FREEMAN MBOWE, MWENYEKITI CHADEMA
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiwaapisha wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Aprili 13 mwaka huu alionya kuwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya usifanywe kwa kuegemea udini, ukabila, ubinafsi, siasa ama kulenga kuvunja Muungano.
Anasema maoni ya wananchi lazima yaheshimiwe hata
kama hayataweza kuingizwa yote katika katiba hiyo, huku akiwataka
wajumbe hao kuweka pembeni maslahi ya makundi wanayotoka kwa kuwa kazi
wanayoifanya ni kwa maslahi ya taifa..
Tume hiyo ilianza kazi yake ya miezi 18, Mei mosi mwaka huu, ambapo mpaka sasa imeshakusanya maoni katika mikoa takribani 15.
Mbali na kukusanya maoni ya wananchi na
kutengeneza rasimu ya katiba, baadaye zitafuata hatua mbili muhimu
ambazo ni kuundwa kwa Bunge Maalumu la kuchambua rasimu hiyo, kisha
wananchi kupiga kura ya maoni.
Tume hiyo ya Katiba leo ndio inamaliza kukusanya
maoni ya Wananchi na kuanza kujipanga kwa taratibu nyingine za kumaliza
kazi yake.
Pamoja na maelezo hayo ya Rais Kikwete watu wa
kada mbalimbali likiwemo Jukwaa la Katiba Tanzania walipinga kwamba
Katiba mpya haiwezi kupatikana Aprili 18, 2014 kama serikali
inavyoeleza.
Wakipendekeza kwamba ili Katiba iweze kutumika ni lazima sheria nyingine zirekebishwe, zoezi ambalo huchukua miaka miwili.
Walisema kinachotakiwa kufanyika ni kurekebishwa
kwa Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa katika vipengele vinavyohusiana na
Tume ya Uchaguzi, ili uchaguzi wa mwaka 2015 uwe huru na wa haki,
kuacha mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ukiendelea kwa utaratibu
mzuri.
Hoja hiyo ilinaonekana kuwagusa wengi na sasa,
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
anasema jambo hilo linatakiwa kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
“Chadema tunaingiwa na hofu kwamba huenda Katiba
mpya isiwe tayari kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014 na
uchaguzi mkuu mwaka 2015” anasema Mbowe.
Anasema hakuna ulazima wa kupatikana kwa Katiba
mpya katika kipindi hicho, badala yake mchakato huo uendelee lakini
yafanyike marekebisho katika Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 ambayo
ndani yake kuna Tume ya Uchaguzi (Nec) na daftari la kudumu la
wapigakura.
“Kuna mambo yanatakiwa kufanyiwa kazi, kwanza ni
kuwa na Tume huru ya Uchaguzi na mchakato wa kupata tume hii ufanyike
bila kuathiri mchakato mzima wa kupata Katiba mpya.
“Tukienda katika chaguzi hizi mbili bila kubadili sheria
nyingine zinazogusa maisha yetu ya kila siku ikiwemo hii ya uchaguzi ni
wazi kuwa tutaingia katika machafuko, uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa
haki kama ukisimamiwa na muundo wa Nec hii inayoteuliwa na Rais” anasema
Mbowe.
Anasema vyama vya upinzani haviwezi kujiandaa na
Uchaguzi Mkuu ujao kwa sababu mpaka sasa havijui mfumo wa uchaguzi huo
utakuwa wa namna gani.
“CCM wao wanajua kila kitu na ndio maana hawana
wasiwasi, pia daftari la kupigia kura nalo ni tatizo kwa kuwa
halijafanyiwa maboresho,” anasema Mbowe.
Anasema licha ya mchakato wa Katiba kuendelea
huku serikali ikieleza wazi kwamba Katiba itapatikana kabla ya mwaka
2015, wao hawaiamini kwa kuwa siasa ni mchezo mchafu.
“Hatuna sababu ya kukiamini chama tawala katika
hili kwa sababu wanachokizungumza ni tofauti na wanachokifanya. Chama
chochote makini lazima kianze kujipanga mapema lakini kwa utaratibu wa
sasa hatuwezi kufanya hivyo,” anasema Mbowe na anaongeza;
“Tutafanya maandalizi kwa sheria ipi, hatujui
Muungano utakuwa wa aina gani, lakini pia hatujui tutakuwa na Tume ya
Uchaguzi ya aina gani na wala hatujui majimbo yatakuwa mangapi.”
Anasema kuwa kwa mara ya kwanza ilipotungwa sheria
ya mabadiliko ya Katiba, chama hicho kiliipinga na kutaka ifanyiwe
marekebisho katika sehemu tatu ambazo ni, muundo wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Bunge la Katiba na Kura ya Maoni.
“Pamoja na sheria hiyo kufanyiwa marekebisho lakini yaligusa sehemu moja tu kati ya hizo tatu,” anasema Mbowe.
Anasema hata kama Tume hiyo itamaliza kazi yake ya
miezi 18, bado kuna ulazima wa mchakato wa kubadili sheria mbalimbali
kuanza kufanywa.
“Chadema hatupingi mchakato wa Katiba Mpya, tume
iendelee na zoezi lake lakini wakati huohuo ufanyike mchakato wa
mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo zinaweza kutuletea matatizo
katika uchaguzi,” anasema Mbowe.
Anasema wanaipinga sheria ya uchaguzi ya mwaka
1985 kwa kuwa ilitungwa wakati nchi ikiwa katika mfumo wa chama kimoja
na hata Tume ya Uchaguzi nayo iliundwa kwa mfumo huo huo.
“Ili nchi iwe na uchaguzi huru ni lazima vyama
vyote vya siasa viwe na imani na Tume ya Uchaguzi, hata katika mechi
ya mpira wa miguu lazima timu ziwe na imani na refa, tusikubali
kuendelea kuwa na sheria mbovu kwa kigezo cha mchakato wa Katiba,”
anasema Mbowe
No comments:
Post a Comment