Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa amesema kuwa kuanzia mwaka huu hadi 2015, chama chake kitaipeleka mchakamchaka CCM, kwa kuwa chama chake kimefanikiwa kuwaamsha Watanzania.
Alisema kwamba Watanzania sasa wameamka na
kutambua utajiri wa nchi yao na jinsi rasilimali zinavyotoroshwa nje
ya nchi na kuanza kudai kufaidika nazo kwa nguvu. Hivyo Chadema
kitaitumia fursa hiyo kuipeleka puta CCM, lengo likiwa kuhakikisha kila
Mtanzania anaishi maisha bora.
Dk Slaa alisema hayo alipokuwa akizungumza katika
kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini, ambao ni wafuasi
wa chama hicho (CHASO), lililofanyika Dar es Salaam jana.
Alieleza kuwa kinachotokea mikoa ya Lindi na
Mtwara, pamoja na maandamano ya hivi karibuni ya wanafunzi wa Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM) ni majibu tosha kwa CCM, kwamba mikutano ya
Chadema iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini imewaamsha wananchi.
Wanafunzi zaidi ya 500 walihudhuria kongamano hilo
kutoka IFM, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu (DUCE) na Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),
pamoja na vyuo mbalimbali vilivyopo Dar es Salaam na mikoani.
Desemba 18 mwaka jana Mwenyekiti wa Chama hicho,
Freeman Mbowe alisema kuwa mwaka huu utakuwa ni wa kuunganisha nguvu ya
umma kitaifa, baada ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa
kuzifanyia kazi hoja mbalimbali zinazotolewa na chama hicho.
Dk Slaa ambaye alitumia saa 1:06 kuzungumza na
wanafunzi hao, alisema kuwa elimu ya uraia waliyoitoa kwa wananchi
katika mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), pamoja na Operesheni
Sangara, wamefanikiwa kwa asilimia 99.
“Tumewapa elimu ya uraia wananchi katika mikoa
yote nchini na sasa wanajua haki zao,.Hiyo ni kazi na mikutano yetu
pamoja na maandamano tuliyoyafanya” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Nawapongeza wanafunzi wa IFM kwa kuandamana,
najua wapo watakaosema nachochea maandamano, lakini wanatakiwa kujua
kwamba wanafunzi hawa walikuwa na haki, haiwezekani wanabakwa kisha
wakae kimya, tena wametoa taarifa polisi na hakuna kilichofanyika.”
Mbali na kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
IGP Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova kujiuzulu kwa kitendo cha kuamuru wanafunzi wa IFM
kupigwa wakati walikuwa wakililia usalama wao, alisema kwamba kuna
tofauti kubwa kati ya vurugu na kudai haki za msingi.
“Inakuwaje polisi wanawapiga mabomu wanafunzi
wanaofanya maandamano, lakini wanashindwa kuzuia Twiga wanaotoroshwa nje
ya nchi, tuungane, tushirikiane na tupige kelele, ili mali zetu
zirudi,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Wananchi wa Mtwara na Lindi sasa wanaandamana kutaka gesi iwanufaishe wao kwanza
Hayo yote ni matokeo ya elimu ya uraia tuliyoitoa nchi nzima. Hivi sasa wananchi hawaogopi wanasema ukweli.”
Alisema kitendo cha Watanzania kudai rasilimali za nchi yao kitafanya rasilimali hizo zitumike kwa maendeleo ya wananchi.
Alifafanua kuwa rasilimali za nchi ya Japan, Canada na Italia zilitumika kujenga nchi hizo na sasa zina utajiri mkubwa, lakini rasilimali za Tanzania zinapakizwa katika ndege ya kupelekwa kusikojulikana.
Alisema kitendo cha Watanzania kudai rasilimali za nchi yao kitafanya rasilimali hizo zitumike kwa maendeleo ya wananchi.
Alifafanua kuwa rasilimali za nchi ya Japan, Canada na Italia zilitumika kujenga nchi hizo na sasa zina utajiri mkubwa, lakini rasilimali za Tanzania zinapakizwa katika ndege ya kupelekwa kusikojulikana.
“Rais Paul Kagame wa Rwanda aliibadilisha nchi
hiyo kwa sababu hana utani, kwetu Tanzania watu hawawajibishwi, utani
umejaa kila kona,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa
kuangalia maendeleo ya mkoa mmoja tu, huku akisisitiza sera ya majimbo
kuwa ni sahihi na ikitumika itaweza kuliletea taifa maendeleo makubwa.
Dk Slaa alisema kwamba Serikali ya CCM iliahidi
maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini hadi sasa kuna Watanzania
wanaoshindwa kulipa kodi ya nyumba na wanakula mlo mmoja kwa siku.
“Ngoja niwaeleze kitu, tafiti zinaonyesha kuwa
asilimia 3 ya matajiri nchini wanamiliki asilimia 97 ya rasilimali za
taifa hili, tutaipigisha mchakamchaka CCM mwaka huu hadi 2015,” alisema
Dk Slaa.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya alisema kuwa
kuna mchezo unafanywa na CCM ili Katiba Mpya iwe na mlengo wa chama
hicho na kufafanua kuwa wanasubiri rasimu ya Katiba itolewe na kwamba
ikiwa itakuwa sawa na mapendekeo yaliyotolewa na chama hicho tawala,
hawataikubali.
Akizungumzia nidhamu ndani ya chama hicho alisema:
“Chadema ni tumaini la Watanzania, hivyo hatuwezi kuwa na wanachama au
viongozi wasio na nidhamu, kama ni demokrasia basi inatakiwa kuishia
pale inapoishia pua yao.”
Urais 2015
Akizungumzia urais 2015, kiongozi huyo alisema kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, kazi aliyopewa ni kukijenga chama hicho na siyo vinginevyo.
“Tangu 2010 kazi niliyopewa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kukijenga chama na siyo kuangalia urais, hao wanaozungumzia urais shauri yao,” alisema Dk Slaa.
Akizungumzia urais 2015, kiongozi huyo alisema kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, kazi aliyopewa ni kukijenga chama hicho na siyo vinginevyo.
“Tangu 2010 kazi niliyopewa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kukijenga chama na siyo kuangalia urais, hao wanaozungumzia urais shauri yao,” alisema Dk Slaa.
No comments:
Post a Comment