Saturday, June 15, 2013

MKUTANO WA CHADEMA WASHAMBULIWA KWA BOMU BOMU LAJERUHI NA KUUA


Habari zilizotufikia zinaeleza kuwa watu wawili wanasadikiwa kufa mkoani Arusha na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni za udiwani  kushambuliwa kwa bomu katika viwanja vya Kaloleni.
MAJERUHI WAKIWA HOSPITALI
Watu wawili wanahofiwa kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu lililolipuka kwenye mkutano wa CHADEMA katika eneo la Soweto, kata ya Kaloleni jijini Arusha, wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani katika maeneo ya jiji hilo.

Waliojeruhiwa wamekimbizwa katika hospitali za Seliani na Mount Meru ambapo baadhi ya watu waliojitolea wanashirikiana na Madaktari na Wauguzi wa hospitali hizo kutoa huduma ya kwanza.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Liberatus Sabas yupo katika moja ya hospitali hizo
.
   
 Bomu hilo linaelezwa kuwa lilitupwa kwenye mkusanyiko wa watu, lilipuka mwendo wa saa kumi na mbili na robo jioni wakati mkutano huo ulipokuwa umekwisha na shughuli ya kukusanya michango ikiendelea.
Viongozi wa juu wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwepo na wameendelea kuwepo kwenye eneo baada ya mlipuko huo. 

 
Polisi wapo katika eneo hilo wakijitahidi kutuliza ghasia lakini inasemekana upo upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi wanaojaribu kuwafukuza, hali iliyowalazimu kupiga mabomu ya machozi na kukamata watu kadhaa wakiwemo viongozi wa CHADEMA. Mwandishi mmoja wa habari anaripotiwa kunyang’anywa kamera yake baada kwa kupiga picha, hata baada ya kujitambulisha. 

Majeruhi. Mungu urehemu tz

Arusha. Mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Arusha, jana ulivunjika baada ya bomu kulipuka na kuua watu wanne na wengine kujeruhiwa.
Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Hilo ni tukio la pili la bomu kulipuka katika mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru Frida Mokiti alisema katika hospitali yake kuna maiti moja ya mtoto na majeruhi 11.
Habari zingine zilisema katika hospitali ya Misheni ya Selian kuna maiti za watu wawili, waliokufa kutokana na shambulio hilo na majeruhi ambao idadi yao haijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema katika tukio hilo watu wawili wamepoteza maisha, mwanamke na mwanamume na kwamba idadi ya majeruhi bado haijafahamika kwa kuwa wametawanywa katika hospitali mbalimbali mkoani humo.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa bomu hilo lililipuka karibu na jukwaa walilokuwa wamekaa viongozi wa Chadema, wakati Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakiwa katika hatua za kumaliza kuhutubia.
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto hali iliyozidisha taharuki.
Baada ya tukio hilo watu waliokuwa katika mkutano huo walitawanyika wakikimbia kuokoa maisha yao huku wakimwacha Mbowe na Lema na viongozi wengine wakiwa bado wako jukwaani.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za mji wa Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia ovyo.
Hali hiyo ya watu kukimbia ovyo kuliwafanya askari polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi hali ambayo ilizidisha taharuki.
Baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wengine katika Hospitali ya Seliani na wafuasi wa Chadema na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo.
Miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo la mlipuko wa bomu ni Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Selian.
Mbowe akizungumza katika hospitali ya Selian jana aliwataka wanachama wa chama hicho watulie kwa sababu tukio hilo ni kubwa na lina mambo mengi ndani yake.
Alisema wanachofanya sasa ni kuhakikisha kuwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo wanapata matibabu kwanza.
Mbowe aliwataka watu wote waliopotelewa na ndugu kufika katika hospitali zote za mji wa Arusha kutambua ndugu zao waliojeruhiwa.
Alisema Chadema itagharimia matibabu ya watu wote waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Mbowe alisema chama chake kwa sasa hakiwezi kutoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo la bomu kwa sababu wanafuatiliwa na baadhi ya askari polisi na maofisa wa Usalama wa Taifa.
Katika hospitali ya Selian, Mganga wa zamu, Dk Ekenywa alisema kuwa hospitali hiyo imepokea majeruhi 25 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.
Waandishi wa habari walishuhudia baadhi ya wanachma wa Chadena pamoja na viongozi wao akiwamo Mbowe wakitoa damu kwa ajili ya majeruhi.
Awali Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alihitimisha kampeni kwa chopa katika Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli na kukumbana na mkutano wa kampeni wa CCM uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa.
Viongozi hao, walifanya mikutano katika kata hiyo na kila chama kilitamba kushinda leo na kuwaondoa wananchi na hofu za kutokea vurugu.
Mbowe licha ya kufanya mkutano huo, pia alifanya mikutano katika Kata ya Kaloleni Uwanja wa Soweto mjini Arusha na mamia ya wakazi wa Arusha wa kata zote nne na mkoani Manyara, katika kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata mbalimbali nchini.
Uchaguzi mdogo wa kata nne za Jiji la Arusha na Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli, unatarajiwa kufanyika leo.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...