Saturday, March 16, 2013

MAAJABU HAYA MTANZANIA ALIYEISHI NA NYOKA MIAKA 34, BAGAMOYO. STORY KAMILI HII HAPA


Bagamoyo.
 Ni mnyama hatari, mwenye sumu kali, anaogopwa, anaua, anaweza hata kukuachia ulemavu.
Hata hivyo Nobert Joseph Chenga, ameweza kucheza na kuishi na nyoka kwa miaka 34 sasa.
Siku hii, namkuta Chenga, maeneo ya Bagamoyo, akiwa katika moja ya kazi zake za kusaka na kufuga nyoka.
Alikuwa mchovu kwa sababu ya shughuli nzito ya kukamata nyoka kutoka mapori ya Miono, wilayani Bagamoyo.
Nilishuhudia nyoka wa aina mbalimbali wenye sumu wakiletwa katika mifuko maalumu.
Chenga mwenyewe ameshika fimbo maalumu ya kuwasogeza au kukamata nyoka.
Wanapofika, Chenga anafungua mkoba kwa ustadi kisha kuwaweka katika chumba, akitumia fimbo hiyo kuwasogeza mahali panapohitajika kukaa.
Wakati mwingine anawashika, kwa mikono lakini kwa namna ambayo nyoka hao hawawezi kuuma. Anawapanga katika vyumba alivyovipa majina kwa mfano; Black Mamba, Boom Slag. Green Mamba, Cobra, Msanga na African Venom.
Nyoka mmoja mweusi, niliyeambiwa anaitwa Black Mamba, akiwa na urefu wa zaidi ya futi tano, anaponyoka mikononi mwa Chenga, tukio lililonifanya nitimue mbio. Si mimi tu niliyetimua mbio, bali hata wasaidizi wa Chenga waliokuwa eneo hilo walikimbia. Hii ni kutokana na Chenga kuthibitisha kuwa nyoka huyo akikuuma, huchukui dakika tano, kabla ya kubadili jina na kuitwa marehemu.
Ananionyesha alama kadhaa za kuumwa na nyoka, mikononi na miguuni mwake. Lakini bado anaishi nao, anawafuga na anaendelea kuwakamata ili wawe wengi zaidi.
Mapenzi na nyoka yalianza 1979
Chenga alianza kupenda nyoka mwaka 1979. Mapenzi hayo kwa nyoka, hayakuja hivihivi, bali yalimwingia baada ya kupewa zawadi ya chatu mwenye kilo 60, akiwa mkoani Mwanza.
“Nilikwenda kikazi mkoani Mwanza, wakati huo nilikuwa Ofisa Utamaduni wa Sanaa na Lugha,” anasema. Anasema kuwa wakati huo, Ofisa Utamaduni alikuwa ni mtu anayeheshimika, hivyo alipokwenda kikazi katika mkoa mwingine, alipokewa kwa ngoma za utamaduni.
“Nilipokewa na ngoma iliyoitwa Bugobogobo, walikuwa wakicheza na chatu wakubwa sana,” anasema.Baada ya kukabidhiwa zawadi, hakufanya ajizi, aliipokea kwa mikono miwili na kurudi nayo jijini Dar es Salaam.
Alimfungia chatu huyo kwenye sanduku kama alivyoelekezwa, akarejea Dar es Salaam na kumjengea banda maalumu.
“Nilianza ufugaji rasmi baada ya kupewa maelekezo kidogo ya jinsi ya kumtunza na kumlinda chatu,” anasimulia.
Mwaka 1980, Chenga alifanya uamuzi. Aliamua kuanza kumtumia chatu yule kama sehemu ya kiburudisho.
“Nilianzisha kikundi cha sanaa na utamaduni kilichoitwa, ‘Muungano Cultural Troupe.’ Tulikuwa tukimtumia nyoka kufanya sanaa za maonyesho,”anasema.
Katika maonyesho hayo, Chenga alikuwa akicheza na nyoka kwa kumkumbatia, kumweka kinywani na kumzungusha shingoni mwake.
“Tulijifunza namna ya kumshika, kucheza naye na namna ya kumfanya awe rafiki yako. Ni sawa na mnyama kama paka au mbwa anavyokuzoea baada ya kuishi naye muda mrefu,” anasema Chenga.
Anaweka wazi kuwa chatu ni nyoka pekee anayeweza kutumika kwa maonyesho, kwani ana uwezo mkubwa wa kukaba, lakini hana sumu.
“Nyoka wenye sumu, katu hawatumiki katika maonyesho,” anasema Chenga akitahadharisha.
Sanaa hii ya maonyesho ilipoendelea kupata umaarufu, Chenga aliongeza idadi ya nyoka na kufikia kumi huku kila mmoja akiwa na kilo zaidi ya 50.
“Tulipata mialiko mingi, tulienda Sweden mara nyingi, Finland, Denmark na Uingereza,” anakumbuka.
Si kwamba Chenga anafanya kazi hii kwa tamaa ya fedha, la hasha, bali ni mapenzi tu, kwani licha ya kwamba alikuwa Ofisa Utamaduni, aliwahi kuwa mwalimu wa Chuo cha Sanaa na sasa anafundisha somo la Biolojia.
Ufugaji
Chenga anasema, kumfuga nyoka si kazi nyepesi, bali kunahitaji fedha, ujuzi, ulinzi na ukaribu.
“Chatu hula wanyama hai tu, nyoka mmoja aina ya chatu, hula sungura watatu kwa siku,” anasema Chenga Chakula kingine kinachopendelewa na Chatu ni mbuzi hai, kuku au ndama.
Anasema ufugaji wa nyoka wakati mwingine una changamoto kwani wanaweza kutoroka na kusababisha madhara.
Chatu alitoroka na kurudi
“Mwaka jana chatu wangu mwenye kilo 70 alitoroka na sikujua amekwenda wapi. Nilikwenda mwenyewe kituo kimoja cha televisheni nikatoa taarifa. Hata hivyo chatu alirudi mwenyewe baada ya siku nne,” anasema Chenga.
Nyoka hukamatwa kwa dawa za kienyeji
Hamis Kilango, mkazi wa Bagamoyo, anasema kuwa nyoka hukamatwa kutoka katika mashimo yao. Anasema njia moja kuu na ya pekee ya kukamata nyoka ni kutumia dawa za kienyeji.
“ Tunachanjwa…, huwezi kumkamata nyoka hivi hivi bila ya kuwa na dawa, kinyume na hapo unakitafuta kifo,” anasema Kilango.
Anaeleza kuwa kwa kawaida waganga wa kienyeji, hasa wale wa nyoka, huwapa dawa maalumu kwa kuwachanja. “Dawa hiyo ukishachanjwa, nyoka hawezi kukuuma, anakuwa mjinga au tuseme anakuwa zezeta,” anasema.
Anaongeza kuwa dawa hiyo huwapa harufu inayofanana na nyoka, hivyo humfanya nyoka asihofu kwani kwa kawaida huijua harufu ya binadamu.
“Sisi tunayajua mashimo ya nyoka, kwa hiyo tunawafuata walipo tena ili kuwapata vizuri ni nyakati za usiku,” anasema.
Anasema mara kwa mara inatokea wakaumwa na nyoka, lakini wanatumia dawa za mitishamba ambazo yeye huamini hutibu mapema kuliko zile za hospitali.
Kwa kawaida, wanatembea na dawa hizo pindi wanapokwenda kuwinda nyoka, ili zinapotokea ajali wasichelee kujitibia.
Kilango, ana utaalamu wa nyoka, anawafahamu majina, anafahamu ukali wa sumu ya kila nyoka na tabia zao.
Kijana huyu, mfanyabiashara, anayeuza nyoka, ananionyesha nyoka aina ya BoomSlang, nyoka mweusi, mrefu na kusema kuwa, ana sumu kali mno.
Hata hivyo pia alinionyesha nyoka aina ya ‘jumping viper’. Huyu ana uwezo wa kuruka na kumgonga mtu kichwani.
Yuko pia nyoka wa majini, huyu anapenda kuishi ndani ya maji, lakini pia huweza kutoka nchi kavu. Alinionyesha nyoka mwenye umbile dogo pengine kuliko wote, huyu anaitwa African…; Nyoka huyu ni mweusi mno na inaelezwa kuwa mwisho wa ukubwa wake ni urefu wa kidole cha mtu mzima.
Mzee maarufu wa kufuga nyoka, Iddy Kisina anakiri kuwa kukamata nyoka bila dawa ni jambo lisilowezekana. Anasema kuwa kawaida yeye huwakamata nyoka katika mapori kwa kutumia dawa maalumu.
Hata hivyo, Kisina anasema ameacha kufuga nyoka baada ya kushindwa kumudu gharama za ufugaji. “Nyoka wanapenda kula vifaranga vya kuku, panya au kuku, wakati mwingine unakosa vitu hivyo na unakosa cha kuwapa,” anasema.
Hata hivyo anasema kuwa ufugaji wa nyoka ulimsaidia kwani aliweza kujipatia kipato, amejenga nyumba na familia yake inaishi vizuri.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...