Thursday, November 28, 2013

SASA WEKINDU WA MSIMBAZI WACHUKUA BEKO WA YANGA NA ATAKUJA IJUMAA HII



NewDocument_951f5.jpg
SIMBA imemtumia tiketi ya ndege kipa wa zamani wa Yanga, Yaw Berko na atatua jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa kufanya mazungumzo ya mwisho na klabu hiyo ya Msimbazi.
Mwanaspoti linaweza kuthibitisha pasipo shaka kuwa Berko atatua kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Kenya kwa ajili ya kufanya makubaliano ya kuidakia Simba kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaoanza Januari 25 mwakani.
Simba imepanga kumpa mkataba wa miezi sita Berko ambao utakwisha Juni mwakani na kuwepo kwake kutategemeana na kanuni mpya za Ligi Kuu Bara kwani huenda kusiwe na makipa wa kigeni kuanzia msimu ujao kama kanuni mpya zitaanza kutumika.
Tayari uongozi wa Simba umempa maagizo kipa wao wa sasa raia wa Uganda, Abel Dhaira kumtaka atafute timu nyingine kutokana na kupungua kiwango pamoja na gharama kubwa.
Mmoja wa waandishi maarufu wa Ghana aliliambia Mwanaspoti jana Jumatano kuwa Berko amepokea tiketi hiyo na atatua katika ardhi ya Tanzania Ijumaa.
Berko alipopigiwa simu kuthibitisha habari hizo, kwanza aliguna, halafu akazungumza kwa Kiswahili; "Wewe nani? Baada ya mwandishi kujitambulisha na kumuuliza kuhusu suala la kujiunga Simba alicheka halafu akasema: ''Nipigie baadaye tuzungumze nipo mazoezini." Hata hivyo hakupatikana tena.
Viongozi wa Simba walionekana kushangazwa kila walipotafutwa kuthibitisha hilo, huku wengi wakisema hawana habari na hilo.
Hata hivyo, uchunguzi wa ndani wa Mwanaspoti unaonyesha kuwa Berko ameipokea tiketi ya ndege aliyotumiwa na Simba na atatua kesho Ijumaa kufanya mazungumzo na klabu hiyo ya Msimbazi.
Berko aliondoka Yanga mwaka huu baada ya klabu hiyo ya Jangwani kumpa dola 7,500 (Sh 12 milioni) alizokuwa anawadai kutokana na kuvunja mkataba.
Yanga ilimtoa Berko kwa mkopo kwenda FC Lipopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili wabadilishane na Mnyarwanda Kabange Twite, pacha wa kiraka wa klabu hiyo, Mbuyu Twite, lakini mpango huo ulishindikana msimu uliopita.
Baadaye kipa huyo bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2011/12 alibaki Jangwani lakini bila kucheza akawa mtu wa kujifungia chumbani muda wote makao makuu ya Yanga.
Berko, ambaye matarajio yake ya mbele ni kuwa mchungaji wa kanisa alipokuwa anawaaga mashabiki wa Yanga mapema mwaka huu, alisema anaondoka Jangwani, lakini kuna siku watamkumbuka.
"Nimefanya kazi vizuri na Yanga na sasa narudi nyumbani kufanya mambo mengine, nitawakumbuka sana, na Yanga najua watanikumbuka sana," alisema Berko alipokuwa anaondoka.
Akiwa Yanga, Berko anakumbukwa kuwa kipa imara klabuni hapo na akawa kipa bora wa ligi msimu wa 2010/2011, ingawa nyota yake ilififia alipokuwa na majeruhi ya bega yaliyokuwa yanamweka benchi mara kwa mara hali ambayo ilizua utata kuwa alikuwa anafanya makusudi.
Berko alijiunga na Yanga mwaka 2009, akitokea Liberty Proffessional ya kwao Ghana, timu ambayo ilimuibua pia Michael Essein na nyota wengine kibao wa Ghana. Aliletwa nchini na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic aliyewahi kufundisha katika klabu ya Hearts of Oak ya huko.
Berko anajivunia kuiwezesha timu kutwaa mataji ya ubingwa wa Bara msimu wa 2010/2011 na Kombe la Kagame mara mbili mfululizo; 2011 na 2012.
Mwaka 2011 alidaka mechi zote Kombe la Kagame, lakini 2012 alidaka hadi robo fainali alipoumia na kumuachia Ally Mustafa 'Barthez' aliyedaka hadi ubingwa.
Chanzo:Mwanasport mtandaoni

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...