Saturday, January 19, 2013

HAYA SASA BAADA YA KULA ZOEZI LA KUTOSHA WAKIWA NCHINI UTURUKI LEO YANGA KUWAONESHA KIWANGO WATANZANIA DHIDI YA BLACK LEOPARD YA AFRICA KUSINI

Kikosi cha Yanga kikifanya mazoezi kilipokuwa ziarani nchini Uturuki
OLIVER ALBERT
YANGA inashuka kwenye Uwanja wa Taifa leo Jumamosi kuwaonyesha mashabiki mavitu ya Uturuki kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Black Leopards ya Afrika Kusini lakini kocha Ernest Brandts amewataka wachezaji kushinda mechi nane tu kuiziba mdomo Simba.

Leopards imecheza mechi 17 kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini na kuambulia sare nane, imepoteza sita na kushinda mechi tatu. Ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa timu 16.

Kocha huyo wa Yanga anaamini ushindi wa mechi hizo nane mfululizo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaoanza Januari 26 utawaweka pazuri dhidi ya wapinzani wao wakubwa Simba na Azam wanaowawinda kileleni.

Yanga iliyokuwa kambini wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itacheza mechi 10 kati ya 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, jambo ambalo linawapa kiburi huku Brandts akiamini kwamba wapinzani wake watateleza tu ndani ya mechi hizo nane na yeye atapeta kwa kuwa yupo vizuri.

"Nafurahi kikosi changu sasa kipo vizuri na ushindani wa namba ni mkubwa hivyo inanipa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mzunguko wa pili wa ligi, na sasa natangaza kuwa tuko tayari kukabiliana na yoyote kwenye ligi hiyo,"alisema kocha huyo ambaye mzunguko wa kwanza ulipokwisha hakwenda likizo akaipeleka timu kambini Uturuki.

"Ingawa hatupaswi kuidharau timu yoyote, kwani hatua hiyo ni ngumu hasa kwa timu zilizo chini ambazo zinapambana kutoshuka daraja na huwa zinakuja uwanjani zikiwa zimepania hivyo tutapaswa kuwa waangalifu.

"Tunaongoza ligi sasa lakini naamini tukishinda michezo nane mfululizo ya kwanza itatupa mwanga wa kutwaa ubingwa, kwani wapinzani wetu wakubwa ni Azam na Simba hivyo lazima kupambana nao vilivyo na kupiga hesabu zetu za ubingwa vizuri ili tusiharibu ingawa najua wapinzani wetu kuna mechi tu watapoteza, kwa kuwa hawako vizuri kama Yanga, "alisema Brandts.

Katika michezo hiyo nane ya mwanzo wa mzunguko wa pili Yanga itacheza na Prisons, Mtibwa, JKT Ruvu, African Lyon, Azam, Kagera Sugar, Toto African na Ruvu Shooting ili kuanza kupiga hesabu za ubingwa kwani itakuwa imefikisha pointi 53 wakati Azam ikishinda michezo nane itakuwa na pointi 48 na Simba watakuwa na 47.

Simba itacheza mechi nne ugenini huku tisa ikicheza jijini Dar es Salaam. Lakini kama Simba na Azam zitapoteza michezo mitatu kama Yanga na Brandts wanavyoombea katika hiyo nane basi Yanga itahitaji pointi mbili tu ili ipate pointi 55 na kutangaza ubingwa kwani hata kama Azam na Simba zitashinda michezo yao mitano iliyobaki haitaweza kufikia pointi 55 za Yanga.

Michezo, ambayo Yanga itacheza kwenye uwanja wao wa nyumbani ni dhidi ya Prisons, Mtibwa, JKT Ruvu, African Lyon, Azam, Kagera Sugar, Toto African na Ruvu Shooting,Oljoro JKT na Simba. Wakati itakazocheza ugenini ni dhidi ya Polisi Morogoro, Mgambo Shooting na Coastal Union.

Yanga imekuwa na ushindani mkubwa wa namba kutokana na wachezaji wake wengi kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, huku wageni Mbuyu Twite, Kabange Twite, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima wakiibua changamoto kubwa kwa wazawa.

Katika hatua nyingine, wanachama wa Yanga watakuwa na mkutano wa kujadili mambo mbalimbali kesho Jumapili kwenye Bwalo la Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...