Wednesday, March 13, 2013

WATU 51 WAFA KWA POMBE YA KIENYEJI



Karibu watu 51 wamekufa kutokana na kunywa pombe ya kienyeji katika mji mkuu wa Tripoli nchini Libya, maafisa wa wizara ya nchi hiyo wamesema.
Maafisa hao wamesema watu 378 wamepelekwa katika hosptali za Tripoli kuanzia siku ya Jumamosi na idadi ya vifo inazidi kuongezeka.
Maafisa wa hosptali wameiambia BBC kuwa vifo hivyo vimetokea kutokana na sumu aina ya methanol na wagonjwa wengi wamefanyiwa tiba ya kuchuja sumu kwenye figo.
Matumizi na biashara ya pombe ni marufuku nchini Libya lakini inapatikana kwa njia ya siri.
Maafisa wa Wizara ya Afya wamesema watu 38 hadi sasa wamekufa katika hosptali ya mji mkuu wa Tripoli na wengine 13 walifariki wakati walipokuwa wakisafirishwa kwenda nchini Tunisia kwa ajili ya matibabu.
Tayari serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura katika mji mkuu wa Tripoli kutokana na tatizo hilo.
Pombe hiyo iliyoleta madhara ni pombe ya kienyeji inayojulikana kwa jina la Bokha. Inatengezwa kwa matunda.
Lakini sumu ya methanol inayotengezwa kiwandani imekuwa wakati mwingine ikitumika kuongeza ukali wa pombe anaripoti mwandishi wa BBC Rana Jiwad akiwa Tripoli.
Matatizo yanayotokana na kutumia sumu ya methanol ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi, upofu, kukosa nguvu na kifo.
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi hiyo Husein Al Amry ameiambia BBC kuwa kikosi maalum kimezunguka eneo ambalo pombe hiyo ya kienyeji inapodhaniwa kutengenezwa.
Ameongeza kusema kuwa Wizara inajiaandaa kutumia nguvu iwapo wamiliki wa eneo hilo hawatakubaliana na amri ya kutoka ndani ya nyumba.
Pombe ni biashara inayofanywa kwa magendo kutoka Libya kwenda nchi za Tunisia, Algeria na Malta.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...