MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Tongoni nje kidogo ya jiji la Tanga, (jina tunalihifadhi) amekutwa amekufa ndani ya nyumba ya kulala wageni alikopelekwa kutolewa mimba bila mafanikio.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na
kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe
mwanafunzi huyo alikutwa amekufa juzi katika nyumba ya kulala wageni
iliyopo barabara ya 21 jijini Tanga.
Mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema kwamba mwanafunzi huyo
aliingia saa 4.00 asubuhi siku ya tukio akiwa ameambatana na kijana
mmoja wakakodi chumba.
“Baadaye alikuja mwanaume mmoja wa makamo ambaye
alituuliza kama wameingia mwanafunzi huyo na mwenzake, tulipomwonyesha
chumba walichoingia naye akakodi chumba cha jirani ndipo tukaona wote
wakijifungia kwenye chumba kimoja,” alisema mhudumu.
Mhudumu huyo alisema baada ya muda wa saa moja,
mvulana na mzee huyo wakaaga kwamba wanatoka huku wakisema kwamba
msichana amebaki chumbani akiwa amepumzika. Akithibitisha habari hizi,
Kamanda Massawe alisema taarifa ya tukio hilo ilitolewa na mhudumu wa
nyumba hiyo ya kulala wageni katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni
Jijini Tanga.
“Tatizo ni kwamba nyumba hii ya wageni wahudumu
wake hawakuwapa wageni hao daftari ili waorodheshe majina yao hivyo
inakuwa vigumu kuwafahamu,” alisema Kamanda Massawe na kufafanua kuwa
alifariki akitolewa mimba ya mwezi mmoja.
Kamanda Massawe alisema mpaka sasa hakuna mtu
aliyekamatwa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini
waliohusika na kifo hicho.
No comments:
Post a Comment