JUMLA ya wanafunzi 6,838 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, mkoani Arusha, wamekosa nafasi ya kujiunga na masomo ya Sekondari kutokana na uhaba wa nyumba vya madarasa 172 .
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Evelyine Itanisa 
alitoa taarifa hiyo, juzi katika kikao cha kamati ya uchaguzi wa 
wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 mkoani Arusha.
Itanisa alisema wanafunzi hao, wanatoka  katika 
halmashauri sita za mkoa Arusha na ni halmashauri moja tu ya Karatu 
ambayo imeweza kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu.
Alisema  katika jiji la Arusha  wanafunzi 2420 
wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba  vya madarasa 61, Ngorongoro
 wanafunzi 441 wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba 11.
Alisema   Halmashauri ya Arusha vijijini  wanafunzi 1880 wameshindwa kujiunga na sekondari kutokana na  uhaba wa vyumba 47.
“Pia Halmashauri ya Longido kuna wanafunzi 140 
ambao wanahitaji madarasa manne, Meru wanafunzi 1,159 wakiwa na mahitaji
 ya vyumba 29, wilaya ya Monduli wanafunzi 807 wamekosa nafasi kutokana 
na kukosekana madarasa 20”alisema Itanisa.
Alisema kutokana na hali hiyo, ameziagiza 
halmashauri hizo sita za mkoa wa Arusha kuiga mfano wa halmashauri ya 
Karatu, kwa kuhakikisha zinajenga vyumba vya madarasa vya kutosha  ili 
kuhakikisha wanafuzi wote waliofaulu wanapata nafasi.
“Ili kuhakikisha watoto waliofaulu wote 
wanaendelea na sekondari, kila halmashauri inapaswa ihakikishe 
inakamilisha ujenzi wa madarasa kabla ya februari  mwakani “alisema 
Itanisa.
Hata hivyo, Katibu Tawala huyo alisema kiwango cha
 ufaulu kwa Mkoa wa Arusha, kimekuwa kikipanda kwa miaka mitatu sasa 
mfululizo ambapo mwaka huu jumla ya wanafunzi 26,464 wamefaulu mitihani 
kati ya wanafunzi 37,493 waliofanya mitihani.
“Matokeo haya yanafanya Mkoa wa Arusha uwe 
umefaulisha kwa asilimia 70.6 na waliofaulu ni wavulana 12,608 na 
wasichana 13,856”alisema Itanisa.
 
 
No comments:
Post a Comment