KWA UFUPI
- Tukiangalia historia ya uanzishwaji wa vyuo vikuu hapa nchini tunagundua kwamba hakuna chuo kikuu kilichoanzishwa baada ya kufanyika kwa mipango madhubuti ambayo ni muhimu katika kutayarisha mazingira stahiki ya kufundishia elimu ya juu.
Safari ya kupita katika kampasi za vyuo vyetu vikuu hapa nchini itamthibitishia mgeni yeyote jambo moja kubwa. Kwamba tumekurupuka kuanzisha utitiri wa vyuo vikuu bila kufanya maandalizi ya kutosha.
Tukiangalia historia ya uanzishwaji wa vyuo vikuu hapa nchini tunagundua kwamba hakuna chuo kikuu kilichoanzishwa baada ya kufanyika kwa mipango madhubuti ambayo ni muhimu katika kutayarisha mazingira stahiki ya kufundishia elimu ya juu.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Kampasi ya Mlimani), ambacho sasa ni moja ya vyuo vikuu vichache vyenye mandhari na mazingira bora barani Afrika kilianzia katika makazi ya muda katika Barabara ya Lumumba, jijini Dar es Salaam mwaka 1963.
Makazi hayo hayakuwa mazuri kwa chuo kikuu na ndio maana Rais Nyerere, kwa kuelewa umuhimu wa elimu ya juu aliagiza itafutwe haraka sehemu kubwa nje ya mji kwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho tunakishuhudia hivi sasa.
Siyo wananchi wengi wanakumbuka kuwa, Rais Nyerere alimteua raia wa Canada kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho na kumkabidhi jukumu la kutafuta sehemu stahiki ya kujenga taasisi hiyo.
Mkanada huyo alichagua sehemu kilichopo chuo hicho hivi sasa, wakati huo likiwa pori kubwa la asili na wakiwamo wanyama wakali. Mji wakati huo ulikuwa unaishia Magomeni na makazi tunayoyaona hivi sasa Manzese, Sinza, Mwenge, Ubungo na kwingineko yalikuwa hayapo, kwani lilikuwa pori nene.
Hivyo, hatukushangazwa na taarifa zilizothibitishwa kwamba maofisa wa Serikali ya Rais Nyerere walipinga vikali uamuzi wa raia huyo wa Canada wa kuchagua ‘pori’ hilo kwa ajili ya kujenga chuo hicho.
Walisema hakuwa na akili nzuri, hivyo walimshtaki kwa Rais Nyerere ili abatilishe uamuzi wa kujenga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam porini. Kwa mshangao wao, Rais alibariki uamuzi wa raia huyo wa Canada, ambaye alianza ujenzi wa chuo hicho ambacho sote tunajivunia hivi leo.
Tumelazimika kuorodhesha yote hayo kwa lengo la kuonyesha jinsi Rais Nyerere na mteule wake huyo walivyokuwa na dira, mwelekeo na upeo mkubwa wa kutambua kwamba mji wa Dar es Salaam ungepanuka katika miaka michache ijayo na kuwa jiji kubwa lenye mamilioni ya watu.
Makosa waliyofanya waasisi wengi wa vyuo vikuu duniani ni kushindwa kutambua kwamba vyuo hivyo vilihitaji nafasi ya kutosha ili viweze kupanuka kwa mahitaji ya wakati huo na wa baadaye.
Lakini inasikitisha kuona kwamba hapa nchini tumeanzisha utitiri wa vyuo vikuu pasipo mipango wala maandalizi.
Vyuo vingi havina majengo wala mazingira yenye hadhi ya kuitwa vyuo vikuu, kwani vimejibanza katika sehemu chafu, finyu na zenye majengo mabovu ambamo vinabuniwa vyumba vya madarasa, maabara, maktaba na kadhalika ambavyo havikidhi viwango vya chuo kikuu.
Mazingira kama hayo hayawezi hata kidogo kutoa wahitimu wenye viwango vya kushindana katika soko la ajira au soko huria la wajasiliamali.
Hivi sasa kuna vyuo vikuu zaidi ya 46 nchini. Pamoja na kuwapo Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2005, vyuo hivyo bado vinaanzishwa kienyeji katika mazingira ya aibu.
Inakuwaje vinashindwa kuboresha mazingira kutokana na fedha zinazolipwa na wanafunzi kama ada kutoka Bodi ya Mikopo?
No comments:
Post a Comment