 
  
            
Wakazi wa mji mdogo wa Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro  
wakiwakimbia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)  katika barabara
 ya Dodoma-Morogoro juzi. Picha na Juma Mtanda 
            
WATU wanane wameuawa na wengine kumi na moja kujeruhiwa kutokana
 na vurugu zilizizotokea jana mkoani Mtwara na Itete wilayani Ulanga, 
mkoani Mororgoro.
 
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya 
Masasi, Mkomaindo, Amima Simbo alithibitisha vifo vya watu saba 
waliofikishwa hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa muuguzi huyo, maiti zilizopokelewa 
hospitalini hapo zilionekana zikiwa na matundu yanayodhaniwa kuwa ni ya 
risasi, baadhi yao kichwani, begani, viunoni na tumboni.
Aidha majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo pia walikuwa na majeraha mbalimbali ikiwamo ya risari.
Habari zaidi zinaeleza kuwa vurugu hizo zilizuka 
baada ya kundi la waandamaji, wengi wakiwa vijana waendesha pikipiki 
maarufu kama bodaboda waliokuwa wakipinga mwenzao kukamatwa na kutaka 
kuvamia Kituo cha Polisi ili kumwokoa.
Vurugu hizo ziliendelea kuutikisa Mkoa wa Mtwara 
kwa siku ya pili mfululizo na kuutikisa Mkoa wa Mtwara, baada ya vurugu 
nyingine kuibuka wilayani Masasi jana.
Habari zinasema mbali na vifo na majeruhi, nyumba 
za wabunge wawili wa wilaya hiyo zimechomwa moto, ambapo pia magari, 
trekta, Ofisi za CCM Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya 
ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.
Wabunge ambao nyumba zao zimemwa moto ni Mariam Kasembe wa Masasi Mjini na Anna Abdallah Mbunge wa Viti Maalumu wilayani humo.
Juzi vurugu hizo zilitokea katika Mikoa ya 
Morogoro kati ya wakulima na wafugaji na kusababisha kifo cha mtu mmoja 
wakati mkoani Mtwara wananchi  wa eneo la Chikongola waliizingira nyumba
 ya diwani wa Kata ya Mikindani, Mohamedi Chehako kwa madai ya 
kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.
Katika vurugu hizo polisi walilazimika kutumia 
silaha yakiwamo mabomu ya machozi ili kupoza hali ya hewa, ambapo nyumba
 ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za 
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia ilichomwa moto.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili kuhusu vurugu 
hizo, Mbunge wa Masasi Mjini, Mariam Kasembe alisema kuwa nyumba yake 
iliyoko Masasi mjini imechomwa moto na kuteketea kabisa, huku mali 
zikiibwa na kwamba familia yake sasa haina makazi.
Aliongeza kwamba mbali na uharibifu, vurugu hizo zimesababisha pia mama yake mzazi kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo.
“Wamechoma trekta na gari lililokuwepo nyumbani 
kwangu, watoto wangu na mume wangu walipoona hali hiyo wakakimbia,” 
alisema Kasembe akieleza kuwa hawezi kuthibitisha chanzo cha vurugu 
hizo, lakini anahisi kuwa zinatokana na mgogoro wa gesi.
Alifafanua kwamba watu hao walifanya uharibifu huo baada ya 
kupanga njama huku wengine wakiwa wamekizingira Kituo cha Polisi, ili 
kuwazuia wasiende kuisaidia familia yake.
“Ofisi ya Bunge ilitaka kunisafirisha ili 
nikaangalie hali ilivyo, lakini wapigakura wangu na ndugu wameniambia 
nisiende ili kulinda usalama wangu,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti 
Maalum (CCM), Anna Abdalla alisema nyumba yake iliyopo eneo la Masasi 
mjini imechomwa moto katika vurugu zilizotokea jana.
“Ni kweli nyumba yangu nimesikia imechomwa moto, lakini sijui kinachoendelea,” alisema.
Mkazi
 wa Kijiji cha Chikunja, alipozaliwa Kasembe, Anna Martin aliliambia 
gazeti hili kuwa kundi jingine la vijana lipo katika harakati za kutaka 
kuichoma nyumba ya mbunge huyo, hali iliyosababisha wanafamilia wa 
mbunge huyo kutoka nje.
Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Idi Mkwachu, 
ambaye ni Mkandarasi wa Wilaya hiyo alisema kuwa vurugu hizo zilianza 
saa mbili asubuhi jana, ambapo kundi la watu lililokuwa likizunguka 
mitaani lilikuwa  likiimba nyimbo za kuitaka Serikali ilipatie ufumbuzi 
suala la gesi.
Mkwachu alisema kuwa suala la gesi limezua uadui 
mkubwa kati ya wananchi na Serikali huku akidai kuwa kuna siri 
imebainika kuwa wabunge wanaoshinikiza gesi itoke Mtwara, wamepewa 
mamilioni ya fedha na Serikali.
“Kwa mfano gridi ya taifa ingeanzia Mtwara 
ingekuwa ni karibu zaidi kuliko gridi hiyo kujengwa katika eneo jingine.
 Mbona  kujenga bomba ni gharama kuliko gridi hiyo?,” alisema Mkwachu.
Alisema kwamba Serikali inavyochukua muda mrefu 
kutoa suluhu ya mgogoro huo, inajipalia makaa kwa sababu mikoa ya Mtwara
 na Lindi imebobea katika umaskini kwa miaka mingi.
Mkwachu alisema 
kuwa hadi kufikia jana saa kumi jioni, baadhi ya majengo yalikuwa 
yakiendelea kuteketea kwa moto, huku askari kutoka Nanyumbu na 
Nachingwea wakiletwa ili kusaidia kutuliza ghasia hizo.
Maaskofu watoa tamko
Wakati 
hayo yakiendelea, Baraza  la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (PCT) 
Mkoani Mtwara, limetoa tamko likiitaka  Serikali isitishe mpango wake wa
 kusafirisha  gesi  kutoka Kijiji cha Msimbati mkoani humo, kwenda 
Kinyerezi Dar es Salaam.
Tamko hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza
 hilo, Charles Chilumba walipozungumza na waandishi wa habari katika 
klabu ya waandishi wa habari Mtwara (MTPC), iliyopo mjini humo.
Chilumba alisema kuwa Serikali inatakiwa kuwa 
sikivu na kusikia kilio cha wananchi wa Mikoa ya Kusini  ya Lindi na 
Mtwara, ambako vyanzo vya uchumi wa gesi vipo ili kutekeleza madai yao.
Alisema
 kuwa, viwanda vya mbolea, plastic na saruji ambavyo viliahidiwa 
kujengwa, vijengwe sasa na zisiwe propaganda za kisiasa kutoka kwa 
viongozi wa Serikali, ili  kuondoa dhana iliyokuwapo miaka ya nyuma kuwa
 kusini ni  ukanda wa vita, hivyo hakuna sababu ya kuendelezwa.
“Serikali isisikilize wabunge wadanganyifu, ambao 
hawana makubaliano na wananchi katika majimbo wanayotoka, ambao 
huchochea mgogoro huu kwa lengo lao na masilahi yao binafsi,”alisema 
Chilumba.
”Inabidi wawaombe radhi bila masharti kwani semi 
zao  zinaleta chuki, uhasama, utengano katika nchi na kusababisha nchi 
isitawalike. Serikali ya CCM itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 
Ibara ya 63 kifungu H na K,”alisema.
                    
Viongozi wa dini hao wameomba Mungu awape hekima viongozi wa  
Serikali kwa kuwa wamepewa dhamana na Mungu kuliongoza taifa kwa 
umahiri, wakionya kuwa ukaidi wa wenye fitina utawaangamiza.
Alipotafutwa msemaji wa Jeshi laPolisi nchini, 
Advera Senso alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo na kuomba 
atafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Maria Nzuki.
“Sawa lakini, naomba umtafute Kamanda wa Polisi wa Mtwara yeye ndiye ataweza kukujibu unachokiuliza,” alisema Senso.
Hata hivyo gazeti hili lilimtafuta Nzuki bila mafanikio kwani simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alipotafutwa alisema kuwa yeye siyo msemaji.
“Mimi siyo msemaji wa masuala hayo, mtafute Waziri (Emmanuel Nchimbi) yupo atazungumzia hilo,” alisema Silima.
Waziri Nchimbi naye kama ilivyokuwa kwa Kamanda Njiku, simu yake ya mkononi jana ilikuwa haipatikani.
Morogoro
Mkoani Morogoro mtu 
mmoja anayeaminika kuwa ni mfugaji katika Wilaya ya Itete, mkoani 
Morogoro ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kundi kubwa la 
wafugaji kuvamia viongozi wa halmashauri waliokamata mifugo yao kwa 
madai ya kulisha maeneo yaliyozuiwa.
Tukio hilo limetokea jana asubuhi baada ya 
viongozi wa eneo la Itete wilayani Ulanga, kupata taarifa kuwa kuna 
makundi ya mifugo yaliyokuwa yakilishwa ndani ya hifadhi ya ardhi oevu, 
ambayo Serikali imepiga marufuku kulisha mifugo.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja aliyekuwapo kwenye 
operesheni ya kukamata mifugo hiyo na ambaye hakupenda jina lake 
liandikwe gazetini, alisema kundi hilo kubwa la wafugaji wakiwa na 
silaha za jadi waliwavamia na kuanza kuwashambulia kwa lengo la kuchukua
 mifugo yao iliyokuwa imekamatwa.
Alisema kwamba viongozi hao wa halmashauri 
walipewa taarifa ya kuwepo kwa mifugo hiyo katika eneo hilo na 
walipofika waliikuta mifugo hiyo na kuamua kuichukua kisha kuipeleka 
kwenye makambi yaliyotengwa kuhifadhi mifugo wilayani hapo.
“Baada ya kuchukua mifugo ile, wafugaji walipata 
taarifa kuwa tumeikamata mifugo yao, ndipo walipojikusanya na kutuvamia 
tukiwa njiani na kuanza kutushambulia,” alisema ofisa huyo.
Aliongeza kuwa katika kundi hilo la viongozi wa 
wilaya, walikuwa na askari wawili tu, huku mmoja ndiye aliyekuwa na 
bunduki, ambapo licha ya kupiga risasi hewani kuwatawanya, wafugaji hao 
walizidi kuwashambulia.
“Askari yule alipoona maisha yake yako hatarini ndipo alipoanza 
kuwafyatulia risasi wananchi hao na kumpata mmoja na kufariki huku 
wengine wote kukimbia,” alieleza
Wakati huo huo, zaidi ya wafugaji 400 wa Kijiji 
cha Mabwegele Kata ya Kitete, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa 
walikusanyika katika kijiji hicho wakipinga kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa 
Morogoro, Joel Bendera ya kutenguliwa uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa
 kukipandisha hadhi na kuwa kijiji kamili, jambo ambalo lilizua vurugu 
kubwa katika mji mdogo wa Dumila jana.
Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Kijiji 
cha Mabwegere wilayani Kilosa, Sharifu Kasenga alisema kuwa wafugaji hao
 wamekusanyika katika kijiji hicho baada ya kusikia taarifa za uharibifu
 wa mali za wafugaji katika mji wa Dumila wakati wa vurugu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine 
Shilogile alilieleza gazeti hili kuwa hali ya amani imerejea katika mji 
mdogo wa Dumila pamoja na kitongoji cha Mabwegere.
Imeandikwa na Florence Majani, Dar Mwanja Ibadi, Masasi, Juma Mtanda, Venance George, Morogoro