Monday, December 24, 2012

OFISA WA TAKUKURU ASHAMBULIWA KWA RISASI NA KUPOTEZA MAISHA


Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hoseah 


OFISA uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Bhoke Ryoba, ameuwawa kwa kupigwa rasisi na watu wasiojulikana.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la Kigamboni Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambako ofisa huyo alikuwa anahudhuria sharehe.
Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hoseah, akizungumzia tukio hilo  alithibitisha na kueleza kuwa alifariki dunia juzi usiku.
“Tumekuwa tukipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakihitaji kufahamu ukweli kuhusu tukio la kupigwa risasi kwa mtumishi wa Takukuru, Bhoke Ryoba,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Dk Hoseah iliyotolewa na ofisi ya habari ya Takukuru.
Iliendelea, “Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hoseah, anapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hili kwamba ni kweli mtumishi Bhoke Ryoba amefariki dunia jana usiku, Jumamosi Desemba 22, 2012 baada ya kupigwa risasi. Uchunguzi wa Polisi kuhusu chanzo cha tukio hilo bado unaendelea”.
Baadaye ofisa habari wa Takukuru Doreen Kapwani alifafanua kuwa ofisa huyo mchunguzi alifikwa na umauti wakati anajumuika na marafiki zake katika moja ya tafrija iliyokuwa ikifanyika katika eneo la Kigamboni.
Alisema akiwa katika hafla hiyo, ghalfa walitokea watu wasiojulikana na kumiminia risasi hadi kufa.
“Hawa watu walimvamia Ryoba aliyekuwa kwenye sherehe moja na kumshambulia kwa risasi na kisha wakatokomea kusikojulikana,” alisema na kuongeza:
“Watu hao hawakutambulika kwa kuwa baada ya kutekeleza azma hiyo walitoweka haraka na kutokomea.”
Alipotakiwa kueleza pengine kumekuwepo matukio yoyote katika siku za hivi karibuni yanayoweza kusababisha tukio hilo, Kapwani alijibu “ni mapema mno sasa kudadisi suala hilo.”
Kapwani alisema Ofisi ya Takukuru kwa sasa haiwezi kueleza chochote kwani tukio hilo limeripotiwa polisi kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova alipotakiwa kuelezea hatua  zilizochukuliwa na jeshi hilo baada ya tukio hilo, alisema kuwa hangeweza kuzungumzia chochote kwa vile alikuwa nje ya ofisi.
“Naomba mtafute Kamanda wa Temeke, nafikiri atakuwa kwenye nafasi ya kukupa taarifa zaidi kwa sasa mimi siko ofisini, hivyo nakushauri ufanye hivyo,”alisema Kamanda Kova.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo pia hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwani kila simu yake ya kiganjani haikupatikana kila alipopigiwa.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai (RCO) wa mkoa huo wa Temeke aliyejulikana kwa jina moja la Ame alipoulizwa kuhusu tukio hilo hakukiri wala kukataa, lakini alisisitiza kuwa anayeweza kulizungumzia ni bosi wake, Kiondo.
”Nimefika hapa ofisini hapa kwa bahati mbaya hayupo, halafu nimejaribu kumtafuta kwenye simu zake zote sikuweza kumpata, na kama unavyojua hapa protocol (itifaki) lazima izingatiwe kwahiyo siwezi kukusaidia zaidi ya hapo, pole sana ndugu yangu,”alisema Ame.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...