Friday, December 14, 2012

KAULI YA KAWAMBWA JUU YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU (VYUO VIKUU) NA MSTAKABALI WA WANAFUNZI WA BADAE


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa 


TUMEKUWA tukisisitiza mara kwa mara kwamba muundo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), una walakini mkubwa. Bila kutafuna maneno, tumekuwa tukisema kwamba bodi hiyo haiwezi kufanya kazi zake kwa ufanisi kutokana na kasoro za kisera na kimuundo ambazo zimeifanya bodi hiyo kufanya kazi kama idara ya Serikali.

Kama hiyo haitoshi, wizara husika nayo imekuwa sehemu ya tatizo, kwani nayo pia imeshindwa kuisimamia bodi hiyo ili itekeleze sheria zilizopitishwa na Bunge kuhusu mikopo ya wanafunzi. Ni jambo la kufadhaisha kuona viongozi wa wizara husika wakiungana na HELSB kulalamika badala ya kubuni mbinu za kutatua matatizo yanayowasibu wanafunzi wa elimu ya juu katika kupata mikopo.

Katika kuendeleza utamaduni huo wa kulalamika, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema juzi kuwa, wizara yake inatatizwa na suala la wanafunzi waliokopa fedha kupitia HELSB kutorejesha fedha hizo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kufaidika na mikopo hiyo.

Alisema hadi Septemba mwaka huu, fedha zilizokusanywa ni Sh23.3 bilioni kutoka kwa wanafunzi 48,235 tu na kwamba kiwango hicho ni chini ya asilimia 50 ya fedha zilizotakiwa kurudishwa. Katika kuonyesha jinsi wizara yake ilivyokata tamaa kuhusu uwezekano wa mikopo hiyo kurejeshwa, alisema wanafunzi hao wasiporejesha mikopo hiyo watafuatiliwa na wakala maalumu aliyeajiriwa na HELSB kwa lengo la kuwafuatilia ambao hawajarejesha mikopo hiyo.

Kama tulivyosema hapo juu, kauli hiyo inaonyesha bayana kwamba ni ya mtu aliyekata tamaa. Huku akikiri kwamba tatizo hilo limekuwa changamoto kubwa kwa wizara yake, alisema wanafunzi hao waliorejesha mikopo ndiyo wamegundulika na kwamba idadi kubwa zaidi bado haijagundulika na haijulikani wako wapi na wanafanya kazi gani.

Pamoja na kusema HELSB imeajiri wakala maalumu wa kufuatilia ambao hawajarejesha mikopo, Waziri Kawambwa alisema ameiambia bodi hiyo kwamba hatakuwa na uhusiano mzuri na bodi hiyo kabla haijafanya kazi ya kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa, hivyo kuitaka bodi hiyo kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.

Tafsiri ya moja kwa moja ya kauli hiyo ya Waziri ni kwamba kuna uzembe mkubwa katika bodi hiyo ingawa inao uwezo wa kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa. Jambo la kushangaza ni kuona anapata kigugumizi kuifukuza bodi hiyo na kuteua mpya itakayokuwa na dhamira na uwezo wa kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa, tena katika kipindi kifupi. Tatizo hapa ni utamaduni wa kuleana na kulindana na hakuna mwenye uchungu wa kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetokana na kodi za wananchi zinarejeshwa.

Tunapata wakati mgumu kuelewa jinsi watu wanavyoweza kuchukua mikopo halafu wakaingia mitini, licha ya kusaini mikataba iliyotayarishwa na wanasheria wasomi na kuwapo sheria ya Bunge inayosimamia mikopo hiyo. Hatutaki kuamini kwamba mikataba hiyo ilitayarishwa na kusainiwa kienyeji, kwa maana ya kutobainisha anuani za makazi na wakopaji kutokuwa na wadhamini ambao mali zao (collateral) zinakamatwa na kunadiwa pindi wadhaminiwa wanapotoweka kusikojulikana kama Waziri Kawambwa anavyodai.
Matatizo yote hayo yasingetokea kama Bodi ingekuwa na watu wabunifu na waadilifu. Tunaambiwa baadhi ya wafanyakazi wake wamepelekwa mahakamani kwa madai ya kuchota mamilioni ya fedha za mikopo. Ushauri wetu kwa Waziri Kawambwa ni kuisafisha bodi hiyo na kuteua mpya itakayoleta ufanisi. Vinginevyo fedha hizo za wananchi zitakuwa zimekwenda kwa mganga, hazitarejeshwa ng’o.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...