Zanzibar. Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Monesmo Magamba amemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana katika Mtaa wa Mlandege jana jioni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,
Haji Hana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba kiongozi huyo
wa dini amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, akiendelea na matibabu
baada ya kujeruhiwa usoni, kifuani na mikononi.
Hana alisema kwamba Padri Magamba (60) alikuwa
akitokea katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine
saa 10.15 jioni na watu waliommwagia walimtega mlangoni kabla ya kufanya
uhalifu huo na kutoweka kwenye vichochoro vya Mitaa ya Mtendeni na
Mchangani.
Alisema polisi wamestushwa na tukio hilo kwa vile
limetanguliwa na matukio matatu ya kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa
dini na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kufanikisha kuwakamata
watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
“Tumeanza kufanya uchunguzi ikiwemo kuchukua
maelezo ya majeruhi, tungependa zaidi kupata msaada wa kitaarifa kwa
watu walioona na wanaojua mahali walipo watu wanaofanya vitendo hivyo,”
alisema Hana.
Mfanyakazi wa Duka la Huduma za Mawasiliano ya
Mtandao, Rukia Yahya Abass alisema anamtambua Padri Magamba kama mteja
wake wa muda mrefu na huja dukani hapo nyakati za asubuhi au jioni kwa
ajili kupata huduma za mawasiliano.
Rukia alisema ameshtushwa kuona padri huyo baada ya kumaliza kupata huduma na kutoka nje akipiga mayowe ya kujeruhiwa.
“Nimezoea kumwita father au babu, ni mteja wangu
kwa kweli, nilimwona akirudi tena ndani huku akiomba msaada, watu
waliokuwa katika mtandao harakahara wakammwagia maji, alikuwa
akilalamika kwa ukali wa maumivu,” alisema Rukia akiwa na huzuni.
Alisema wasamaria wema ndiyo waliomchukua na
kumpeleka hospitali. Kabla ya tukio hilo alilipa gharama za huduma
ambazo zilikuwa ni Sh2,000 na kurudishiwa chenji yake baada ya kutoa
noti ya Sh10,000.
Daktari Jamal Adam ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu
wa Hospitali ya Mnazi Mmoja alisema kwamba Padri Magamba amepatiwa
huduma ya kwanza na anaonekana amejeruhiwa usoni, mikononi na kifuani.
“Ni mapema mno kusema ameathirika kwa kiasi gani kutokana na tukio hilo, tunaendelea na juhudi za kumtibu, ”alisema Dk Jamal.
Huu ni mfululizo wa visa vipatavyo vinne vya
kikatili ambavyo vimefanyika Zanzibar, vikiwalenga watu maalumu katika
kipindi cha miezi 10 iliyopita.
No comments:
Post a Comment