Monday, January 7, 2013
MTANZANIA ANAYEKIPIGA KATIKA TIMU YA DENIZLISPOR FC YA UTURUKI KUWA VAA YANGA LEO
Waturuki wamchezesha Mtanzania mechi na Yanga YANGA ambayo wachezaji wake wote wapo fiti itaivaa timu ngumu ya Denizlispor FC ya Uturuki kwenye mchezo wa pili wa kirafiki utakaochezwa leo Jumanne saa 10 jioni kwa saa Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Selen Football ulioko eneo la Kalimya nje ya Antalya.
Itavaana na Mtanzania Eric Odhiambo, anayechezea timu hiyo ya Denizlispor.
Katika mechi ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 wikiendi iliyopita dhidi ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani ambayo kocha wake alimtamani sana beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua.
Mechi ya leo Jumanne huenda ikawa ngumu na nzuri zaidi kwa maandalizi ya Yanga kutokana na Waturuki hao kukaa pamoja muda mrefu na kuwa na wachezaji wengi wazoefu tofauti na Arminia ambayo ilikuwa na vijana wengi inaowatengeneza kwa Ligi Daraja la Tatu Ujerumani.
Denizlispor FC ni kati ya timu maarufu mjini hapa iliyoanzishwa mwaka 1966 na ilishuka daraja mwaka 2010 kwa tofauti ya mabao.
Klabu hiyo ina wachezaji wengi wa kigeni akiwamo Mtanzania Odhiambo aliyezaliwa England.
Kikosi hicho kipo chini ya Kocha Mturuki, Engin Ipekoglu kipo mjini hapa tayari kwa Ligi Daraja la Kwanza kuwania kurejea Ligi Kuu ya Uturuki ambayo imekuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuwa na timu ngumu na tajiri Ulaya.
Wachezaji wa Yanga juzi Jumapili jioni walifanya mazoezi mepesi kwenye gym ya Hoteli ya Fame na jana Jumatatu asubuhi walirudi uwanjani huku kila mmoja akionyesha uchangamfu na hakuna majeruhi kwani Athuman Idd na Hamisi Kiiza wapo vizuri.
Yanga ipo kambini mjini hapa hadi Jumamosi usiku itakapoanza safari ya kurejea Dar es Salaam na itawasili Jumapili jioni tayari kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Januari 26.
Wachezaji wa Yanga wamekuwa wakionyesha ushindani mkubwa ingawa mjini hapa kumekuwa na wageni wengi waliopo likizo ambao kila mmoja amekuwa akijishughulisha zaidi na mambo yake ya starehe kuliko kuangalia mpira au kujishughulisha na wachezaji.
Timu kadhaa kutoka barani Ulaya zimepiga kambi kwenye maeneo mbalimbali ya Antalya kutokana na miundombinu mizuri ya viwanja na hoteli pamoja na utulivu wa eneo hilo tofauti na Mji Mkuu wa Istanbul ambako kuna baridi kali kwa sasa.
Hali ya hewa ya Antalya kwa wiki moja sasa ni jua na hakuna mvua na baridi kama awali Yanga ilipowasili hapa na kufanya mazoezi na makoti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment