ASILIMIA 20 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini ni bandia, hivyo
kuhatarisha maisha ya wananchi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Dk Kigoda alisema kama hali hiyo itaachwa iendelee itasababisha
madhara makubwa kwa wananchi na taifa kwa jumla.
Alisema kuenea kwa soko la bidhaa bandia nchini kunatokana na bei za bidhaa hizo kuwa ndogo, hivyo kuwavutia wateja wengi.
“Watanzania wenye kipato cha chini ndiyo wapenzi
zaidi wa bidhaa hizi lakini wanatakiwa kutambua kuwa madhara yake ni
makubwa mno,” alisema Dk Kigoda na kueleza kuwa Serikali imetangaza vita
na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hizo.
Dk Kigoda aliwataka wafanyabiashara wanaouza
bidhaa hizo kuziondoa sokoni haraka kabla Serikali haijaanza kuziondoa
kwa nguvu. Waziri Kigoda alisema uchunguzi umebaini kuwa, kati ya Dar es
Salaam na Bagamoyo mkoani Pwani, kuna bandari bubu 32, ambazo hutumika
kupakua bidhaa hizo bandia.
Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni matairi ya magari na
pikipiki, mafuta ya kupaka, maziwa ya watoto, nyaya za umeme, simu za
mkononi na vyakula mbalimbali.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wizara
yake inashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuchunguza
bidhaa zinazoingia nchini kabla hazijasambazwa katika soko.
Alipoulizwa ni lini operesheni ya kuwakamata
wanaouza bidhaa hizo itaanza, Dk Kigoda alimtupia swali hilo Katibu Mkuu
wa Wizara yake, Joyce Mapunjo ambaye alisema huenda ikaanza leo, huku
akisema wizara inachokifanya kwanza ni kutoa tahadhari. Dk Kigoda
akaongeza... “Tukianza (operesheni maalumu) hatutakuwa na mjadala.”
“Zipo nyaya bandia za umeme ambazo kwa kiasi
fulani zinaweza kuwa chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya nyumba
kuteketea kwa moto nchini, pia yapo matairi ya magari na pikipiki ambayo
nayo kwa kiasi fulani yanachangia kuongezeka kwa ajali.”
Akitolea mfano Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Kigoda
alisema kuanzia Januari mpaka Novemba mwaka huu, kulikuwa na ajali za
pikipiki 1997, zilizosababisha vifo vya watu 140.
“Tumejipanga kuhakikisha jambo hili tunalimaliza
kabisa, kwanza tumegundua bandari bubu 32 ambazo pamoja na mambo
mengine, zinaifanya Serikali kukosa mapato na kuhatarisha usalama wa
wananchi” alisema Dk Kigoda.
Alisema kuwa tayari wameshazieleza taasisi zilizo
chini ya wizara hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kutumia
bidhaa bandia yakiwamo ya hasara kutokana na kuharibika katika kipindi
kifupi.
“Wafanyabishara wanaonunua bidhaa kutoka China wanatakiwa kuwa
makini kwa sababu bidhaa zao wanaziuza kulingana na ubora wake, zipo
zenye ubora wa juu hadi wa chini,” alisema Dk Kigoda na kuongeza: “Sasa
wapo Watanzania wanaonunua za ubora wa chini na kuja kuuza nchini kwa
sababu wanataka kupata faida zaidi.”
Alisema katika kuhakikisha kuwa ajali za
barabarani zinapungua, Serikali imetoa pendekezo kwamba kila anayeuza
pikipiki ni lazima auze na kofia ngumu (helmet) mbili.
“Hili ni pendekezo ambalo ni kama limeshapita kwa
sababu kwa hali ya kawaida kuvaa helmeti ndiyo tahadhari kwa wanaotumia
pikipiki,” alisema Dk Kigoda. Dk Kigoda alisema wizara hiyo imekuwa
ikipokea barua mbalimbali kutoka kwa wananchi, zinazowataja vinara wa
kuuza bidhaa hizo, pamoja na maduka au maeneo ambayo bidhaa bandia,
huuzwa kwa wingi.... “Hivyo tunawajua wanaofanya hivyo, tunawataka
kuziondoa haraka.”
No comments:
Post a Comment