Saturday, December 8, 2012

CUF; CCM NI KICHAKA CHA WALA RUSHWA,

Chama Cha Mapinduzi (CCM) - Dodoma, Tanzania
MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema CCM ni kichaka cha wala rushwa ambacho kinadhoofisha juhudi za mapambano dhidi ya rushwa na kuwasababishia wananchi ugumu wa maisha. Amesema katika chaguzi za ndani za CCM zilizomalizika Novemba mwaka huu, asilimia 70 ya viongozi wamepatikana kwa njia ya rushwa.

Profesa Lipumba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mdahalo wa wadau wa mapambano dhidi ya rushwa ikiwani sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Duniani.

Katika mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Profesa Lipumba alisema, “Ukifuatilia uchaguzi wa ndani wa CCM uliomalizika hivi karibuni utaona jinsi tatizo hili linavyozidi kuwa gumu.” Alisema hata Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alilalamikia kuchezewa rafu katika chaguzi za CCM kwa sababu ya rushwa.

“Waziri Mkuu Mstaafu, Sumaye alilalamikia rushwa, kwanini hamkumkaribisha ili awape taarifa za aliyoyaona kwenye chaguzi hizo, hamkuhangaika hata kumtafuta,” alisema.

Alisema mtandao huo wa CCM umeshaweka viongozi waliopatikana kwa njia za rushwa tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Viongozi waliopatikana kwa njia za rushwa wakishika dola hawatahangaika katika kupambana na rushwa kwa sababu hawaichukii,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema vita ya rushwa ni ngumu kwa sababu CCM ni chama ambacho kinashika dola kimeonyesha mfano mbaya katika chaguzi zake.
Alisema hata watumishi wa Serikali wanapoona vitendo vya rushwa vinavyofanywa na chama hicho nao hawawezi kuogopa hivyo nao kwa nafasi zao wataendelea kupokea rushwa na kuwasababishia wananchi ugumu wa maisha.

Alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano bora katika mapambano dhidi ya rushwa na kwamba wanatakiwa kuonyesha kwa vitendo namna wanavyoichukia rushwa.

Naye Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento alisema Takukuru kisiwe chombo cha kuwadhalilisha watu na kwamba wengi wamekuwa wakikamatwa lakini kesi zao zimekuwa hazina nguvu.

“Nimekuwa nasikia watu wengi wakikamatwa na Takukuru lakini kesi zao huwa hazina nguvu kwa sababu hawafanyi uchunguzi mapema,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayoub Rioba alisema wala rushwa wenye mali wamekuwa wakionekana mashujaa mbele ya jamii na kwamba waadilifu wamekuwa wakidharaulika.
“Anayepata mali kwa rushwa ndiye anayesifiwa katika jamii zetu hivi sasa na kwamba muadilifu asiye na mali huchekwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...