Thursday, April 11, 2013

BAJETI FINYU YAIKWAMISHA WIZARA YA UTALII


Wakati Bunge limeanza vikao vyake na jana kuanza kujadili Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, asilimia 50 ya miradi  mbalimbali ya  Wizara ya Maliasili na Utalii iliyokuwa  kwenye mchakato  wa kupewa ruzuku  kutoka kwenye Mfuko wa  Misitu  Nchini (TFF) imeshindwa kukamilika kutokana na ufinyu wa bajeti.
Miradi hiyo ambayo ilikuwa 70 ilitarajiwa kupata ruzuku ya Sh1.9 bilioni, nusu yake haijakamilika na haitoweza kukamilika mwaka huu wa fedha baada ya fedha kupunguzwa kwenye  bajeti  ya 2012/2013  na kusababisha miradi hiyo kuzorota.
Waziri wa  Maliasili na Utalii,  Balozi Khamisi Kagasheki amesema miradi hiyo haijakamilika baada ya wizara hiyo kupewa bajeti finyu na kusababisha miradi hiyo kutokamilika kama ilivyokuwa imekusudiwa awali.
Amesema kwamba  bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013,  ilikuwa Sh84 bilioni, lakini zilizoelekezwa katika wizara yake ni Sh 78 bilioni tu na kupunguza  kiasi na wizaru kutofikia lengo.

Bajeti ilikuwa finyu
 “Miradi hii  tumeshindwa kuikamilisha yote  kutokana na mambo mengi, lakini kubwa zaidi ni ufinyu wa bajeti  tuliyokuwa nayo, hivyo masuala mengine  tumeshidwa kufanya  kwa sababu fedha ni kidogo  na hasa kwenye suala la miradi, kwani mingi haijakamilika.
“Ni vyema kiasi halisi cha bajeti  kinachotangazwa kwa wananchi kilingane na  kile kinachopelekwa wizarani kwani  wananchi wanakumbukumbu na hesabu iliyotangazwa bungeni, bajeti inayopelekwa wizarani ni tofauti na  hivyo kusababisha sintofahamu kati ya wananchi na wizara husika,”anasema Kagasheki.
Amesema ufinyu wa bajeti  unasababishwa na Wizara ya  Fedha na kwamba ni kikwazo kwa maendeleo ya Wizara ya Maliasili na Utalii  na kwa Wizara nyingine  kwa sababu bajeti haitoshi, kwani mara nyingi bunge  linakuwa linapitisha bajeti,  lakini kwa wakati mwingine bajeti hizo hazitoshelezi matumizi na mahitaji ya wizara husika.
“Tusitengeneze bajeti ambazo  zinakuwa shida kwa wananachi,  kwani tunaonekana kama wezi  kumbe hela zinakuwa zimepunguzwa  kutoka kwenye bajeti husika,” anasema Kagasheki.
Kagasheki anasema kuwa  kwa upande wa tafiti mbalimbali  katika  Wizara hiyo ikiwamo utafiti wa  magonjwa ya wanyamapori na mifugo pamoja na  utafiti kuhusu ufugaji wa nyuki zinaendelea kufanywa kwa ufasaha na zipo mbioni kukamilika .
Anaeleza kuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji wa Nyuki kilichoko mkoani Tabora  kinafanya vizuri na kimeweka kipaumbele kuhusu mafunzo hayo jambo ambalo linaashiria maendeleo mazuri kuhusu elimu ya nyuki.
Kagasheki amebainisha kwamba  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  amechangia  kiasi kikubwa kuwahamasisha wananchi kuhusu ufugaji wa nyuki na faida zake hasa katika mikoa ya Kanda ya magharibi, ikiwamo  Tabora, Katavi na mikoa inayozunguka kanda hiyo.
“Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele kututia moyo kuhusu ufugaji wa nyuki na faida zake na hata kuwahamasisha wananchi wa Kanda ya Magharibi kufuga nyuki kwa wingi, hili nalo limekuwa faraja kwetu katika kuendeleza  Wizara ya Maliasili naUtalii,” anasema Kagasheki.

Miundombinu mbalimbali iliyopewa kipaumbele ili wizara hiyo iwe na ufanisi ni ujenzi wa barabara za mbuga  za wanyama kwa mfano Katavi, Ruaha, Mikumi  na Saadani, ambako imejengwa kwa kiwango cha changarawe  na kuwa na uwezo wa kupitika.
Kagasheki anasema pamoja na matatizo mengi yaliopo kwenye wizara hiyo bado wameweza kujenga hoteli kubwa nne za kitalii katika mbuga mbalimbali nchini zikiwamo mbuga za Ngorongoro mkoani Arusha,  na Serengeti.
Dar hakuna hoteli zenye hadhi
Anasema tatizo kubwa katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine ni uhaba  wa kuwa na hoteli zenye hadhi na hata zenye majina makubwa ukulinganisha na nchi nyingine kama Kenya.
“Tuna changamoto nyingi, lakini pamoja na hayo tumejitahidi kujenga hoteli nne za kitalii ambazo zipo mbioni kukamilika kwani hatuna hoteli kubwa na za kifahari zitakazovutia watalii kama ambavyo ipo kwa  majirani zetu Kenya” anasema Kagasheki.
Anabainisha kwamba miradi pamoja na mipango mingine ambayo haikufanikiwa kukamilika kwa mwaka wa fedha 2012/13 itapewa vipaumbele katika mwaka ujao wa fedha wa 2013/14.
Wakati baadhi ya miradi kama anavyosema Waziri ikishindwa kutekelezwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya wizara, sekta ya utalii bado inatakwimu nzuri za kimapato ikilinganishwa na sekta nyingine.
Sekta hiyo inashika nafasi ya pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya madini, vilevile takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa mapato katika sekta hiyo yaliongezeka kutoka dola 739.06 milioni za Marekani mpaka dola 1,353.29  milioni katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2011 na pia mchango wake katika pato la Taifa uliongezeka na kufikia asilimia 17.
Pia ikumbukwe mwaka huu vivutio vitatu vya kitalii vya Tanzania, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro zilishinda katika shindano la maajabu saba ya asili ya Afrika, ushindi ambao unazidi kuongeza fursa za kitalii Tanzania.Wakati tukisubiri bajeti mpya ya 2013/2014 ni changamoto kwa serikali na wadau wa sekta hiyo kama Bodi ya Utalii (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa) na wengine kutazama upya namna ya kufanikisha miradi mingi inayopangwa na Serikali.
Katika bajeti ya mwaka 2011/12 vipaumbele vililenga kuboresha miundombinu katika sekta ya utalii, huduma za utalii, kutangaza utalii, urithi wa maliasili.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...