Wednesday, December 12, 2012

VURUGU ZATOKEA KATIKA MKUTANO WA KUKUSANYA MAONI HUKO Z'BAR PATA HABARI KAMILI


Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji warioba 


MIKUTANO ya kukusanya maoni ya upatikanaji wa Katiba Mpya Visiwani Zanzibar, imeingia dosari baada kuzuka ghasia na baadhi ya watu kujeruhiwa kwa kuchomwa visu.

Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa, zilitokana na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano iliyokuwa ikifanyika Unguja na kusababisha hofu za kiusalama.

Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni Shehia za Magomeni na Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.Hii ni mara ya kwanza ghasia kuzuka katika mikutano ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya visiwani humo.

Tukio la kuchomana visu, lilitokea katika Shehia ya Mpendae baada ya vurugu zilizosababishwa na vijana kuvamia mkutano uliokuwa ufanyike jana mchana.
Vijana hao walianzisha ghasia hizo baada ya kutaka kuvunja utaratibu uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae mbele ya wengine waliokuwa wametangulia katika mkutano huo.

Hatua hiyo ilipingwa na kuibua ghasia ziliozababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.

Tukio jingine lililovuruga mkutano huo ni lile lililotokea katika Shehia ya Magomeni, Jumatatu wiki hii baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya makundi mawili yenye misimamo tofauti juu ya mfumo wa Muungano; kuna wanaopinga na wanaoukubali.
Misimamo hiyo imeelezwa kujikita katika misingi na sera za vyama vyao vya kisiasa.
Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja kuwa na mamlaka kamili na Muungano uwe wa mkataba wakati, CCM kinasimamia kwenye Serikali mbili; Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Shehia ya Magomeni
Saa mbili kabla mkutano kuanza, watu wengi walifika Uwanja wa Mzalendo ambako mkutano ulitakiwa kufanyika. Walijipanga kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Tume ambao ni aliyewahi kufika ndiye anayetangulia kutoa maoni.

Hali hiyo ilisababisha wakazi wa Shehia hiyo waliokuwa wenyeji wa mkutano, kukosa nafasi ambayo ingewawezesha kutoa maoni kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema hawakuwa tayari kuwa wenyeji wa mkutano ambao hawatashiriki akisema waliokuwa wamejipanga wote walifikishwa kituoni hapo kwa magari kwa lengo maalumu la kuwakosesha wenyeji kutoa maoni yao, kwa kuwa inafahamika kuwa wengi wao ni wana CCM.

Hoja hizo alizitoa kwa wajumbe wa Tume ambao pia hawakuridhishwa na hali ya usalama katika eneo hilo kutokana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM na CUF.

“Kwa hali ilivyo, hatuwezi kupata utulivu utakaowezesha tufanye kazi kwa ufanisi na kumaliza mkutano kwa amani bila fujo. Natangaza rasmi kuwa leo hakuna mkutano,” Mwenyekiti wa Timu ya Tume hiyo inayokusanya maoni visiwani hapa, Profesa Mwesiga Baregu.

Akizungumza baada ya kuvunjika kwa mkutano huo, Salmin alisema waliokuwa wamefika kutoa maoni walikuwa wakitaka kunadi misimamo ya vyama vyao akisema hiyo ni hali ya kihistoria inayowakabili wakazi visiwani humo.
“Hata katika kupata huduma za kijamii, siasa inapewa kupaumbele na hili ndilo chimbuko la matatizo yote haya, ndiyo maana hata maoni yanayotolewa ni ya aina mbili, Muungano udumu au uwe wa mkataba na serikali mbili.

Dalili za vurugu
Dalili za kuwapo kwa vurugu zilianzia kwenye mkutano uliofanyika Jumatatu asubuhi kwenye Viwanja vya Kibanda Maiti katika Shehiya ya Kwa-Alamsha, ambako watu waliotaka Muungano ubaki, walizomewa huku waliotaka Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja ikiwa na mamlaka kamili, muungano uwe wa mkataba walishangiliwa.

Hali hiyo ilitawala mkutano huo bila kujali jitihada za Profesa Baregu kukemea mara kwa mara hali hiyo. Pamoja na kwamba maoni yatafanyiwa mchujo, Wananchi hao wanaamini kuwa upande utakaotoa maoni kwa wingi ndiyo utakaoshinda kwa matakwa yao kuingizwa kwenye Katiba Mpya.

Mbunge amshambulia Mratibu
Katika mkutano uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Wandarasi, Shehia ya Meya, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Faharia Shomari alimshambulia Mratibu wa shughuli za Tume visiwani humo, Ahmed Haji Saadat kwa maneno akiwambia:
“Mimi ni Mjumbe wa Tume ya Bunge ya Sheria na Katiba. Nilihusika kutunga sheria inayowaongoza kufanya kazi hii, inatakiwa wakazi wa shehia mnayofanyia mkutano watoe maoni kwa kuzungumza, wengine wapewe fomu; tatizo wewe unajidai mkubwa kuliko hata tume yenyewe. Mikutano yote umeivuruga wewe, tangu mwanzo nilikwambia, kiko wapi sasa,” alisema mbunge kwa hasira.

baada ya mashambulizi hayo, Saadat naye alijibu: “Mheshimiwa, ninakuheshimu sana, ikiwa tatizo unaliona ndani ya sheria na unakiri ulihusika kutunga sheria hiyo bila kueleza uzoefu ulionao kwa mazingira ya Zanzibar, wewe ni sehemu ya tatizo. Tangu nilipokuwa Mji Mkongwe umekuwa ukinifuata kwa maneno, tatizo lako hasa nini?”
Zogo hilo lilikuwa kubwa na kusababisha askari kumwondoa mbunge huyo kumpeleka pembeni. Lakini baada ya muda, mbunge huyo alijivuta mpaka alikokuwa Saadat na kuanza tena kumwandama kwa maneno akisema: “Kiko wapi? Jana hamkufanya mkutano kwa kujidai kwako, leo pia zogo hilo, huenda msiufanye kwa kujidai mkubwa lol, unajidai una nguvu kuliko hata wajumbe wa tume? Kiko wapi sasa?”
Maneno hayo yalimkera Mratibu huyo ambaye alimtaka athibitishe anayomtuhumu kwa maandishi.

Iliwalazimu askari polisi kuingilia kati tena kati na kumshauri Saadati kumfungulia mashtaka mbunge huyo.

Mbunge huyo alitoa maoni yake kwenye Jimbo la Mji Mkongwe, Vuga na kuhudhuria mkutano wa maoni uliyofanyika siku hiyo hiyo kwenye Hoteli ya Bwawani ambako inadaiwa kuwa ndiko alikoanza kuzozana na Saadat; akimtuhumu kupendelea wanaotaka muungano uwe wa mkataba na Serikali ya Zanzibar yenye mamlaka yake kamili.

Tuhuma hizo zilitokana na Saadat kukataa kuruhusu kundi la wanawake ambao Shomari alitaka wakatoe maoni tofauti na utaratibu uliowekwa ambao unampa nafasi aliyewahi kufika na kujipanga kwenye foleni kutoa maoni kwanza.

“Nimeishakuona unapendelea watu wa mkataba, subiri nitakuripoti kwa (mmoja wa wajumbe ambaye pia ni kada wa CCM),” Shomari alisikika akimweleza Saadat ambaye alimjibu kuwa kinachoangaliwa si nani wala itikadi gani, bali utaratibu uliowekwa tu.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...