Monday, December 17, 2012

Lowassa: Ukosefu wa ajira ni tishio kwa usalama wa nchi

 
 Edward Lowassa

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ameonya juu ya tatizo la ajira kwa vijana linavyoweza kuhatarisha usalama nchini.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ukarabati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Akyeri Kati Dayosisi ya Meru mkoani Arusha, Lowassa alisema kuwa dunia hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya tatizo la ajira, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na changamoto hiyo.
“Tusipolishughulikia tatizo hili, hali itakuwa mbaya, hapatakalika. Tumeona katika nchi za Ulaya huko jinsi watu wanavyoandamana kudai ajira na maisha bora, tusiache tukafika huko,” alionya Lowassa ambaye amekuwa mzungumzaji mkubwa wa tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Alirejelea wito wake wa kuyataka makanisa na mashirika mengine kusaidia kutatua tatizo hilo.
“Huko nyuma niliwahi kusema makanisa, mashirika na watu binafsi wasaidie juhudi za Serikali katika kukabiliana na tatizo hili,” alisema na kuongeza kuwa eneo la Meru linakabiliwa kwa kiasi kikubwa na tatizo hili kama yalivyo maeneo ya mijini.
Kutokana na hali hiyo, ametaka uongozi wa Halmashauri ya Meru kuharakisha zoezi la kuwapatia ardhi wakazi wa eneo hilo, katika Wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga.
“Naomba viongozi mlichangamkia zoezi hilo, msiogope, hii Tanzania ni ya Watanzania, mtu unaishi popote na haya yanawezekana kwa sababu ya uongozi imara na umoja wa Chama cha Mapinduzi,” alisema Lowassa.
Alisema kuwa katika nchi nyingine suala hilo la watu wa eneo fulani kwenda kuishi kwa shughuli ya kilimo au ufugaji kwenye eneo jingine haliwezekani.
Kutokana na uhaba wa ardhi yalitolewa mapandekezo ya kuwahamishia baadhi ya wakazi wa Meru kwenye Wilaya za Handeni na Kilindi kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Hata hivyo utekelezaji wa mapendekezo  hayo umekuwa ukisuasua kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Meru, Paul Akyoo alimsifu Lowassa kwa kusema kuwa ni kiongozi mchapakazi na mtu wa ibada.
“Wakati ukiwa Waziri Mkuu ukimsaidia Rais kazi, sisi tuliona na kushuhudia jinsi ulivyokuwa na maono ya mbali katika kutatua kero na shida za Watanzania,” alisema Askofu Akyoo na kuongeza kuwa wanamshukuru Mungu kwa ajili ya Lowassa.
Wewe ni mzee wa kujituma na kufuatilia kwa karibu sana uamuzi unaotolewa. Pia tumeshuhudia jinsi unavyosaidia dini na madhehebu mbalimbali nchini,” alimpongeza.
amilia yake na marafiki zake walitoa Sh33.2 milioni.
Malengo ya harambee hiyo yalikuwa ni kukusanya Sh160 milioni.
Lowassa alisema kuwa hana hela ya Harambee isipokuwa nguvu yake ni marafiki wanaomchangia.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...