Thursday, March 17, 2016

Wazee kulipwa pension zao kuanzia april Zanzibar

ZANZIBAR


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia mwezi April mwaka huu, itaanza kulipa pensheni kwa wazee wote wenye umri wa kuanzia miaka sabini ili kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili wazee waishio visiwani humsheinMpaka sasa jumla ya shilingi bilioni moja nukta tano zimetengwa kwa ajili ya malipo ya miezi mitatu ya pensheni hiyo kabla ya kuisha kwa mwaka huu wa fedha, kipindi ambapo Baraza la Wawakilishi litapitisha kiwango kipya cha pesa za pensheni kwa mwaka ujao wa fedha.

Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Salum Rashid Mohemmed, amesema hayo leo katika mkutano wa kitaifa ulioandaliwa na asasi ya HelpAge International tawi la Tanzania, kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa sheria za kimataifa na za kikanda, za usimamizi na ulinzi wa haki za wazee ambazo Tanzania kama nchi imeziridhia.

Kwa mujibu wa Bw. Mohammed, takribani wazee elfu ishirini watanufaikia na mpango huo ambapo kila mmoja atapatiwa kiasi cha shilingi elfu ishirini kila mwezi huku kiwango cha pensheni kikitarajiwa kupanda kulingana na hali ya uchumi itakavyokuwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Help Age Tanzania Bw. Smart Daniel, amesema kuna haja ya Tanzania Bara kuiga mpango huo wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwani wazee nchini wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi huku sababu kuu ikiwa ni hatua ya serikali kutosaini sheria ya wazee takribani miaka kumi na tatu tangu bunge litunge na kuipitisha.

Akinukuu ripoti ya mwaka jana ya hali ya wazee duniani; Bw. Daniel amesema hali ya wazee nchini sio nzuri kwani katika ripoti hiyo, Tanzania imeshika nafasi ya tisini na moja kati ya nchi tisini na sita zilizofanyiwa utafiti.

Aidha, amesema licha ya wazee kukabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, wao ndio wamekuwa walezi wa kundi kubwa la wajukuu ambao wengi wao ni watoto yatima, sambamba na kuwa na jukumu la kuhudumia watoto na wajukuu wao walioathirika kwa ugonjwa hatari wa ukimwi.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...