MAHAKAMA ya Rufani imemrejesha bungeni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ikiwa ni miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya
kushinda rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Arusha iliyotolewa
Aprili 5, mwaka huu.
Hukumu hiyo iliyosomwa jana na Naibu Msajili wa
Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu imemtambua Lema kuwa mbunge halali
wa Arusha Mjini na kuwaamuru wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard
Luanda kwa niaba ya wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo,
Mahakama ya Rufani ilisema kuwa wajibu rufani hawakuwa na haki ya
kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi
yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na
amri ya Mahakama Kuu. Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha
Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo.
Uamuzi huo uliwafanya wanachama na wafuasi wa
Chadema waliokuwa wamefurika ndani ya ukumbi wa Mahakama hiyo, kulipuka
kwa furaha huku wakiimba kibwagizo cha “People’s Power!” na wengine
wakiongeza kwa kuimba “Lema! Lema! Lema!”
Wanachama na wafuasi hao wa Chadema walianza
kusukumana kwenda kumkumbatia Lema, huku wengine wakipanda kwenye viti
(mabenchi) ya mahakamani.
Tukio hilo lilisababisha taharuki kutokana na
kusukumana, huku wengine wakianguka kwenye mabenchi, hali ambayo pia
iliwapa wakati mgumu viongozi wa Chadema akiwamo, Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe kutoka nje ya ukumbi huo.
Hoja mpya
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliibua na kutolea uamuzi hoja mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote mahakamani hapo.
Hoja mpya
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliibua na kutolea uamuzi hoja mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote mahakamani hapo.
Hoja hiyo ambayo iliibuka kwa mara ya kwanza
kabisa siku ya kusikiliza rufaa hiyo ni kama warufani walikuwa ni wapiga
kura waliojiandikisha.
Katika uamuzi wake kuhusu hoja hiyo, Mahakama
ilisema kuwa wajibu rufaa hao, hawakuwa wapiga kura kwa kuwa katika
kumbukumbu za Mahakama hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ni wapiga kura
waliosajiliwa.
Mahakama ilipoibua hoja hiyo, Wakili wa warufani,
Mughway alijibu kuwa wajibu rufaa hao ni wapiga kura halali
waliosajiliwa na kwamba hata Mahakama ilijiridhisha kwa kuangalia kadi
zao za kupigia kura.
Wakili Mughaway alidai kuwa suala hilo
lilijitokeza Mahakama Kuu na wajibu rufaa hao wakawasilisha kadi zao
mahakamani ambazo ilinakili majina na namba zao na kisha kuzirejesha kwa
wenyewe.
Lakini Wakili wa Lema alidai kuwa hata kama kadi hizo
ziliwasilishwa mahakamani, utaratibu ambao ulitumika haukuwa wa
kisheria, akidai kwamba zilipaswa ziwasilishwe kama vielelezo vya
ushahidi na si jaji kuziangalia na kisha kuzirejesha kwa wahusika.
Katika hukumu yake jana, Mahakama ya Rufani
ilikubaliana na hoja za mawakili wa warufani, ikisema kumbukumbu za
Mahakama hazionyeshi mahali ambako kadi hizo zimepokewa mahakamani kama
vielelezo vya ushahidi.
Mahakama ilisema kwamba kinachoonekana katika
kumbukumbu za Mahakama ni kiambatisho na maelezo tu kuwa wajibu rufani
ni wapiga kura waliosajiliwa na kwamba badala yake wakili wao ndiye
aliyejaribu kuthibitisha hilo kwa maelezo, badala ya vielelezo.
“Katika kesi hii, Wakili Alute (Mghway)
aliwasilisha kadi za wajibu rufaa kwa Jaji (Aloyce Mujuluzi)
kuthibitisha kuwa wajibu rufaa walikuwa wapiga kura halali,” ilisema
Mahakama katika hukumu yake hiyo.
Mahakama hiyo ilisema utaratibu huo ni kinyume cha
sheria kwa kuwa ushahidi kama huo ulipaswa uwasilishwe moja kwa moja
mahakamani na utolewe na mmiliki wa nyaraka hizo.
Pia Mahakama hiyo ilisema kumbukumbu hizo
hazionyeshi kama mrufani alipewa fursa ya kuzungumza lolote kuhusiana na
utaratibu huo wa kuwasilisha hati hizo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilisema kuwa hata kama
ingethibitika kuwa wajibu rufani walikuwa wapiga kura waliosajiliwa,
bado hawakuwa na haki kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi
kwa madai ya mrufani kutumia lugha za matusi kwenye kampeni zake.
Ilisema kwa kuwa kisheria hayo ni maslahi ya umma
kufikishwa mahakamani chini ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba, kanuni ya haki
ya kisheria kufungua kesi ni kwamba mlalamikaji anapaswa kuonyesha haki
zake au maslahi ambayo yameingiliwa na athari alizozipata.
“Hivyo mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua
kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambako haki zake hazikukiukwa,”
ilisema Mahakama ya Rufani.
Ilisema kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya
Tanzania, raia anakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kwa maslahi ya
jamii, kama ilivyotokea katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila
dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 1995.
Mahakama ilisema kuwa shauri hilo halikufunguliwa
chini ya Ibara ya 26 (2) ambayo inampa fursa na haki raia yeyote
kufungua shauri mahakamani lenye maslahi ya umma, huku ikisisitiza kuwa
madai ya wajibu rufani katika kesi hiyo hayagusi maslahi ya jamii yote.
Katika hoja hiyo, Wakili wa wajibu rufani, Mughway
alitumia kesi ya William Bakari na mwenzake dhidi ya Chediel Mgonja na
AG, namba 84 ya mwaka 1980.
Katika kesi hiyo Mahakama Kuu iliamua kuwa inapothibitika kuwa
mpiga kura amejiandikisha ana haki ya kufungua kesi kupinga matokeo.
Mahakama ya Rufaa ilisema kwa uamuzi huo wa
Mahakama Kuu katika kesi hiyo ina maana kuwa mpiga kura ana haki zisizo
na mpaka kufungua kesi hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna
yoyote.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa
Mahakama Kuu katika kesi hiyo iliamua kwa makosa na kwamba haidhani kuwa
sheria haikukusudia kusema kuwa mtu yeyote bila kujali mahali
alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo
lolote nchini.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilisisitiza
kuwa katika kesi kama hiyo ilikuwa ni wajibu wa yule tu ambaye anaona
haki zake zilikiukwa.
Kutokana na kuamua hoja ya kwamba mpiga kura hana
haki ya kufungua kesi, mahakama haikushughulika na hoja nyingine
zilizowasilishwa na warufani, wala rufaa iliyofunguliwa na wajibu rufaa.
No comments:
Post a Comment