Thursday, December 20, 2012

LEMA NA HATIMA YAKE YA UBUNGE KUJULIKANA KESHO


MBIVU na mbichi kuhusu hatima ya ubunge wa Godbless Lema katika Jimbo la Arusha Mjini zitajulikana kesho, wakati Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wa rufaa iliyokatwa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotengua ubunge huo.
Habari zilizopatikana jana kutoka mahakamani hapo zilisema kuwa jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo limeshakamilisha kuandika hukumu yake na kwamba itasomwa kesho kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Lema ambaye ni kada wa Chadema, alivuliwa ubunge Aprili 5, mwaka huu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalia kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa 2010.
Pamoja na kumvua ubunge, Jaji huyo pia alimwagiza Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuhusu Lema kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwa Kifungu cha 114 cha sheria ya uchaguzi ambacho kinamnyima kupiga au kupigiwa kura kwa kipindi cha miaka mitano.
Matumizi ya kifungu hicho ni miongoni mwa hoja zilizowasilishwa na Lema kupitia kwa mawakili wake akidai Jaji alikosea kwa sababu makosa yaliyomvua ubunge hayaangukii kwenye vitendo vya rushwa, kuzuia watu kupiga kura.
Jaji Rwakibarila alimvua Lema ubunge baada ya kuridhika kuwa alitumia lugha na kauli za udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian), inayoangukia kwenye Kifungu cha 113.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa mawakili wake Method Kimomogoro na Tundu Lissu alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akiwasilisha hoja 18 za kuipinga.
Hukumu ya Jaji Rwakibarila pia ilipingwa na mawakili wa Serikali waliokuwa wakimwakilisha Mwanasheria Mkuu katika shauri hilo, Timon Vitalis na Juma Masanja ambao wanadai haina hadhi ya kuitwa hukumu kutokana na kujaa dosari za kisheria.
Hata hivyo, wakati Lema akikata rufaa, warufaniwa; Mkanga, Mollel na Kivuyo nao waliwasilisha rufaa kupitia kwa Mawakili wao, Alute Mughwai na Modest Akida kupinga uamuzi wa Jaji Rwakibarila kutupilia mbali baadhi ya madai yao.
Lema na mmoja wa wakili wake, Kimomogoro jana walithibitisha kwa nyakati tofauti kupokea hati za kuitwa mahakamani kusikiliza hukumu hiyo.
Taarifa kwamba hukumu itasomwa kesho zilitawala Jiji la Arusha jana na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Katibu wa Mkoa, Amani Golugwa walionekana wakijiandaa kuelekea Dar es Salaam kusikiliza uamuzi huo.
Akizungumza kwa simu jana alasiri, Golugwa alisema ataongoza kundi la wanachama na viongozi zaidi ya 40 kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam leo.
Rufaa
Rufaa hiyo ilisikilizwa na jopo la Majaji, Salum Massati, Bernard Luanda wakiongozwa na Jaji Nathalia Kimaro.
Siku ya usikilizwaji upande wa wajibu rufaa waliweka pingamizi dhidi ya rufaa ya Lema, wakidai kuwa ilikuwa na dosari za kisheria, huku wakiomba Mahakama hiyo itupilie mbali bila kutoa nafasi yoyote ya kukatwa upya.
Katika uamuzi wake dhidi ya pingamizi hilo, Novemba 8, 2012 Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo ya Lema baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lakini ikatoa fursa ya kukatwa upya katika muda wa siku 14 kwa mujibu wa Kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama ya Rufani.
Baada ya kufanya marekebisho hayo ndani ya muda huo kama alivyoamuriwa na Mahakama, ilisikilizwa Desemba 4, 2012.
Hoja za warufani
Lema aliyeibuka na ushindi wa zaidi ya kura 19,000 dhidi ya Dk Burian, anadai Jaji Rwakibarila alimvua ubunge kwa kuzingatia ushahidi wa mdomo usio na nyaraka za kuuthibitisha kinyume cha sheria.
Alitoa hoja 18 kupinga hukumu hiyo na pia alimtuhumu Jaji Rwakibarila kutozingatia ushahidi wake na mashahidi wake watatu kwa madai kuwa walikuwa wanachama na viongozi wa Chadema, hivyo walikuwa na masilahi, lakini papohapo akakubali na kutumia ushahidi wa wanachama na viongozi wa CCM.
Kwa upande wake, Wakili Vitalis alidai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa Lema, kwa madai ya kutumia lugha za matusi, akidai kuwa Bunge limeruhusu wanasiasa kutukanana kwenye kampeni.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 108 cha Sheria ya Uchaguzi , Sura ya 313 ya 2010, matusi si miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kutengua matokeo ya uchaguzi na kwamba Bunge liliruhusu kutukana kutoka na kufanya marekebisho ya  Sheria ya Uchaguzi ya 1995 baada ya hukumu ya kesi kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Aman Walid Kabouru.
Vitalis alidai kuwa sheria ilikuwa ikiruhusu matokeo ya uchaguzi kutenguliwa kutokana na lugha za matusi, lakini baada ya hukumu ya kesi ya Kabouru Januari 1995, Julai mwaka huo Bunge lilifanya marekebisho na kuondoa suala la matusi katika mambo yanayoweza kutengua uchaguzi.
Pia alidai kuwa kifungu cha 108 (2) cha Sheria ya Uchaguzi kinaeleza aina za ubaguzi zinazokatazwa ni pamoja na wa kidini na kikabila na kwamba aina nyingine kama makazi (Uzanzibar, Ubara) hazijatajwa.
Wakili  Vitalis alidai kuwa wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa mrufani (Lema), kwa kasoro zilizotokea wakati wa kampeni kwa sababu hawakuwa wahusika katika mchakato wa kampeni za uchaguzi huo.
Vitalis alidai kuwa anayepaswa kufungua kesi mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule aliyetukanwa kwa kuwa hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata anapokufa, madai yake nayo hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu mwingine.
“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai lakini watu wengine ndiyo waje mahakamani kufungua kesi?” alihoji wakili huyo.
Warufaniwa
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili Mughway akidai kuwa si kweli kwamba Bunge limeruhusu kauli za matusi kwenye kampeni.
“Sikubaliani na maneno ya AG (kupitia Wakili Vitalis) kuwa ni ruksa wanasiasa kutukanana,” alisema na kusisitiza kuwa madhumuni ya kukataza vitendo hivyo ni kudumisha siasa safi na kuhakikisha nchi inatawaliwa na siasa safi.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 2 (2) (b), viongozi na wagombea hawatakiwi kutumia lugha za matusi wala kejeli za namna yoyote wala udhalilishaji wa namna yoyote.
Katika rufaa yao, warufaniwa hao walidai kuwa Jaji Rwakibalira alikosea katika hukumu yake kwa kuchanganya vituo vilivyotolewa ushahidi na mashahidi wanne na hatimaye akakataa ushahidi mmojawapo, pamoja na tarehe za ratiba ya kampeni za CCM na Chadema.
Pia walidai  Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata kama Lema kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk Burian ni mkazi wa Zanzibar, na hatafaa kwa hiyo  ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.

No comments:

Post a Comment

sikiliza ngoma zinazo kamata kwa sasa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...