MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, Mathayo Mwangomo, amewataka wananchi wilayani humo kutokukubali maneno ya uchochezi yanayodhoofisha maendeleo na juhudi za Serikali katika kutatua matatizo ya wananchi wake.
Mwangomo alitoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ruiwa wilayani humo.
Alisema kuwa, hivi sasa Chama cha Mapinduzi
ambacho kipo madarakani kinatekeleza sera zake hivyo wananchi hawana
sababu za kuendelea kusikiliza maneno ya kubeza maendeleo yanayofanywa
na chama hicho.
“Wananchi mnatakiwa kutokubali maneno ya uchochezi
yanayotolewa na wanachache ambayo msingi wake ni kudhoofisha maendeleo
na juhudi za Serikali katika kutatua matatizo yenu,”alisema Mwangomo.
Alisema kuwa, CCM imefanya mambo mazuri katika
jamii ikiwa ni pamoja na kujenga shule za msingi na sekondari za kata,
ambazo zimeongeza kiwango cha elimu nchini.
Mbali na kuwaleeza hivyo wananchi hao, Mwenyekiti
huyo pia alipokea kero za wananchi wa kata hiyo ya Ruiwa ikiwa ni pamoja
na ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh60 milioni zilizochangwa na wananchi
hao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Gwili ambazo zinadaiwa
kutafunwa na diwani wa kata hiyo, Alex Mdimilage, anayedaiwa kumtorosha
mhasibu wa shule hiyo na kutoroka na fedha za wananchi zaidi ya
Sh27milioni na kuiacha shule hiyo ikiwa haina chochote.
Sambamba na hilo wananchi hao pia walilalamikia
vitendo vya diwani wao kuwa, amekuwa kikwazo cha maendeleo ya kata hiyo
kutokana na uwajibikaji wake mbovu uliopelekea wananchi wengi kukihama
chama hicho.
Akijibu tuhuma hizo mbele ya Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi wa wilaya, Diwani wa kata ya Ruiwa , Alex Mdimilage
alikanusha tuhuma hizo na kudai kuwa mambo yote yanayozungumzwa dhidi
yake ni chuki za kisiasa na kwamba kwa kipindi chake hiki amesimamia
miradi mbalimbali kijijini hapo na kata kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM huyo alikiri kuwepo kwa viongozi
wazembe wilayani humo, hivyo amewataka viongozi wanaohusika na tuhuma
hizo kujiengua mapema na hawatasubiri Takukuru na Polisi na kero zote
zilizowasilishwa na wananchi atazifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment