Thursday, December 6, 2012

MWANDISHI WA HABARI APIGWA RISASI NA POLIS KUNDUCHI DAR ER SALAAM



MWANDISHI wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaban Matutu 

MWANDISHI wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaban Matutu amejeruhiwa kwa risasi juzi usiku baada ya Polisi wenye silaha kuvamia nyumbani kwake, Kunduchi Dar es Salaam wakidai kumsaka kibaka aliyekimbilia ndani ya nyumba hiyo.

Hilo ni tukio la pili ndani ya mwezi mmoja kwa waandishi wa habari kujeruhiwa kwa risasi. Novemba 2, mwaka huu Mhariri wa Gazeti la Business Times, Mnaku Mbani alijeruhiwa kwa risasi mdomoni na kupoteza meno matatu na watu waliosadikiwa kuwa majambazi akiwa njiani kwenda nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam.

Wakati tukio likitokea jana saa 4:00 usiku, kijana aliyekuwa amejeruhiwa kwa bomu na polisi katika vurugu zilizotokea Tegeta wiki iliyopita, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akielezea tukio hilo, Matutu alisema akiwa amelala chumbani na mkewe walisikia sauti ya mtu nje ikimwita mkewe kwa jina la Mama Jumanne. Alimwamsha na kumtaka aende akamsikilize.
Alisema wakati mkewe akielekea mlangoni, alimtaka mtu aliyekuwa akimwita ajitambulishe lakini hakufanya hivyo.
“Wakati mke wangu anajiandaa kwenda kufungua mlango nikasikia sauti za watu wengi wakiongea nje na sauti zilikuwa za wanaume, ikanibidi nimzuie,” alisema Matutu.
Alisema baada ya kumzuia, aliamka na kuchukua panga kwa ajili ya kujihadhari na kwenda kufungua mlango. Lakini kabla ya kuufungua, alishtuka kuona mlango ukisukumwa kwa nguvu hivyo naye kulazimika kuuzuia.

Katika patashika hiyo, anasema alimulikwa kwa tochi yenye mwanga mkali usoni na kisha kusikia kishindo cha bunduki jambo lililomfanya aamini kuwa mkewe ameuawa.
“Sikujua kuwa ni mimi ndiye niliyejeruhiwa nilipomwona mke wangu yupo salama na mimi damu ikiwa inanitoka ndipo nikabaini kuwa aliyejeruhiwa ni mimi,” alisema Matutu.

Alisema baada ya tukio hilo alihoji sababu za shambulio hilo na askari hao wakamwambia kuwa wanamtafuta Mama Juma. Hata hivyo, alipowaonyesha mkewe walisema siye huku wakitaka kumtoa risasi iliyokuwa mwilini mwake.
Aliwakatalia na kuwaomba wampeleke kupata matibabu, wakati huo akiwasiliana na baadhi ya ndugu na jamaa zake kuwapa taarifa ya kilichompata.

Polisi wajitetea
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alidai kuwa kujeruhiwa kwa mwandishi huyo kulitokana na yeye kuanza kumshambulia askari kwa panga.

Alimtaja askari huyo, F.8991 D/C Idrisa na kueleza kuwa alifika na wenzake katika nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwa kuna majambazi sugu waliojificha humo.

“Askari huyo aliyekuwa na wenzake wanne, baada ya kujeruhiwa alirukiwa na huyo aliyemkata panga, katika purukushani hizo risasi moja ilifyatuka kutoka kwenye silaha aina ya bastola aliyokuwa nayo huyo askari na kumjeruhi kwenye bega la kushoto mtu aliyekuwa akipambana naye,” alidai Kenyela.
Mashuhuda
Baadhi ya mashuhuda akiwamo aliyetoa taarifa za kuwapo kwa uhalifu eneo hilo, walisema askari hao walielekezwa chumba cha mwanamke waliyemtaja kwa jina la Mama Jay ambaye ndiye waliyekuwa na wasiwasi juu ya mwenendo wake.

Walisema hata baada ya kuelekezwa, askari hao hawakufuata maelezo hayo na badala yake wakaenda katika chumba cha mwandishi huyo pasipokuwa na kiongozi yeyote wa eneo hilo.
“Tunachojua sisi katika mazingira kama yale wangekwenda kwa mjumbe lakini hawakufanya hivyo na hata chumba walichokwenda siyo kule tulipowaambia,” alisema mmoja wa watu hao aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom Kibanda alisema jana kwamba Matutu alipigwa risasi katika bega la kushoto karibu na moyo.

“Nilikuwa miongoni mwa watu waliompeleka Matutu Muhimbili na ilipofika saa nane usiku walimhamishia Moi  kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi,” alisema Kibanda.
Ofisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almas alithibitisha Matutu kufikishwa katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa jana asubuhi alipelekwa katika chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuondoa risasi hiyo.
“Tayari ameshaanza matibabu, saa 2.30 asubuhi alipelekwa katika chumba cha upasuaji,” alisema Almas.
Almas alisema kuwa baada ya kuondolewa risasi hiyo Matutu alipelekwa katika Wodi ya Sewa Haji kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Aliyejeruhiwa kwa bomu afariki

Majeruhi aliyekuwa amelazwa Muhimbili baada ya kulipukiwa na bomu Novemba 29, mwaka huu katika eneo la Tegeta, Dar es Salaam amefariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Kifo cha kijana huyo John Paul (16), kimetokana na  majeraha hayo ya bomu aliyopata katika vurugu zilizotokea wakati Kampuni ya Udalali ya Mwankinga ilipokuwa ikifanya operesheni ya kukamata magari yaliyoegeshwa pembezoni mwa barabara kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...