Sunday, March 31, 2013

MKAPA: ASEMA TUSITANGULIZE UDINI KWENYE KATIBA


Dar. Ujumbe wa amani na tahadhari ya umakini kwenye utoaji maoni kwenye Katiba ndiyo vilitawala wakati wa misa za Sikukuu ya Pasaka zilizofanyika sehemu mbalimbali nchini jana na juzi.
Miongoni mwa waliotoa hotuba wakati wa sikukuu hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alikuwa mkoani Mtwara; na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyekuwa jijini Dar es Salaam.
Mkapa akataa udini
Rais mstaafu Mkapa alitumia fursa ya kutoa salamu katika Kanisa Katoliki mjini Masasi kuliasa taifa kujiepusha na utoaji wa maoni ya Katiba kwa misingi ya dini.
Mkapa alisema katiba ijayo haipaswi kuwa na itikadi za kidini kwa kuwa zinaweza kuliangamiza taifa.
“Wapo watakaopata uwakilishi kupitia rasimu ya Katiba ya nchi. Namwomba Mwenyezi Mungu awape mwanga, muhakikishe jambo moja tu ambalo litakuwa msingi mkubwa wa amani na maendeleo na umoja wa taifa letu.
Watupatie Katiba ambayo inatoa fursa kamilifu ya kila mtu kuwa na imani yake.
“Katiba inayoheshimu imani ya kikatiba na imani zote zinazofanywa na wananchi wa Kitanzania…Vilevile ihakikishe kwamba dola au nchi yetu haina imani rasmi kama vile nchi yetu isivyo ya kabila moja, hivyo haiwezekani kuwa na Katiba ambayo inatambua kwa dhana au maandalizi ya vipengele mbalimbali kwamba kuna udini, haiwezekani.”
Askofu na Muungano
Watanzania wametakiwa kuwapuuza watu wanaohubiri kuuvunja Muungano kwani watu hao wana agenda binafsi ambazo si kwa faida au masilahi ya nchi, bali wao na baadhi ya mataifa yanawafanya vibaraka wa kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki la Dodoma wakati wa misa ya Pasaka ambayo iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mt. Paulo wa Msalaba mjini humo.
Askofu Nyaisonga alisema hata kama kuna baadhi ya matatizo katika Muungano, yanapaswa kuboreshwa badala ya kuuvunja kabisa Muungano ambao kimantiki umeijengea nchi heshima.
“Muungano ni heshima ya taifa, tusiuvunje, tutumie Katiba Mpya kuboresha pale tunapoona kuna upungufu na tujiepushe na hoja za watu wenye masilahi binafsi ambao wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya mataifa kutaka kutuvuruga kwa kusema Muungano hauna faida, hao wana masilahi binafsi tuwapuuze,” alisema Askofu Nyaisonga.
Pengo ataka mafundisho
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliwaambia waumini wa kanisa hilo, “Tutafute ufumbuzi wa matatizo yetu kwa njia ya imani.”
Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati wa misa ya mkesha wa Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika juzi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.
Ulinzi uliendelea kuimarishwa ndani na nje ya kanisa hilo kwa waumini waliofika kukaguliwa na polisi mlangoni kabla ya kuingia kanisani, kitendo ambacho pia kilifanyika siku ya Alhamisi Kuu.
Pia Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro jana liliimarisha ulinzi katika makanisa mbalimbali mjini Moshi wakati wa ibada ya Pasaka kutokana na vitisho vya kuhujumiwa kwa baadhi ya makanisa.
Katika milango ya makanisa, walionekana askari kanzu, wenye sare na kuruta kutoka Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA-zamani CCP), wakishika doria.
Akataza visasi
Waumini wa dini nchini wametakiwa kutolipiza visasi kwa sababu vinaweza kusababisha chuki, mfarakano na hatimaye machafuko kwa watu wasio na hatia. Hayo yalisemwa na Paroko Msaidizi wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Osterbay jijini Dar es Salaam, Padre Gerald Kamina kwenye misa ya Sikukuu ya Pasaka jana.
Imeandikwa na Abdallah Bakari, Israel Mgussi, Patricia Kimelemeta, Imani Makongoro, Daniel Mjema, Sanjito Msafiri, Godfrey Kahango, Florence Focus na Venance George.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...