Baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza matokeo ya sensa, inayokaribia
watu 45 milioni, siku chache baadaye deni la taifa lilitangazwa kufikia
Sh21 trilioni huku katika wastani kila mtu akidaiwa Sh467,404.
Fedha
hizo zinatokana na mkopo baada ya Serikali kukopa kwa ajili ya kujenga
miundombinu kama barabara, bomba la gesi, mishahara ya wafanyakazi, na
miradi mingine.
Kwa mujibu wa taasisi isiokuwa ya kiserikali ya
Tanzania Coalition on Debt and Development (TCDD), serikali inadaiwa
‘mzigo wa madeni’ unaofika Sh21 trilioni.
Mkurugenzi wa taasisi
hiyo Hebroni Mwakagenda, anafafanua kwamba Serikali inakopa fedha hizo
Benki Kuu (BoT), Benki za Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya
Hifadhi za Jamii, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB)
na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).
Mwakagenda anasema deni
limeongezeka kwa dola 456.1 milioni sawa na Sh7.3 trilioni katika
kipindi cha mwaka mmoja tu, tangu Oktoba 2011.
Akichanganua
kuhusu deni hilo Mwakagenda abainisha kuwa mpaka kufikia Oktoba mwaka
jana, deni la nje lilikuwa Sh15.9 trilioni, kiwango ambacho ni cha juu
kabisa kwa nchi kukopa kutoka kwenye masoko ya kimataifa. Amesema
taarifa za BoT zinaonyesha kuwa deni la ndani limefikia Sh5.1 trilioni
hadi kufikia Oktoba mwaka jana na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko
la Sh513 bilioni tangu mwaka 2011.
“Deni la ndani linakua kwa
kasi kubwa kwa sababu Serikali imeanza kukopa kwenye benki za biashara
ambazo zinatoza riba kubwa. Hii ni hatari kwa uchumi wa nchi,” anasema
Mwakagenda.
Vizazi vijavyo kulipa deni
Dk Prosper Ngowi,
kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro anasema deni siyo kitu kibaya ila
tatizo likuja endapo fedha zilizokopwa zimetumika vibaya.
“Deni
hili ni kubwa na hali ni mbaya kwa kuwa litalipwa na riba na haliwezi
kumalizika leo litaendelea hadi kizazi kijacho,” amesema Dk Ngowi.
Kwa
upande wake Profesa Humfrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
anasema ni lazima tujiulize deni hilo linatokana na miradi gani.
“Tuangalie
fursa za kukopa na tupunguze matumizi yasiyokuwa ya lazima kama magari
ya kifahari, safari zisizokuwa za lazima, kuwa na wajumbe wengi katika
mambo madogo,” ameshauri Profesa Moshi.
Wakati wataalamu hao
wakizungumza hivyo, takwimu za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Mahusiano
na Uratibu Stephen Wasira, alipowasilisha bungeni taarifa ya hali ya
uchumi kwa mwaka 2011 na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2012/13—
zilionyesha kwamba pato la Taifa lilikuwa kwa Sh37.5 trilioni.
Hii
inatokana na idadi ya watu Tanzania Bara, ambao wanakadiriwa kufikia
43.2 milioni mwaka 2010 na watu milioni 44.5 mwaka 2011, na pato la
wastani la kila mtu lilikuwa Sh869,436.3 mwaka 2011. Mbali na hayo
ukuaji halisi wa pato la Taifa ulikuwa kwa asilimia 6.4 mwaka 2011
ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010.
Hivi sasa idadi ya
watu inaongezeka kwa asilimia 2.6 kwa mwaka, kwa kipindi cha mika kumi
iliyopita Watanzania milioni 10 waliongezeka.
Rais Jakaya Kikwete anasema idadi ya watu inakuwa kwa kiwango kikubwa na kwamba ongezeko lijalo litakuwa mzigo mkubwa kwa Taifa.
Kwa
mujibu wa Rais kama ongezeko hilo litaendelea, ifikapo mwaka 2016,
Tanzania itakuwa na watu 51 milioni kiwango kisichokidhi mahitaji halisi
ya uchumi na mipango mengine.
Ongezeko hilo lisiloendana na kiwango
cha uzalishaji linatia shaka zaidi huku msongomano wa watu katika miji
mikubwa ukiendelea kuwa mkubwa, kwa mfano Dar es Salaam ina watu 2, 294
kwa kilometa moja ya mraba, ikifuatiwa na Mwanza watu 186 na Kilimanjaro
126.
Wasiwasi wa Rais unakuja huku Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudentia Kabaka akitoa ripoti mwezi machi mwaka jana kwamba kiwango cha
ukosefu wa ajira nchini ni asilimia 11.7 kwa watu wenye umri wa kuanzia
miaka 15 na kuendelea.
Wasira anasema vijana walioajiriwa wenye
umri wa miaka 15 hadi 34 ni milioni 9.5 sawa na asilimia 86.6 na vijana
wasio na ajira ni milioni1.4 sawa na asilimia 13.4 ya nguvukazi yote ya
taifa.
Mbali na hayo Dk Ngowi anasema watu 1.6 milioni tu ndiyo
wanaolipa kodi, na wengine wasiolipa huku idadi kubwa iliyobaki ikiacha
mzigo huo kwa watu wachache.
Dk Ngowi anasema ili kujinasua na
janga hilo, serikali inatakiwa kukusanya mapato ya kutosha ya ndani,
lakini pia ijiepushe na matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Kuhusu elimu
kutolewa bure, Dk Ngowi anasema mpango huo unatia shaka kwa kuwa
Tanzania nchi maskini hivyo huduma za elimu bure, itakuwa na uwalakini.
Anabainisha kwamba ni bora elimu iwe ya kulipia, lakini iwe ya kiwango kinachotakiwa.
Serikali ikope kwa nidhamu
Naye
Profesa Moshi alitahadharisha kuwa kama nchi itaendelea kuwa na madeni
makubwa kiasi hicho, basi itashindwa kupiga hatua katika maendeleo yake
ya kiuchumi kwa miaka ijayo.
“Nchi inapokuwa na deni kubwa kama hili,
inaweza kuzuia wawekezaji wasije, kwa sababu watalazimishwa kulipa kodi
kubwa ili kupunguza deni la nchi. “Tukope endapo kuna suala la muhini
na ni lazima kufanya hivyo,” anasema Profesa
Kauli za wataalamu
hao wa uchumi zinaoana na ile ya Mwakagenda ambaye pia anasema serikali
inapaswa kufikiri mara mbili kabla ya kuamua kukopa, na kuwapo kwa
nidhamu katika kukopa kwa kuwa deni hilo limevuka kiwango cha kimataifa.
Katika
mapendekezo yake Mwakagenda anasema umefikia wakati kwa Serikali
iruhusiwe kukopa baada ya ya Bunge kujadili kwa sababu mikopo mingi
haina faida zaidi ya kuwaumiza wananchi.
Profesa Moshi
anatahadharisha serikali isije kuomba kufutiwa madeni kama mwaka 2000
kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC).
Wakati
deni hilo likiwa kubwa kiasi hicho, malengo ya uchumi na mendeleo ya
jamii kwa Serikali katika mwaka 2012/13 ni pato la taifa kukua kutoka
asilimia 6.8 na kufikia asilimia 8.5 mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment