Tuesday, December 4, 2012

Yanga yakubali kumnunua Okwi kwa Sh 395 milioni

 


Emmanuel Okwi

SIMBA imeweka mfukoni Dola 40,000 (Sh63 milioni) na inaondoka leo Jumanne kwenda Kampala, Uganda kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja, Emmanuel Okwi, lakini Yanga wamesema wapo tayari kutoa Dola 250,000 (Sh395 milioni) kumsainisha straika huyo.

Okwi alikuwa akishinikiza kupewa Dola 80,000 (Sh126 milioni) aongeze mkataba wa miaka miwili na Simba lakini baadaye Wekundu hao wa Msimbazi wakamlainisha na kuridhia kwamba atasaini mkataba wa mwaka mmoja tu kwa Dola 40,000 (Sh63 milioni) na tayari amepewa gari na nyumba Sinza Mori, jijini Dar es Salaam.

Simba wamepanga kwenda kumalizana na Okwi leo Jumanne pamoja na kukamilisha mazungumzo na kocha wa timu ya taifa ya Malawi, Kinnah Phiri.

Mpaka mwisho mwa wiki hii, Simba watakuwa wameingia mikataba miwili ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba wa mwaka mmoja na Okwi pamoja na kocha Kinnah Phiri, ambaye atachukua mikoba ya Cirkovic Milovan.

Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano ya Yanga, Abdallah Binkleb alisema jana Jumatatu kuwa watatoa hata Dola 250,000 (Sh395 milioni) ili kununua Okwi kutoka Simba.

"Okwi ni mchezaji mzuri, Simba wakikubali kuchukua Dola 200,000 (Sh316 milioni) mpaka 250,000 (Sh395 milioni) sisi tutawapa, hiyo ni halali kwa huyo mchezaji. Lakini nakwambia hawawezi kukubali kutuuzia kwa hiyo bei, wataongeza zaidi, hawako tayari kumuuza," alisema kiongozi huyo.

Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hanspope wamesema Okwi anauzwa Dola 400,000(Sh 631 milioni).

"Ni mchezaji mzuri na mwenye thamani, sisi kwa mchezaji kama Haruna Niyonzima ambaye anatakiwa na El Merreikh ya Sudan hatuwezi kumuuza hata kwa Dola 200,000 (Sh316 milioni) wale jamaa watakuja muda wowote kuanzia sasa, lakini tutakaa tukubaliane, watatakiwa kutoa pesa ambayo sisi hatutaweza kuitoa,mara tatu au hata nne.

"Siwezi kusema thamani ya Haruna kwa sasa lakini ni miongoni mwa wachezaji ghali, tukishakaa na Merreikh tutafanya uamuzi, tukizungumza sasa tutaharibu biashara," alisema kiongozi huyo na kuongeza kwamba mpaka kufikia wikiendi hii watakuwa wameshamalizana na wachezaji wa kupelekwa kwa mkopo na wapya.

Kuhusu kambi alisema: "Tumepata sehemu kama nne kule Uturuki lakini zote ziko nje ya mji mkuu yaani Instanbul, ni miji ambayo iko kwenye ufukwe wa Bahari ya Mediteranian. Tunataka sehemu tulivu sana na ambayo itakuwa na viwanja vizuri na hali ya hewa nzuri."

Yanga itaondoka Desemba 27 kwenda Uturuki kuweka kambi ya wiki mbili na ikiwa huko itacheza mechi mbili au tatu za kirafiki.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...