Dar na Zanzibar. Wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 ili kuwa sheria kamili, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamemshauri asifanye hivyo, wakisema itapatikana Katiba Mpya isiyo na tija.
Wananchi hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara
ya kushauriana na kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali ili kujua
nini kifanyike, kabla ya kuamua kusaini muswada huo.
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa
iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni
iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari. Katika
tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na
maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa
Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Wapinzani walisema Serikali iliubadili kwa nguvu
muswada huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo
cha wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda
Zanzibar kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Gaudence Mpangala alisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ulikuwa
ukienda vizuri... “Lakini umebadilika vibaya, tena katika kipindi
muhimu. Kupitishwa kwa muswada na kusubiri saini ya Rais kunaweza kuleta
Katiba Mpya, ikawa siyo ile ambayo Watanzania wanaitarajia.” Alishauri
busara itumike kabla ya kusainiwa kuwa sheria kamili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali
Uki alisema hakuna haja ya muswada kukimbiliwa kusainiwa kwani katiba ni
mali ya wananchi na kuupitisha ili uwe sheria bila kuyashirikisha
makundi mengine, kutaendeleza malalamiko na kurudisha nyuma malengo ya
kupatikana kwake. Uki alisema upo wasiwasi kwamba Katiba Mpya itatokana
na utashi wa kisiasa badala ya matakwa ya wananchi, jambo ambalo alisema
linaweza kuathiri malengo ya kuandikwa kwake.
“Utashi wa vyama umeanza kujitokeza, huku chama
kimoja kikiwa na uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo, chama kimoja kina
uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba,” alisema Uki.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5
cha muswada huo kwamba vina kasoro kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la
Katiba kufanya uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa
theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Profesa mwingine wa UDSM, Chris Peter Maina
alisema ikiwa kuna nia njema ya kupata Katiba bora, lazima suala la
uwiano wa idadi ya wabunge katika Bunge la Katiba litazamwe upya.
“Rasimu ya pili ikishatolewa na kukabidhiwa kwa
Bunge la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo itakuwa
imekwisha. Sasa inakuwaje Bunge linajadili Rasimu ya Katiba huku
waliyoiandaa hawapo, hiki kitu kinashangaza,” alisema Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Frank Tilly
alisema hakuna umuhimu wa kukimbiza muswada kutiwa saini wakati kuna
mambo mengi ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi... “Watanzania
hawajakubaliana kwa pamoja, ili jambo liwe zuri ni lazima pande mbili au
zaidi zenye masilahi na kitu husika zikubaliane, sasa hilo
halijafanyika tunakimbilia wapi?” alihoji.
Mhadhiri wa UDSM, Bashiru Ally alisema mchakato mzima wa Katiba
umeshaingia doa kwa kupitishwa muswada unaolalamikiwa na kwamba
manung’uniko ya wananchi hayajajibiwa.
Alisema busara zisipotumika, itapatikana Katiba
isiyokuwa na uhalali wa kisiasa... “Nasema hivi kwa sababu wanasiasa
hawajakubaliana katika kupitisha sheria itakayounda Bunge la Katiba”.
Vyama vya kiraia
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar,
Hassan Nassor Moyo alisema Rais anapaswa kutafakari kwa umakini kabla ya
kusaini muswada huo na kuwa sheria mpya kwa kuwa bado kuna
manung’uniko.
“Hakuna mantiki ya kuupitisha muswada ukawe sheria
wakati kuna manung’uniko. Wakati umefika misimamo ya vyama kuwekwa
kando ili malengo yenye manufaa na tija yaweze kufikiwa kutokana na
mahitaji ya wananchi.”
Moyo alisema ushirikishwaji wa Wazanzibari ulikuwa
finyu kwani waliopata fursa ya kutoa maoni yao walikuwa ni viongozi wa
Serikali pekee.
“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umetokana na
washirika wawili, Zanzibar si mtoto wa kambo, ni mshirika na mdau mkuu
katika kupata Muungano uliopo,” alisema Mzee Moyo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha kupitishwa muswada
wenye kasoro ni wazi kuwa kitazalisha Katiba isiyo na tija kwa taifa.
“Muswada umepitishwa na wabunge wa CCM kwa
asilimia 80, sidhani kama hii ni sawa katika hatua muhimu kama hii na
haitoi picha kamili ya mwelekeo chanya wa kupata katiba stahiki,”
alisema Dk Bisimba.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Gratian Mukoba alisema: “Ukipitisha sheria kinyemela maana yake ni
kwamba unataka ifanye kazi kinyume na matakwa ya watu wengi, jambo
ambalo ni hatari kiuchumi na kielimu.”
Alisema Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara
katika suala hilo, kwa maelezo kuwa, amebakiza muda mfupi kumaliza
kipindi chake cha utawala, hivyo aache Katiba yenye tija kwa Watanzania.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(Tucta), Nicolaus Mgaya alisema: “Ikiwezekana muswada uliopitishwa
usisainiwe na urejeshwe bungeni na kupitiwa upya ikiwa ni pamoja na
pande zote mbili za Muungano kutoa maoni sambamba na kurekebishwa kwa
kasoro zilizopo.”
Alisema watu wataondoka lakini Tanzania itaendelea kuwapo, hivyo
ni jambo la busara kama ikipatikana Katiba itakayokuwa na masilahi kwa
wakati huu na ujao.
Wanasiasa
Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib alisema
muundo wa Bunge la Katiba ndio unaozua malalamiko kutokana na wanasiasa
kupewa nafasi kubwa, jambo ambalo alisema linaweza kutanguliza dhima ya
kisiasa na kuweka kando masilahi ya kitaifa na utaifa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
kitendo cha Zanzibar kutoshirikishwa ni kosa kwani Katiba hiyo ni ya
Jamhuri ya Muungano... “Namshauri Rais asisaini muswada huu kwani
utakuwa ni majanga. Namshauri akutane na watu walioonyesha wasiwasi na
sheria hiyo ili kusikiliza mawazo yao, huenda wakamshauri jambo la
msingi la kufanya na iwapo atasaini bila kufanya hivyo mchakato mzima
hautakuwa wa taifa, bali wa CCM.”
Chanzo- Mwananchi
Chanzo- Mwananchi
No comments:
Post a Comment