 na hapo unaweza kushindana nao na inabaki bilioni 1.5.
Miundo mbinu duni ya klabu
August 8 Simba inafikisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936. Simba haina hata uwanja wake wa kufanyia mazoezi, mimi kama mwanachama na mpenzi wa Simba inaniuma. Wenzetu wameanza juzi na tayari wanauwanja wao. Kwahiyo malengo yangu ni kwamba, tukitenga bilioni 1.5 kwa miaka mitatu, tutajenga uwanja, gym, swimming pool, nutrition centre, na recovery centre, lazima tuwe na wataam wa kila aina.
Tutengeneze miundo mbinu ya kisasa, tunauwanja pale Bunju lazima tuwekeze. Lakini ukitaka kuwekeza vizuri, huwezi kuwekeza kwa shilingi milioni 500, unahitaji bioni 5. Kwahiyo unatenga bioni 1.5 kila mwaka kwa miaka mitatu unapata kiasi hicho cha pesa halafu unafanya utekelezaji.
Timu za vijana
Ili ufanikiwe katika soka lazima uwe na timu za vijana U18, U16, U14 na U12. Kuendesha hizi timu nne unahitaji kuwa na pesa. Kwahiyo mimi dhamira yangu sio kupata hela kutoka Simba, ninabiashara zangu zaidi ya 100 jambo ninalotaka ni kuwekeza Simba na kubadilisha mfumo, tuwe na mfumo wa uwazi wa uendeshaji wa timu kuwa wa kiueledi ili siku moja tuwe mabingwa Afrika kwasababu mimi sitaki niishie Tanzania tu.
Wanachama wa siku nyingi kufaidika
Wanachama walioitumikia Simba kwa siku nyingi sana, hatuwezi kuacha kuwafikiria, mimi fikra yangu tupange na tuwape hisa bure kuliko kuwa na kadi tu ambazo hazina faida. Watapata hisa, huko mbele klabu ikifanya vizuri wanaweza kuuza hisa zao au kama watakuwa na pesa wataweza kununua hisa zaidi lakini pia watapata gawio. Hawa watu wametoa jasho na damu kuitumikia klabu ya Simba na huko nyuma hawajapata chochote kwahiyo ni haki yao kupata hisa za Simba SC.
No comments:
Post a Comment