USAJILI WA OKWI YANGA WAZUIWA
Shirikisho
 la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji 
Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri 
ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati
 ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo (Januari 22 
mwaka huu) kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya
 kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali 
maalumu kutoka FIFA.
Okwi
 ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia 
aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional 
permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi
 ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Katika
 FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi 
ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel 
imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du 
Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola
 za Marekani 300,000.
Hivyo,
 TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza 
Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika 
shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.
MECHI ZA TANZANIA PRISONS YAZASOGEZWA
Shirikisho
 la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesogeza mbele mechi za raundi ya 14
 na 15 zinazoihusu timu ya Tanzania Prisons zilizokuwa zichezwe Januari 
25 na 29 mwaka huu.
Awali
 Tanzania Prisons ilitakiwa kutafuta uwanja mwingine wa kuchezea mechi 
hizo dhidi ya Ruvu Shooting na JKT Ruvu kutokana na Uwanja wa Kumbukumbu
 ya Sokoine kutokuwa tayari kwa Ligi Kuu ya Vodacom wikiendi hii.
Mechi hizo sasa zitachezwa kati ya Februari 6 na 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Sokoine.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)



                   Said Ramadhani Bwanamdogo