Monday, December 17, 2012

MAMBO YAMEKUWA MAMBO CHADEMA; SASA WAANZA KUTIMUANA


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa 


KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Wilaya ya Karatu, imependekeza kufukuzwa uanachama kwa Diwani wa Kata ya Karatu Mjini, Jubilate Mnyenye, ili kukinusuru chama hicho.

Pendekezo hilo linakuja wakati Kamati Kuu ya Chadema, leo inatarajia kutangaza uamuzi, kuhusu mgogoro wa viongozi wa chama hicho wilayani humo.
Mnyenye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mradi wa Kusambaza Maji wilayani Karatu (Kaviwasu), alitiwa hatiani na kamati hiyo, akidaiwa kukisaliti chama.

Pia kuhujumu mradi huo, ambao ndiyo nguzo ya chama hicho wilayani Karatu. Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe ,alikiri Kamati ya Utendaji ya chama hicho, kupendekeza kwa Kamati Kuu, imvue uanachama Mnyenye kwa kukisaliti chama.

Alisema Manyenye ametiwa hatiani kutokana na mikwaruzo kati yake na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Maasai na viongozi wengine. Pia kusaliti msimamo wa madiwani wa Chadema katika vikao vya baraza la madiwani.

“Mwenzetu huyu pia, amekuwa akishiriki katika vikao mbalimbali vya vijana wa CCM katika mji wa Karatu, jambo ambalo tunaamini ni makosa,” alisema Darabe.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alipotakiwa kuelezea uamuzi ya Kamati Kuu, alisema, “Mzungumzaji ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, John Mnyika.
“Naomba uwasiliane na Mnyika ndiye tuliyempa jukumu la kuzungumza na vyombo vya habari,” alisema Dk Slaa.

Hata hivyo, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubunge, alipotakiwa kueleza uamuzi wa kikao hicho, alisema: “Yote yanayohusu kikao yatatangazwa kesho [leo],” alisema.
Wakati Chadema wakisigana, Chama Cha Mapinduzi, (CCM), kinatumia nafasi hiyo ya mgogoro kujitengenezea mazingira ya kulirejesha jimbo hilo mikononi mwake.

Kuonyesha kuwa kinalitaka kwa dhati jimbo hilo, CCM wilayani Karatu imezindua kampeni za kurejesha jimbo hilo na Halmashauri ya Karatu, vinavyoshikiliwa na Chadema. Tayari chama hicho tawala kimeanza mkakati wake wa kushughulikia tatizo la uhaba wa maji, ambalo sasa limewaingiza katika mgogoro mkubwa viongozi wa Chadema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Wilaya ya Karatu, Daniel Awakie, alizindua kampeni ya kulirejesha jimbo na halmashauri wakati wa mkutano wa kwanza wa CCM tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wanachama wa chama hicho, ulifanyika kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...