NUSU ya watu wanaotumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na mimba ama magonjwa ya zinaa, hawajui namna ya kuitumia mipira hiyo, utafiti umeeleza.
Utafiti huo mpya ulifanywa na Dk Stephanie Sanders wa Taasisi ya Kinsley inayohusika na Utafiti wa Masuala ya Jinsia, Jinsi na Uzalishaji katika Chuo Kikuu cha Indiana.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa katika nchi 14 ikiwamo Tanzania katika kipindi cha miaka 16 iliyopita kuanzia mwaka 1995 hadi 2011, watu wengi wamekuwa wakifanya makosa kwa namna mbalimbali katika kutumia kandomu ikiwamo uvaaji.
“Makosa yanayofanywa mara kwa mara na watumiaji wa kondomu ni pamoja na kuingiza kinga hiyo nusu katika uume wakati wa ngono au kuitoa kabla tendo hilo halijamalizika au kusubiri mpaka isinyae,” imesema sehemu ya utafiti huo.
Makosa mengine ni kutoacha nafasi katika ncha ya kondomu kwa ajili ya mbegu za kiume na kuzifungua vibaya katika pakiti yake.
Jambo hilo linalosababisha kucha kuzitoboa na hatimaye kupitisha mbegu au majimaji kwenda kwa mwanamke,” umeeleza utafiti huo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa makosa mengine ni kuigeuza kondomu ndani-nje, kuihifadhi katika sehemu isiyostahili na kurudia kuitumia katika tendo lingine la ngono.
Kuivua vibaya: Asilimia 57 ya watu waliohojiwa, walikiri kuvua kondomu kimakosa baada ya tendo la ngono. Kati yao asilimia 27 walikuwa wanawake na asilimia 31 ni wanaume.
Pamoja na makosa hayo ya uvaaji wa kondomu, watafiti nchini India wanatarajiwa kufanya utafiti mwingine mkubwa kuhusu suala hilo kubaini sababu yake.
Watafiti hao waliamua kufanya uchunguzi baada ya kubainika kuwapo kwa wanaume ambao maumbile yao ni makubwa au madogo kuliko mipira hiyo ya kiume.
Hata hivyo, kondomu zinazopatikana nchini Tanzania hazitofautiani ukubwa.
Dk Sanders alisema makosa yanayofanywa wakati wa kutumia mipira hiyo yanachochewa na watumiaji wenyewe na kukosekana kwa msisitizo wa elimu ya namna ya kuzitumia kondomu hizo kutoka kwa watengenezaji au taasisi za Ukimwi.
Makundi tofauti yalijumuishwa katika utafiti huo wakiwemo wanandoa, wafanyabiashara ya ngono na wanafunzi wa vyuo.
Kati ya asilimia 17 na 51.1 ya watu walioulizwa maswali katika utafiti huo walikiri kuwa huingiza kondomu nusu katika uume wakati wa tendo la ngono.
Dk Sander alisema: “Kuvaa kondomu nusu uume hakuzuii maambukizi kwa sababu majimaji huwepo wakati wote wakati wa kitendo hicho na si wakati mwanamume au mwanamke anapomwaga mbegu zake tu.”
Matokeo mengine yalionyesha kuwa kati ya asilimia 1.5 na 24.8 ya watu waliowahi kufanya mapenzi kwa kutumia mipira walikiri kuchelewa kuvua mipira hiyo wakati wa tendo.
Aidha, ulibainisha kuwa zaidi ya asilimia 25.3 walikosea kuvaa kondomu kwa kuikunjua kabla ya kuiivaa badala ya kufanya hivyo inapoingizwa katika uume.
Zaidi ya nusu ya watumiaji hao walikiri kuwa walishindwa kuacha nafasi katika ncha au chuchu ya kondomu ambapo mbegu hutakiwa kukaa.
Kati ya asilimia nane na 40.7 walisema wamewahi kukumbana na mkasa wa kondomu kupasuka katikati ya tendo hilo.
“Utafiti wa kina zaidi unahitajika kufanyika katika nchi zinazoendelea kwa sababu huko tuligundua tatizo la kutumia mara mbili kondomu hasa kutokana na umaskini na elimu duni,” alisema Dk Sander.
Utafiti huo ulisema matangazo mengi ya kondomu yanajikita katika kueleza ubora wa kinga hiyo na kusahau kuonyesha matumizi sahihi na salama.
Kauli ya Tacaids
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Morris Lekule amekiri tatizo hilo na akaeleza kuwa kama jitihada za makusudi hazitafanyika kubadili tabia za watu, hili ni janga kwa nchi zinazoendelea.
Aliiambia Mwananchi jana kuwa Watanzania wengi hawajui matumizi sahihi ya mipira hiyo na kuna uzembe katika kulishughulikia suala hilo katika ngazi ya kitaifa.
“Hiyo ni kweli kabisa. Wengi hawajui kutumia mipira ya kiume na ni jambo muhimu watu waelimishwe, uzembe ni wa hali ya juu sana,” alisema Dk Lekule.
Alisema kazi ya Tacaids ni kufanya tathmini ya kondomu zinavyosambazwa maeneo mbalimbali nchini na kudhibiti kiasi kinachotakiwa. Haijihusishi na kufuatilia namna zinavyotumika.
“Kutumia kondomu ni muhimu, lakini matumizi salama ni muhimu zaidi hasa katika nchi zinazoendelea,” alisema Dk Lekule.
Wasemavyo watumiaji
Musa Makyao Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam alisema anayafahamu baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuvaa mipira ya kiume, lakini alisahau kuzingatia wakati wa kuvua.
Yohana Ibrahim, ambaye yeye hutumia kondomu kama njia ya uzazi wa mpango alikiri kuwa kondomu iliwahi kupasuka wakati wa tendo la ndoa.
Mary John, mkazi wa jijini Dar es Salaam alisema yeye havai kondomu, huhakikisha kuwa anamvalisha mwenza wake kabla ya tendo, lakini huwa hazingatii kanuni za matumizi salama ya mipira hiyo.Shirika la Afya Duniani (WHO) linathibitisha kuwa kondomu inaweza kuzuia mimba na magonjwa ya zinaa kwa asilimia 98, imebainishwa kuwa watumiaji wengi wa mipira hiyo hawaitumii ipasavyo jambo linalosababisha maambukizi ya virusi vya Ukimwi, mimba na magonjwa mengine ya zinaa.
No comments:
Post a Comment