Monday, December 17, 2012

KASHIFA/TUHUMA JUU YA KUMILIKI KAMPUNI YA KITALII,NAIBU WAZIRI NYARANDU AFUNGUKA NA KUJITETEA


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu 


NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani) anadaiwa kumiliki kampuni inayojishughulisha na masuala ya utalii kitendo ambacho kinamwingiza kwenye mgongano wa kimasilahi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyalandu anamiliki Kampuni ya Nitoke Safaris Ltd jambo ambalo limeelezwa kuwa ni kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma hasa kwa kuwa yeye ni msimamizi wa sekta hiyo.
Taarifa kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni na Leseni (Brela), zinaonyesha kuwa wamiliki wa Kampuni hiyo ni L.S.Nyalandu na Faraja G. Nyalandu, huku kila mmoja akimiliki asilimia 30 ya hisa.
Kampuni hiyo ilisajiliwa Aprili 24, 2009 na kupewa nambari 70735, wakati huo Nyalandu akiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, wadhifa alioupata kuanzia mwaka 2000.
Ofisi za kampuni hiyo ziko PPF Complex Suit, namba 24 Barabara ya Mzingo, Arusha na magari ya kampuni hiyo yamekuwa yakibeba watalii mkoani Arusha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana akiwa Mwanza, Waziri Nyalandu alikiri kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo lakini akasema tayari alishajitoa.
Katika kujenga hoja ya utetezi wake, Nyalandu alisema kama ambavyo haipendezi yeye kumiliki kampuni ya utalii akiwa waziri wa wizara hiyo, haitapendeza pia waziri wa habari kumiliki gazeti.
“Huwezi kuwa Waziri wa Utalii na ukafanya biashara ya utalii huko katika kampuni hiyo mie nilishatoka kitambo,” alisema bila kufafanua zaidi.
Hata hivyo, kumbukumbu za Brela zinaonyesha kuwa waziri huyo bado ni mmoja wa wanahisa ingawa haijafahamika kama ni tatizo la Brela kutorekebisha kumbukumbu za jalada lake baada ya kujitoa au la.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alipoulizwa na gazeti hili jana alionyesha kushtushwa na taarifa hizo na kusema hajui kama Naibu wake anamiliki kampuni ya utalii.
“Siwezi ku comment (kutoa maoni), chochote juu ya jambo hilo kwa sababu sijui kama ana kampuni ya utalii na pili, ndiyo kwanza nasikia hizo taarifa kutoka kwako (mwandishi),” alisema Kagasheki.
Taarifa zilizowakariri baadhi ya mawakala wa utalii mikoa ya Kilimanjaro na Arusha zilidai kuwa Nyalandu ni mmoja wa washindani katika biashara hasa ya kwenda mbuga za wanyama
Haijafahamika kama Nyalandu aliwahi kutangaza kuwa na masilahi na kampuni hiyo au kama aliwahi kuiorodhesha kama moja ya mali anazomiliki kama Sheria ya Maadili ya Viongozi inavyotaka.
“Siyo tatizo kiongozi kumiliki kampuni, lakini unatakiwa ku-declare interest (kutangaza masilahi) lakini kwa Nyalandu ni tofauti kidogo kwa sababu sasa yuko kwenye sekta hiyo,” alidokeza wakili mmoja.
Wakili huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema hata kama Nyalandu atakuwa haipi upendeleo kampuni hiyo, lakini kwa akili ya kawaida, ni rahisi binadamu kuhisi kampuni hiyo itakuwa ikipewa upendeleo wa aina fulani.
Hata hivyo, Wakili mwingine, Albert Msando wa Arusha, alisema kwa dhana nzima ya utawala bora, Waziri wa Maliasili na Utalii au Naibu wake au watendaji wa Tanapa hawapaswi kumiliki kampuni ya utalii.
“Kwa waziri ku-declare interest (kutangaza masilahi), haitoshi kwa sababu kwanza ndiyo itachochea zaidi watu kufanya biashara na kampuni yako hata kama hauko kwenye utendaji wa kila siku,” alisema.
Wakili Msando alisema mara baada ya Rais Kikwete kumteua kuwa Naibu Waziri wa Utalii na Maliasili, Nyalandu alitakiwa aachie hisa zake zote na kubaki na uwaziri au abaki na kampuni.
“Waziri anaingia vikao vyote vya kusimamia sekta ya utalii…unaenda nje kwenye maonyesho kwa nini watu wasiamini unapokwenda huko unatangaza pia kampuni yako kwa fedha za Serikali?” alihoji.
Septemba 11, 2009, Rais Jakaya Kikwete alinukuliwa akisema mchakato wa kutungwa kwa sheria mpya ya kutenganisha biashara na siasa upo katika hatua za mwisho na ungewasilishwa bungeni.
Rais Kikwete alikuwa akizindua Baraza la Usimamizi la Taifa (NGC) la Mpango wa Kutathmini Utawala Bora barani Afrika (APRM), katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Alisema madhumuni ya kutenganisha biashara na siasa kwa watumishi wa umma itawapa fursa viongozi kuwatumikia wananchi kwa karibu zaidi katika kufanikisha dhana ya utawala bora.
Hata hivyo, Serikali haijapeleka muswada huo bungeni ambao ungewazuia viongozi wa kisiasa wakiwamo madiwani, makatibu wakuu wizarani, wabunge na mawaziri kujihusisha na biashara.
Tuhuma dhidi ya Waziri Nyalandu zimekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti taarifa kuwa aliingilia utendaji kazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kwa masilahi binafsi.
Nyalandu anadaiwa kuiandikia barua Menejimenti ya Tanapa akiiagiza ikutane na Kampuni ya Ahsante Tours ambayo ilikopeshwa kinyemela na Tanapa  hadi deni kufikia Dola 80,000 za Marekani.
Utaratibu unataka kampuni ya utalii inayotaka kupandisha mgeni mlimani kulipia kwa kadi benki.
Mgogoro huo umeibuka baada ya Tanapa kuifungia kampuni hiyo kwa udanganyifu, lakini Waziri Nyalandu akaingilia kati na kuiamuru Tanapa kukutana na Ahsante Tours na kumaliza mgogoro huo.
Jumatatu iliyopita, Nyalandu aliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam akidai kuwa uamuzi wa Tanapa wa kuifungia Ahsante Tours ulikuwa wa dhuluma na kuituhumu Tanapa kwa rushwa.
Agizo hilo la Nyalandu limeibua mtafaruku mkubwa huku kampuni nyingi za utalii zikihoji ilikuwaje Tanapa iiruhusu kampuni hiyo kupitisha wageni bila kulipa ada stahili kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...