Raymond Kaminyoge na Bakari Kiango
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe amewasimamisha kazi vigogo 16 wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) kwa tuhuma za ufisadi.
Idadi hiyo inafanya waliosimamishwa kazi katika bandari hiyo hadi sasa kufikia 23.
Akizungumza
na wafanyakazi wa TPA Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe alisema vigogo
hao wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali.
“ Bodi
imewasimamisha kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za wizi na migongano
ya kimaslahi, hawa wamesimamishwa baada ya bodi kuichambua ripoti ya
uchunguzi iliyotolewa na tume niliyoiunda,” alisema.
Waliosimamishwa
kazi na nyadhifa zao kwenye mabano ni Bakari Kilo (Mkurugenzi
Uhandisi), Raymond Swai (Meneja Uhandisi), Frolence Nkya (Mkurugenzi wa
Mipango) na Mahebe Machibya (Meneja Ununuzi na Ugavi).
Wengine ni
Teophil Kimaro (Meneja Ununuzi), Mary Mhayaya (Afisa Uhandisi Mkuu),
Ayoub Kamti (Mkurugenzi wa Tehama), Mathew Antony (Meneja Kitengo cha
Kontena) Maimuna Mrisho (Mkurugenzi wa Mifumo wa Menejimenti).
Wengine
ni Fortunatus Sandalia (Askari kitengo cha Ulinzi), Fadhili Ngolongo
(Kitengo cha Marine), Mathew Antony (Meneja Kontena), Mohamed Abdullah
(Kitengo cha Mafuta), Kilimba (Idara ya ulinzi) na Owen Rwebu.
Mwakyembe
alisema katika ripoti ya uchunguzi imegundulika kwamba baadhi ya vigogo
wa Bandari wanamiliki kampuni ambazo zinafanya kazi za TPA.
“Tumebaini
kuwa kuna mgongano mkubwa wa kimaslahi ndani ya bandari, kuna
wafanyakazi wengine wana kampuni za mkononi ambazo hazijasajiliwa na
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) lakini zimepewa kazi za
TPA,” alisema.
Alisema kampuni hizo zinapomaliza muda wa mikataba yao huongezewa muda wa mikataba mingine.
Dk
Mwakyembe alisema kuna mtandao mkubwa unaofanywa kwa watu mbalimbali
kwa kushirikiana na vigogo wa bandari ili kufanikisha wizi katika
bandari.
“Kontena zinayeyuka, zinaibwa kama Twiga
walivyopandishwa kwenye ndege, ninaapa mtandao huu nitaumaliza hapa
bandarini,” alisema Mwakyembe huku akishangiliwa na wafanyakazi.
Aidha Mwakyembe amepiga marufuku utaratibu wa kuingia bandarini na kulipia kiingilio cha Sh200 unaojulikana kama potipasi.
“
Utaratibu huo ndiyo umekuwa ukisababisha wizi bandari, ni marufuku watu
wasiohusika kuingia bandarini, Sh200 wanazotoa zitatusaidia nini,”
alihoji Mwakyembe.
Hata hivyo alipongeza juhudi ambazo zimeanza
kuonekana katika mamlaka hiyo ya kuongeza mapato kila mwezi tangu
alipoisimamisha bodi hiyo.
Alisema mamlaka hiyo kabla ya mageuzi ilikuwa inakusanya mapato ya Sh28 bilioni lakini sasa inakusanya Sh50 bilioni kwa mwezi.
Aidha, Mwakyembe alisema watumishi wa bandari waliajiriwa kwa njia za ujanja ujanja watachunguzwa na hatimaye kufukuzwa kazi.
“Bandari
tumebaini kwamba kuna wafanyakazi wengi ambao wameajiriwa kwa undugu,
ujomba ujomba, tutawashughulikia katika siku chache zijazo,” alisema.
No comments:
Post a Comment